Dk Winnie Mpanju-Shumbusho |
Uteuzi huo wa Dk Mpanju unaanza Juni mosi, mwaka huu na ulitangazwa wakati wa kikao cha Baraza la WHO lililofanyika Mei 18 hadi Mei 26, mwaka huu Geneva, Uswisi.
Kutokana na uteuzi huo, Dk Mpanju sasa ataongoza Kitengo cha WHO kinachoshughulikia Ukimwi, kifua kikuu, malaria na magonjwa yasiyopewa kipaumbele.
Atafanya kazi hiyo kwa kushirikiana na nchi husika katika kudhibiti magonjwa hayo, hivyo kutoa mchango katika maendeleo na mafanikio ya Malengo ya Milenia na Malengo Endelevu ya Maendeleo.
Dk Mpanju ana uzoefu wa zaidi ya miaka 30 katika nafasi za juu za uongozi wa masuala ya afya, afya ya jamii, ushirikiano wa kimataifa na elimu kwa ujumla.
Kabla ya uteuzi huo, Mpanju alikuwa Mkurugenzi katika ofisi ya Mkurugenzi Msaidizi wa WHO anayeshughulikia Ukimwi, kifua kikuu, malaria na magonjwa yasiyopewa kipaumbele Chini ya uongozi wake, WHO ilisaidia nchi zinazoendelea, hasa zile zinazotishiwa na magonjwa, kupata misaada ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 10 kutoka Mfuko uitwao Global Fund, kugharimia programu za kitaifa za kupambana na Ukimwi, kifua kikuu na malaria, na programu za tiba na kinga za kuboresha afya ya uzazi, mama na mtoto.
Pia, Dk Mpanju amewahi kuwa Mkuurugenzi Mkuu wa Sekretatieti ya Masuala ya Afya ya Jumuiya ya Madola kwa ajili ya nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika. Ofisi za sekretarieti hiyo zipo Arusha, Tanzania.
Amewahi kuwa mjumbe wa bodi mbalimbali za kitaifa na kimataifa, ikiwemo Global Fund kwa ajili ya kupambana na Ukimwi, kifua kikuu na malaria na Bodi ya Mamlaka za Maji Mijini nchini Tanzania.
Dk Mpanju-Shumbusho ana Shahada ya Udaktari kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Shahada ya Uzamili katika Afya ya Jamii kutoka Chuo Kikuu cha Tulane, New Orleans, Marekani.
Pia ana Shahada ya Uzamili ya Udaktari kuhusu Watoto na Afya ya Watoto ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Dk Mpanju ameolewa na ana watoto.
No comments:
Post a Comment