Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumatano ya Tarehe 27 May 2015


Vita Dhidi ya Madawa ya Kulevya ni Ngumu - Kikwete

Rais Kikwete amewaongoza watanzania katika maadhimisho ya siku ya kupinga matumizi ya dawa za kulevya duniani yaliyofanyika kitaifa mjini Bagamoyo katika viwanja vya shule ya msingi Mwanamakuka.

Shughuli hizo zilianza kwa maandamano katika viwanja hivyo ambapo badaye mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo alimkaribisha Rais pamoja na wananchi waliohudhuria katika viwanja hivyo.

Katika hotuba yake, Rais Jakaya kikwete alisema vita dhidi ya madawa ya kulevya ni kubwa na inahusisha wafanyabiashara wakubwa ambapo fedha zinazopatikana hutumika kufadhili uhalifu wa kimataifa ikiwemo ugaidi.

Rais Kikwete alisema anajivunia kutungwa kwa sheria mpya ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya ya mwaka 2015 katika serikali ya awamu ya nne, ambayo inaweka masharti ya kuundwa kwa chombo maalum kitakachoshughulikia kwa ukaribu tatizo hilo, na kwamba anataka chombo hicho kiwe kimeundwa kabla ya Oktoba ili kutoa baraka zake kabla hajaondoka madarakani, na atamkabidhi Rais ajaye aendelee kuanzia hapo.

Awali Waziri wa Afya na ustawi wa jamii, Dkt Seif Rashid alipata fursa ya kufafanua mikakati ya serikali katika kupambana na tatizo la matumizi ya madawa ya kulevya na kuwapiga vita wafanyabiashara wanaojihusisha na dawa hizo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi isiyokuwa ya serikali inayojishughulisha na masuala ya vijana Tanzania Youth Aliance TAYOA, Peter Masika alisema kwamba wamezindua namba ya simu itakayotumika kuwaelimisha vijana dhidi ya athari ya matumizi ya madawa ya kulevya.

Wakati huo huo mwanaharakati anayepambana na matumizi ya madawa ya kulevya Rehema Chalamila – Ray C aliwataka vijana wenzake waliojitumbukiza katika janga hili waweze kufuata mfano wake na wajitokeze kutokomeza janga hili kwa kutumia dawa za Methadoni na kuacha kabisa madawa.

Katika maadhimisho hayo ambayo yaliyoongozwa na kauli mbiu ya tujenge jamii na maisha ya utu bila dawa za kulevya, Rais kikwete alihimiza ushirikiano kwa jamii katika kupinga matumizi ya dawa za kulevya kwa vijana na kutokomeza biashara hiyo ikiwemo utoaji wa elimu ya kutosha kwa jamii ili kuwasaidia vijana walioathirika na dawa za kulevya.

Timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 15 kujinoa MBEYA

Timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 15 kujinoa MBEYA
Kikosi cha timu ya Taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 15 kinatarajia kusafiri kuelekea jijini Mbeya kwa ajili ya mchezo wa kirafiki na timu kombaini ya mbeya chini ya miaka 15.
Timu hiyo ya vijana ambayo inanolewa na kocha Bakari Shime, itaondoka na kikosi cha wachezaji wa thelathini ambapo wanatarajiwa kucheza michezo miwili ya kirafiki na timu ya kombani ya mkoa wa Mbeya ya vijana wenye umri chini ya miaka 15.

Timu itacheza michezo ya kirafiki siku ya jumapili na jumatatu ambapo kocha Shime atatumia nafasi hiyo kutambua uwezo wa wachezaji wake na kuongeza wachezaji wengine watakaonekana kutoka katika kombani ya mkoa wa Mbeya.

Mwezi ujao kikosi cha timu hiyo ya vijana chini ya miaka 15 kitaelekea kisiwani Zanzibar kucheza michezo ya kirafiki na timu za kombaini ya Zanzibar kisha baadae kuendelea na ziara ya kucheza michezo ya kirafiki katika mikoa ya Iringa, Morogoro, Tanga, Arusha, Mwanza na Dodoma.

Lengo la TFF ni kuhakikisha Tanzania inakua na kikosi bora cha timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 kitachoshiriki kuwania kufuzu kwa fainali za vijana Afrika wenye umri chini ya miaka 17 mwaka 2017 nchini Madagascar.

Walimu washauri kuanzishwa kwa mtaala wa afya ya uzazi

BAADHI ya walimu wa shule za msingi na sekondari mkoani Rukwa wameelezea umuhimu wa serikali kuanzisha mtaala wa mafunzo ya afya ya uzazi na ujinsia kwa ajili ya wanafunzi wote nchini ili kuwezesha kuelewa fursa sawa kwa mwanamke na mwanaume katika kushiriki uboreshaji wa afya ya jamii na shughuli za kimaendeleo na kiuchumi

WALIMU hao kutoka katika halmashauri za wilaya za NKASI KALAMBO na SUMBAWANGA wameiambia TBC kwa nyakati tofauti wakati wa maandalizi ya kuukabidhi mradi wa mpango wa Afya ya uzazi na ujinsia-TMEP-kwa serikali ya mkoa wa Rukwa, kuwa tofauti kubwa ya kupata haki za kimsingi kati ya mwanamke na mwanaume inachangia kuzorota kwa shughuli za maendeleo

WAMESEMA kutolewa kwa elimu hiyo kwa wanafunzi wote nchini tofauti na ilivyokuwa sasa kwa mikoa miwili ya mradi ya Rukwa na Singida kutawawezesha wanafunzi hao kuepukana na mimba za utotoni sambamba na kuelewa majukukumu sawa kwa mwanamke na mwanaume kwa ajili ya ustawi bora wa jamii

Kafulila ang’ang’ana mabehewa feki

MBUNGE wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR Mageuzi) ameitaka Serikali kuwasilisha bungeni taarifa ya kashfa ya ununuzi wa mabehewa feki katika Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na kusababisha hasara ya Sh bilioni 230.
Baada ya kipindi cha maswali na majibu bungeni jana, mbunge huyo alisimama kuomba muongoza wa Spika kwamba kutokana na unyeti wa jambo hilo, ikiwa ni pamoja na madai kwamba Kampuni iliyopewa zabuni ya kuagiza mabehewa hayo haikuwa na uwezo huo, kwa nini suala hilo lisipelekwe bungeni kujadiliwa.
Mbunge huyo alihoji kwamba si vyema suala hilo likazungumzwa na kuishia nje ya Bunge badala ya kujadiliwa na kupata ufumbuzi, lakini akijibu muongozo huo Spika wa Bunge, Anna Makinda alisema jambo hilo ni la kisekta na kwamba lilitakiwa lianzie kwenye kamati inayohusika.
Hata hivyo, akichangia muswada wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2015 wenye lengo la kuzifanyia marekebisho sheria 16 zinazohusu masuala ya fedha, kodi, ushuru na tozo mbalimbali nchini uliowasilishwa jana na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, mbunge huyo alirudia suala hilo la TRL akisema kuna haja ya jambo hilo kufanyiwa kazi kwani matumizi mabovu ya sh bilioni 230 hayawezi kufumbiwa macho.
Alisisitiza taarifa ya jambo hilo ipelekwe bungeni na kuhoji kampuni hiyo iliyohusika na kuagiza zabuni hiyo imelipwaje fedha zote hizo kabla ya kutimiza masharti na kumuomba Spika Makinda aagize taarifa iwasilishwe bungeni na sio kuwalinda.
Kauli hiyo ya kuwalinda ilimfanya Spika Makinda kusimama na kusema halindi mtu na kumtaka mchangiaji ajielekeze katika hoja husika.
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta wakati akifanya majumuisho ya bajeti yake Mei mwaka huu, alisema maofisa watano wa serikali wanatarajiwa kupandishwa kizimbani hivi karibuni, kutokana na kashfa ya uagizaji wa mabehewa 274 kutoka India, huku wengine wakitarajiwa kuchukuliwa hatua za kiutawala.
Aprili mwaka huu, Sitta alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Kipallo Kisamfu na wengine wanne, ili kupisha uchunguzi wa kashfa ya uingizaji wa mabehewa feki ya mizigo.
Wengine waliosimamishwa kazi ni Mkuu wa Mitandao, Ngosomwile Ngosomiles, Mhasibu Mkuu, Mbaraka Mchopa, Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Jasper Kisiranga na Meneja Mkuu wa Manunuzi, Ferdinand Soka.

Ahadi za Kikwete za ujenzi kutekelezwa zote

MIRADI yote ya barabara na madaraja ambayo Rais Jakaya Kikwete ameahidi kuitekeleza, itafanyiwa kazi na kukamilishwa kwa wakati, imeelezwa.
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, alisema hayo jana, akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum-CHADEMA, Susan Kiwanga, aliyetaka kujua ni lini ahadi ya Rais Jakaya Kikwete ya kujenga barabara ya kutoka Kidatu kwenda Morogoro itatekelezwa.
Akijibu, Dk Magufuli alisema kuwa, ahadi yoyote inayotolewa na Rais katika eneo lolote nchini, kwa mawaziri wa Serikali hilo ni agizo na watendaji wake watahakikisha zinatekelezwa.
Dk Magufuli alisema, ujenzi wa barabara hiyo utaanza pindi usanifu wa kina utakapokamilika na baada ya kumalizika kwa ujenzi wa daraja la mto Kilombero.
Akijibu swali la Mbunge wa Mpanda Vijijini, Moshi Kasoko, kuhusu ujenzi wa barabara inayounganisha mkoa wa Kigoma na Katavi Waziri Magufuli alisema Serikali imetenga Sh bilioni 751 ili kuanza utaratibu wa ujenzi wa barabara hiyo.
Dk Magufuli pia alimhakikishia Mbunge wa Meatu (CHADEMA), Meshack Opulukwa, kuwa serikali inajenga daraja la mto Sibiri na kwamba mkandarasi alisimama kwa muda tu kusubiri mafuriko yapungue.
Kuhusu swali la msingi lililoulizwa na Mbunge wa Mpanda Mjini, Said Arf (CHADEMA), lini barabara ya lami kuunganisha wilaya ya Mpanda, Mlela, Sikonge na Tabora, itajengwa Dk Magufuli alijibu kuwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara hiyo ya kilomita 364 kutoka Mpanda kwenda Tabora umekamilika.
Alisema, “Serikali inakamilisha mazungumzo na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), iliyokubali kutoa fedha za mkopo kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Km 334, kwa kiwango cha lami, kutoka Mpanda hadi Pangale (Tabora)”.
“Pia Serikali kwa kutumia fedha za ndani, imeanza kujenga sehemu ya Pangale–Tabora yenye urefu wa Km 30”
©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved