TUKIO la
wananchi kuchoma Kituo Kidogo cha Polisi cha Bunju A kilichopo wilayani
Kinondoni, jijini Dar mwishoni mwa wiki iliyopita lilizua mshtuko wa
aina yake na kuweka rekodi mbaya nchini, Uwazi linakupa habari kamili.
Chanzo cha wananchi hao kuchoma kituo
hicho kilielezwa kuwa ni baada ya mwanafunzi wa darasa la nne katika
Shule ya Msingi Bunju B aliyetajwa kwa jina la Tabia Omary (11) kugongwa
na daladala Julai 10, mwaka huu alipokuwa anavuka kuelekea shuleni.
Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo
aliyejitambulisha kwa jina la Miriamu Njuki, katika eneo lililotokea
ajali, alikuwepo askari wa usalama barabarani akisaidia watoto hao
kuvuka barabara kwa kusimamisha magari lakini dereva huyo wa daladala
alikaidi na kumgonga mwanafunzi huyo na kufariki papo hapo.
“Baada ya askari huyo kuona daladala
limefanya tukio hilo na kutosimama, ilibidi ajiongeze na kuanza
kukimbizana na nalo kwa kutumia gari lingine ambapo alifanikiwa
kumkamata dereva huyo,” alisema Miriamu.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo ambaye
hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema baada ya askari kumkimbiza
dereva huyo na kuuacha mwili wa marehemu barabarani kwa muda mrefu ndipo
wananchi hao walipopatwa na jazba na kwenda kuchoma moto kituo cha
polisi jambo ambalo halikuwa sahihi.
“Hakuna uhusiano wowote kati ya
mwanafunzi huyo kugongwa na kuchomwa kituo cha polisi kwa sababu kituo
chenyewe kipo umbali mrefu na eneo alipogongewa mwanafunzi huyo,
walikuwa na chuki zao tu,” alisema mkazi huyo.
Imeelezwa kuwa wananchi hao baada ya kuchoma moto kituo, wengi wao walikimbilia mikoani kukwepa kukamatwa.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule
Msingi Bunju B, Ezekiel Johnson, amesema kukosekana kwa matuta katika
eneo hilo kunachangia ajali nyingi kutokea.
“Mpaka sasa wameshagongwa watoto wanne
na kati yao, wawili wamepoteza maisha na wawili wamepata ulemavu wa
kudumu tangu mwaka huu uanze,” alisema mwalimu huyo.
Katika tukio hilo, wahalifu hao licha ya
kupasua vioo na kuiba spea za magari kadhaa yaliyokuwepo kituoni hapo,
walifanya uharibifu mkubwa katika gari la mwanamke aliyetambuliwa kwa
jina la Husna Shabani
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck
Sadick aliyekwenda kushuhudia tukio hilo alieleza masikitiko yake kwa
wananchi waliochukua sheria mkononi na kumuagiza Kamanda wa Polisi, Mkoa
wa Kipolisi Kinondoni, Camilius Wambura kuhakikisha watuhumiwa wote
wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Jeshi la polisi linawashikilia zaidi ya
watu 32 kwa tuhuma za kukichoma kituo hicho na upelelezi unaendelea.
Marehemu Tabia alizikwa Jumamosi iliyopita katika mtaa wa Chalinze Bunju
B ambao ndugu, jamaa na marafiki waliokuwa na simanzi waliangua vilio
kwa kuondokewa na mpendwa wao huyo.
No comments:
Post a Comment