JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limekamata kontena
likiwa na rola 15 za nyaya za umeme mali ya Shirika la Umeme Tanzania
(Tanesco) zenye thamani ya Sh milioni 150.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Kamishna wa Polisi
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Simon Sirro, alisema nyanya hizo ziliibwa
Februari 26 zikiwa zinasafirishwa kuelekea mkoani Kagera kwa ajili ya
Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Alisema baada ya wizi wa kontena hilo, kesi ilifunguliwa katika Kituo
cha Polisi Buguruni na watuhumiwa watano kukamatwa na kufikishwa
mahakamani.
Aliongeza kuwa wakati upelelezi ukiendelea Mei 25 mwaka huu, polisi
walipokea taarifa kutoka kwa msiri kwamba maeneo ya Kibamba mtaa wa
Kibengewe kuna kontena katika kiwanda cha kutengenezea matofali.
Alisema askari walifika eneo la tukio na kukuta kontena hilo lenye
namba 00LU2876031 na kumhoji mlinzi wa eneo hilo ili kumpata mmiliki wa
eneo na kontena hilo.
“Tunashukuru ilipofika saa 5:00 usiku tulifanikiwa kumpata mmiliki wa
eneo hilo, Donesia Aidan (40) ambaye ni mfanyabiashara mkazi wa Mbezi
makabe,” alisema Sirro.
Alisema taratibu zilikamilika na askari walifungua kontena hilo na
zilikutwa rola za nyaya zipatazo 15 kati ya 17 zilizokuwepo katika
kontena hilo siku lilipokuwa likisafirishwa.
Pia alisema jeshi la polisi lilifanikiwa kumkamata mtu mwingine
anayehusika katika wizi wa kontena hilo, Prosper Mtei (43) ambaye ni
mfanyabiashara na upelelezi unaendelea ili aweze kuunganishwa na
watuhumiwa wengine katika kesi ya msingi.
No comments:
Post a Comment