RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema uteuzi wa mgombea wa
CCM katika nafasi ya rais wa Jamhuri ya Muungano katika uchaguzi mkuu,
Dk John Magufuli ndio chaguo sahihi la kupambana na upinzani na kuleta
ushindi katika CCM na kushika dola.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwasili Zanzibar
kutoka Dodoma, Dk Shein alimtaja Magufuli kama kiongozi hodari muaminifu
mwenye shauku kubwa ya kuleta maendeleo ya nchi yake.
Dk Shein katika mkutano mkuu uliomalizika Dodoma hivi karibuni
Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi imemwidhinisha kuwania nafasi ya
urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM tayari kupambana na chama kikuu cha
CUF.
Alisema, Magufuli katika nyadhifa mbalimbali alizoshika ameonesha
uhodari wa kuchapa kazi na uzalendo pamoja na kusimamia majukumu yake
pamoja na walio chini yake. Alifahamisha kwamba ndiyo kigezo sahihi cha
kupambana na wapinzani na kuleta maendeleo ya wananchi wa Tanzania.
‘’Mimi namfahamu vizuri sana Magufuli nimefanya kazi naye katika
kipindi cha miaka 9 katika baraza la mawaziri nikiwa makamu wa
rais......ni mchapa kazi hodari, mwadilifu mwenye mapenzi makubwa na
wananchi wake,’’alisema.
Kwa mfano alisema katika Wizara zote alizopata kufanya kazi alionesha
uwezo wa ubunifu wa kuleta maendeleo akizitaja Wizara ya Uvuvi pamoja
na Ujenzi.
Aidha alimpongeza kwa kumteua Samia Suluhun Hassan, Waziri wa Nchi
Ofisi ya Makamu wa Rais kuwa mgombea mwenza huku Chama Cha Mapinduzi
kikiweka rekodi ya kuwa na mgombea mwenza mwanamke.
Alisema Samia ameonesha uwezo wa kazi katika nafasi mbalimbali
alizopata kuzishika tangu akiwa katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
hadi Muungano.
Alifahamisha kwamba Demokrasia ndani ya Chama Cha Mapinduzi
imeimarika kwa kiwango kikubwa ambapo nafasi za wanachama mbalimbali
kugombea nafasi za juu za uongozi ni kubwa sana ikiwemo wanawake.
Kwa mfano, alisema Chama Cha Mapinduzi kimeweka historia kubwa ya
kuteua wanawake wawili kuingia katika hatua ya mwisho ya uteuzi wa tatu
bora. ‘’Hicho ndicho Chama Cha Mapinduzi demokrasia yake katika makundi
mbalimbali imekuwa kwa kiwango kikubwa ikiwemo wanawake kushirikishwa
katika mchakato wa hatua za mwisho na kushika nafasi ya mgombea
mwenza,’’ alisema.
Alipoulizwa kuhusu wingi wa wagombea wa nafasi ya juu ya urais,
alisema demokrasia katika Chama Cha Mapinduzi imepanuka kwa kiwango
kikubwa tofauti na vyama vyengine vya siasa.
Alisema katika mchakato wa nafasi ya urais jumla ya wanachama wa CCM
42 walijitokeza kuwania nafasi hiyo tofauti na miaka ya 2000 ambapo
walijitokeza wanachama 17. ‘’Chama Cha Mapinduzi kinajengwa kwa nguvu ya
msingi mmoja mkubwa ambao ni demokrasia iliyopevuka inayotoa makundi
mbalimbali ya wanachama kuwania nafasi za juu za uongozi,’’alisema.
Akisoma risala ya wananchi wa mikoa sita kichama, naibu katibu mkuu
wa Umoja wa Vijana (UVCCM Zanzibar), Shaka Hamdu alisema wamefurahishwa
na maamuzi ya vikao vya chama kuwateuwa wagombea wa nafasi za juu za
urais kwa upande wa Jamhuri ya Muungano na Zanzibar.
Shaka alisema wanachama wa CCM Zanzibar wanaunga mkono uteuzi huo wa
majina ya viongozi hao ambao watapeperusha bendera ya chama kuelekea
uchaguzi mkuu wa mwaka huu na kukileta ushindi chama.
‘’Wanachama wa mikoa sita matumaini yao makubwa kwamba wagombea wa
nafasi za urais kuanzia John Magufuli nafasi ya urais wa Muungano pamoja
na Dk Ali Mohamed Shein kwa nafasi ya urais wa Zanzibar kwamba ni
uteuzi sahihi wa wagombea wenye sifa watakaokiletea chama
ushindi,’’alisema.
Mamia ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi na wananchi kwa ujumla
wamejitokeza katika mapokezi ya mgombea wa urais wa Zanzibar kuanzia
uwanja wa ndege wa Abeid Amaan Karume hadi katika makao makuu ya CCM
Kisiwandui.
No comments:
Post a Comment