Simba yamvutia pumzi Singano


https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhO75cszZiaFwlACSFsEaH2C3gsZj1VDm0-QG8LIOhSdarGHM75h4OvCsxuNF-J0KQwJWFxpAugw_HvSxinGBC4wFKxgC0EgzVKoXPUdrTr5oQ8sYQDTbuEIIZzTYq8e6Ver1uKa6SdAlqF/s1600/3.jpg
Ramadhani Singano `Messi’
UONGOZI wa klabu ya Simba umesema kuwa, tamko la kumuadhibu mchezaji wao Ramadhani Singano `Messi’ watalitoa baada ya pande hizo mbili kukutana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
TFF juzi ilikiri kusikitishwa na mgogoro uliopo kati ya uongozi wa Simba na mchezaji huyo chipukizi mwenye kipaji cha hali ya juu. Habari kutoka chanzo kilicho karibu na uongozi wa Simba kilisema jana kuwa, uongozi huo utatoa tamko la adhabu baada ya kikao chao, Messi na TFF, Jumanne.
Kwa muda sasa mchezaji huyo na uongozi wa Simba wako katika mgogoro wa kimkataba, ambapo mchezaji huyo amekuwa akisisitiza kuwa anakaribia kumaliza mkataba wake wakati uongozi ukisema bado mwaka mmoja.
Messi amekuwa akipinga kuwa alisaini mkataba wa miaka mitatu Simba huku akisisitiza kuwa ni miaka miwili, mkataba ambao unamalizika mwaka huu. Simba ina mkataba wa miaka mitatu ambao ulisainiwa na Mei mosi mwaka 2013 na unamalizika Julai 1, 2015.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari juzi TFF, kupitia Mkurugenzi wa Ligi, Boniface Wambura, imeagiza mwakilishi wa klabu ya samba pamoja na Messi wafike katika Ofisi za Shirikisho hilo Jumanne, Juni 9 kwa mazungumzo.
“Katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye mazungumzo hayo, TFF inaziasa pande zote mbili (klabu na mchezaji), Zijiepushe kutoa matamko yanayoweza kuchochea hali ya kutoelewana na kuamsha hisia mbaya katika familia ya mpira wa miguu Tanzania,” ilieleza taarifa hiyo.
Messi amekuwa akisema kuwa mkataba wake na Simba ulimalizika mwishoni mwa msimu uliopita na sasa anahitaji mkataba mpya au apewe ruhusa ya kuondoka.
Pia Messi hivi karibuni alikaririwa akisema kuwa Simba imekuwa ikimlipa kidogo tofauti na kazi kubwa na yenye thamani anayoifanya katika timu hiyo.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved