![]() |
Spika wa Bunge, Anne Makinda |
Dar es Salaam. Spika Anne Makinda amesema endapo Watanzania wataendekeza itikadi za udini na ukabila, Taifa litagawanyika na hakuna atakayenusurika na machafuko.
Makinda alisema kinachosikitisha kwa sasa ni uongo unaopandikizwa na wanasiasa juu ya tofauti mbalimbali zinazojitokeza, kama ilivyokuwa kwenye mchakato wa Katiba.
Kauli hiyo aliitoa jana wakati wa ibada ya maziko ya mbunge wa Ukonga (CCM), Eugen Mwaiposa aliyefariki dunia siku tano zilizopita kwa shinikizo la damu.
“Kuna kundi la watu wasioitakia mema nchi yetu, lakini hawana hoja. Wanasambaza na kuwapandikizia uongo wananchi, kwa mfano walieneza uongo kwenye Katiba Watanzania wakajigawa. Tusipokuwa makini tutagawanyika,” alisema Makinda.
“Ni ajabu sana mtu mwenye elimu na vyeo vyake akaonekana kuwa sehemu ya kuleta mpasuko kwenye jamii, lakini huyo ni shetani tu kwani tunaamini Mungu yupo…ni vyema kila mtu afikirie mchango wake katika jamii.”
Alikuwa akisisitiza maneno yaliyotolewa na Msaidizi wa Askofu wa kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Chediel Lwiza ambaye alimzungumzia Mwaiposa kuwa ni mtu asiye na ubaguzi, muadilifu na aliyejihusisha na jamii kwa karibu bila kujali makundi yao.
Mwaiposa jana alizikwa nyumbani kwake na wabunge walioongozwa na Spika Makinda, mameya na wakuu wa wilaya za Mkoa wa Dar es salaam.
Awali Askofu Lwiza alitoa tahadhari kwa Watanzania kuchagua kiongozi makini atakayelivusha Taifa kwenye mpasuko wa udini na ukabila.
Alionyesha masikitiko yake akisema kwa sasa hatari ukabila na udini, imeshaanza kuonekana kwenye jamii hususani katika kipindi cha uchaguzi.
“Sasa hivi wananchi wamekuwa hata wakiangalia kwanza dini au kabila kabla ya kumchagua mtu, baadaye wanaangalia undugu na ujamaa,” alisema huku akitoa mfano:
“Udini na ukabila unaanza kwa kutafuna kama mchwa, baada ya muda unaona matokeo yake, kwa Rwanda na Burundi hali ilikuwa hivyo na kauli ya mtu mmoja tu ndiyo iliyoathiri machafuko kwa Taifa zima, kwa hivyo lazima tuwe makini kwani tunayo bahati ya kuachiwa msingi wa umoja na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.”
Chediel alitoa tahadhari katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, akiwataka Watanzania kumtanguliza Mungu ili kupata kiongozi bora.
“Uchaguzi huu ni muhimu sana, tuangalie kiongozi gani atakayetuleta katika umoja, kutuondolea makundi na mipasuko inayojitokeza,” alisema.
Katika msiba huo pia alikuwepo Makamu wa Rais, Dk Gharib Bilal na Waziri wa Kilimo na Chakula, Stephen Wasira.
Juzi, Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Ilala, Assah Simba na Mwenyekiti wa CCM, jimbo la Ukonga, Abdulah Kidulaza walisema kifo cha Mwaiposa ni pigo ndani ya chama na jimbo hilo.
Chanzo Mwananchi
No comments:
Post a Comment