Nyalandu atangaza nia, kuchukua fomu leo

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgeIrUjl2zrv1vBrIZt7221tRQaJfJkxZo944ivrYSV_FVaq7gjd6QzK_jSdG7CEa4Vk6BXp_qIxAVr0jY6PDzLPL9BOjSj0JR2uJvw6gp8dfFqYSX0FZAKKqFfN9LVgiNpZUCObwxulEA/s1600/MUSOMA+UTALII.6.jpg
 Waziri Wa Maliasili Na Utalii Lazaro nyalandu
MAKADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wameendelea kupigana vikumbo katika kutangaza nia na kuchukua fomu kuwania uteuzi wa kugombea urais wa Tanzania, akiwemo Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu aliyetangaza nia jana mkoani Singida.
Uwezekano wa kufikia wagombea 30 kwa sasa ni mkubwa maana waliochukua fomu Dodoma wamefikia wagombea 15, wakiwemo makada wasio na majina makubwa; Wakili wa Mahakama Kuu, Godwin Mwapango aliyekuwa wa 15 kuchukua fomu jana na Peter Isaiah Nyalali, anayetarajiwa kuchukua fomu leo.
Alipozungumza kwa kifupi na waandishi wa habari jana, Mwapango aliwahimiza wanaCCM wengine kujitokeza kwa wingi kutumia haki hiyo ya Kikatiba kuomba ridhaa ya kuteuliwa kuwania urais wa Tanzania. “Niwatie moyo wale ambao wana nia lakini wanakatishwa tamaa, waje wachukue fomu.
Nawaomba wasikilize sauti iliyo mioyoni mwao na waitikie sauti hiyo na dhamira zao. Usitishwe, usikatishwe tamaa,” alisema Wakili Mwapango mwenye umri wa miaka 43.
Alisema hakutaka kutangaza nia kwa sababu ya kuogopa kukatishwa tamaa, lakini sasa akiwa na fomu hiyo ataweka hadharani mipango yake kwa waandishi wa habari kesho jijini Dar es Salaam.
Alisema yeye au mwenzake atakayefanikiwa kushinda uteuzi ndani ya CCM na kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, hana budi kuendeleza utamaduni wa kuwapa nafasi hata wanachama wa kawaida kama yeye kuomba uteuzi huo wa nafasi ya juu ya nchi.
Nyalandu Akihutubia Watanzania katika mkutano uliorushwa moja kwa moja kutoka Singida, Nyalandu kwanza alielezea rekodi yake nzuri ya utendaji serikalini, ikiwamo kupambana na ujangili wa tembo, ambao alisema umesaidia kuongezeka kwa wanyamapori hao muhimu kwa utalii, kwa kiasi kilichoshitua jumuiya ya kimataifa.
Nyalandu anayetarajiwa kuchukua fomu ya kugombea urais leo mjini Dodoma katika makao makuu ya CCM, alisema anaomba ridhaa ya CCM kwa kuwa anajua kuwa sera za nchi zipo vizuri, lakini kinachohitajika ni jitihada kidogo za kuzisimamia ili Taifa lifike katika hatua ya kuwa uchumi wa kati.
Alitaja kipaumbele chake kuwa ni amani na upendo na kuwataka Watanzania waliokuwa wakimsikiliza, kusimama kwa muda, ili kuwakumbuka waasisi wa Taifa hili waliotangulia mbele ya haki, kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kuleta Watanzania pamoja.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved