Mambo Yalivo Kuwa Uwanja Wa Kumbukumbu Sheikh Amri Abeid


May 30 2015 inakuwa siku ambayo inaingia kwenye Historia kubwa kwenye ishu za siasa Tanzania.. Bado miezi michache ufanyike Uchaguzi Mkuu, mmoja ya watu ambao walitajwa sana na kuwa kwenye headlines kubwa kwenye vyombo  vya habari ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa.Ngoyai
DSC_0166
Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid katikati ya Jiji la Arusha umeshuhudia kwa mara nyingine kujaa kwa watu ambao walikuja kwa ajili ya kushuhudia Mbunge huyo akitangaza nia rasmi kabisa kwamba atagombea Urais mwaka huu.
“Watanzania wanahitaji mabadiliko, nina uwezo wa kusimamia mabadiliko hayo.. Mwalimu Nyerere alisema Watanzania wasipoyapata mabadiliko hayo ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM. Sina shaka tukijipanga vizuri ndani ya CCM tunaweza kuwapa Watanzania mabadiliko wanayoyataka”>>> Edward Lowassa.
“Nchi yetu inahitaji viongozi wenye sifa hizi.. uongozi wenye uthubutu usioogopa kufanya maamuzi magumu, uongozi usioyumba.. Aweze kuwaunganisha Watanzania na kutoa utofauti kati ya walio nacho na wasio nacho“>>> Edward Lowassa.
“Nina hamu, nina shauku na nina uwezo wa kuiongoza Tanzania… Ninaamini nina kila kigezo cha kuibeba dhamana ya nchi yetu.. Katika vitu ninavyojivunia ni pale nilipoenda kupigana vita ya Kagera, nilishiriki kikamilifu nikiwa miongoni mwa askari wa mbele kuikomboa nchi yetu, muwaulize wengine waliwahi hata kufika Kagera?”
“Kwa wingi wa rasilimali tulizonazo tuna kila sababu ya kuwa ombaomba… Haya ninayoyaeleza ndio msingi wa utendaji wa Serikali nitakayoiongoza nikichaguliwa.. nimeamua kugombea Urais ili kupambana na umaskini.. Uongozi wangu utaleta mchakamchaka wa maendeleo”– Edward Lowassa.
“Najua Watanzania wangapi wanaishi kwa bodaboda, mama ntilie.. hawa ni rafiki zangu hawatafukuzwa barabarani.. ni raia wa Tanzania wanaostahili kula kama wewe“
“Kwenye michezo tumechoka kuwa kichwa cha mwendawazimu, tutaibadili hali hii kwa kasi sana“>>> Edward Lowassa.
DSC_0176
DSC_0184




Huu ndio mwonekano wa Headlines chache za Magazetini leo MAY 29 2015, utaweza kuzisoma zotezote ukiingia hapa>>>http://millardayo.com/magazeti-2905tza/

Ahadi ya JK kwa walimu

Ahadi ya JK kwa walimu                                AHADI ya Rais Jakaya Kikwete ya kushughulikia changamoto za walimu kabla ya kumaliza muda wa uongozi wake mwishoni mwa mwaka huu, inatarajiwa kuanza kutekelezwa mwezi ujao.
Tayari Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, limeelezwa kuwa zaidi ya walimu 80,000 watanufaika na malipo ya malimbikizo ya madeni mbalimbali yatakayofanyika mwisho mwa mwezi ujao.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Kassim Majaliwa alisema hayo bungeni jana alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Karatu, Mchungaji Israel Natse (Chadema).
Alisema Serikali imeshalipa zaidi ya Sh bilioni 25 ya fedha katika madeni ya walimu yaliyohakikiwa na Sh bilioni tatu nyingine zitalipwa hadi kufikia Juni 30, mwaka huu, ambapo walimu 80,000 wanatarajiwa kulipwa stahiki zao katika malipo hayo.
Katika swali lake, Mchungaji Natse alitaka kufahamu idadi ya walimu walioguswa na mabadiliko ya madaraja katika jimbo analoongoza, wanadai kiasi gani na watalipwa lini.
Nyongeza Majaliwa alisema Serikali pia imeridhia na kutoa muundo mpya wa kada za walimu kuanzia Julai 2014, ambao umewezesha walimu waliokuwa wamefikia ukomo katika muundo wa zamani, kunufaika kwa kupata nyongeza ya ngazi ya muundo mpya kupitia bajeti ya mwaka 2015/2016.
Kuhusu madai ya walimu katika Jimbo la Karatu, Majaliwa alisema, “katika Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, mabadiliko haya yamewagusa walimu 295.
Alisema uchambuzi wa taarifa za walimu walioguswa na mabadiliko hayo, umebaini katika Halmashauri ya Wilaya ya Karatu walimu 295 wanadai Sh bilioni 1.09 ambazo walimu wataanza kulipwa mwaka 2015/2016.
“Pamoja na mabadiliko hayo, Serikali imeondoa utaratibu wa kuwataka watumishi kukubali vyeo kabla ya kuwarekebishia mishahara, hali ambayo imerahisisha kazi ya urekebishaji wa mishahara ya watumishi kwa pamoja. “Awali, mwalimu alikuwa anaandikiwa barua ya kupandishwa daraja na kutakiwa kukubali ndipo taratibu nyingine zianze.
Kwa sasa, mwalimu atapata barua na taratibu zikiwa zinaendelea,” alifafanua Naibu Waziri. Aidha alisema kwa sasa halmashauri zimeagizwa kutohamisha watumishi kama hawana fedha, labla kama ni kwa kuwianisha ikama.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM) aliomba Mwongozo wa Spika akihoji kuwa wapo walimu wapya wilayani Kwimba hawajapewa posho zao tangu waripoti mwanzoni mwa mwezi huu, na kutaka kusikia kauli ya Serikali juu ya hilo.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alisema hilo linashughulikiwa na Tamisemi, na maagizo yalikuwa ni walimu wote hao zaidi ya 31,000 nchini kulipwa wanapofika vituoni mwao bila upungufu wowote.
Hivi karibuni Rais Kikwete alisema atahakikisha anamaliza matatizo yote yanayowakabili walimu kote nchini katika kipindi kilichobaki cha utawala wake. Alitoa ahadi hiyo wakati alipozungumza na walimu wapatao 1,500 kutoka wilaya 153 na mikoa yote ya Tanzania Bara, pamoja na wawakilishi kutoka Visiwani.
Akizungumza kwa hisia katika mkutano huo wilayani Arumeru mkoani Arusha, Rais Kikwete alisisitiza kuwa Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) anachokiongoza, kinaendelea kujali maslahi ya walimu kama watumishi muhimu zaidi katika Taifa. Alisema kwamba kilio chao ni cha umma na ni wajibu wa viongozi wote kutilia maanani.
“Nimeyasikia matatizo yenu kupitia risala maalumu, na mengi tulikwishaanza kuyafanyia kazi “Nawaahidi kutatua matatizo yenu kabla sijaondoka rasmi mwishoni mwa mwaka huu, na hata kama nitastaafu hapo baadaye, mengine yaliyosalia yataendelea kutatuliwa na viongozi wa serikali ijayo nami binafsi nitaacha maagizo hayo,” alisema Kikwete.

Ofisi ya fatwa Misri: Hujuma za Daesh Saudia sio Uislamu

Ofisi ya fatwa Misri: Hujuma za Daesh Saudia sio UislamuOfisi ya fatwa nchini Misri Darul-Iftaa, imelaani shambulizi la kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh dhidi ya msikiti wa al-Anuud katika mji wa Dammam mashariki mwa Saudi Arabia na kukitaja kitendo hicho kuwa, kinakinzana na mafundisho ya dini Tukufu ya Kiislamu. Taarifa iliyotolewa na idara hiyo, sanjari na kulaani kitendo hicho cha kigaidi, imesema kuwa wahusika wa jinai hiyo wanalenga kuibua machafuko na mauaji makubwa katika nchi za Kiarabu. Watu wanne walipoteza maisha na wengine 10 kujeruhiwa hapo jana wakati wa sala ya Ijumaa baada ya gaidi aliyekuwa  amebeba mada za miripuko kujilipua karibu na msikiti huo. Hii ni katika hali ambayo, wiki iliyopita, gaidi mwingine kutoka kundi hilo la kigaidi na kitakfiri alijiripua katikati ya waumini wa madhehebu ya Kishia waliokuwa wakisali sala ya Ijumaa katika msikiti wa Qadeeh mkoani Qatif, na kupelekea makumi ya watu kuuawa na wengine wengi kujerihiwa. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudi Arabia imesema hujuma hiyo ya jana ilijiri katika eneo la kuegeshea magari la Msikiti wa Imam Hussein (as) mjini Dammam yapata kilomita 400 kutoka mji mkuu, Riyadh. Miongoni wa watu waliopoteza maisha ni pamoja na gaidi huyo. Kundi la kigaidi la Daesh limekiri kuhusika na hujuma hiyo. Ingawa serikali ya Riyadh imetangaza kutohusika na hujuma hizo za kigaidi, lakini weledi wa mambo wanasema kuwa yanatekelezwa kwa malengo maalumu na kwa ushirikiano na viongozi wa serikali. Kufuatia hali hiyo maelfu ya raia wa maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo, wamefanya maandamano makubwa kulaani hujuma hizo za kigaidi dhidi yao. Katika maandamano yaliyoshuhudiwa katika miji ya Dammam na Qatif waandamanaji wametaka wahusika wa ugaidi kukamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria ili kujibu mashtaka dhidi yao.

Tanzania kuanzisha kambi nyingine ya wakimbizi

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, Mathias Chikawe, amesema serikali iko mbioni kuanzisha kambi nyingine ya wakimbizi mbali kidogo na kambi ya Nyarugusu ili kuwasaidia wakimbizi kutoka Burundi. Waziri Chikawe amesema kambi ya Nyarugusu ambayo kwa sasa inawahifadhi wakimbizi kutoka DRC imeanza kuzidiwa nguvu baada ya mamia ya maelfu ya wakimbizi wa Burundi kuwasili hapo. Tayari Wakongomani wanaoishi kambini hapo wameanza kugombana na wenzao Warundi na wameitaka serikali ya Tanzania kuharakisha mchakato wa kuanzisha kambi mpya ya wakimbizi. Wakimbizi wa DRC wamesema tayari mlipuko wa kipindupindu umesambaa kwa kasi na kuna hatari ya kuripuka magonjwa mengine ya kuambukiza. Masomo kwa watoto wakimbizi yamesimama katika kambi ya Nyarugusu kufuatia madarasa yao kutumiwa kama nyumba za kulala na Warundi wanaokimbia machafuko nchini mwao.

Bunge la Afrika lataka mapambano dhidi ya ugaidi

Tokeo la picha la bunge la afrika                                                                                                               Bunge la Afrika limetaka kuzidishwa mapambano zaidi dhidi ya ugaidi katika nchi za bara hilo. Taarifa iliyotolewa na The Pan-African Parliament, imezitaka nchi wanachama kutumia nyenzo za kila aina katika kukabiliana na migogoro ya bara hilo likiwemo wimbi la ugaidi sanjari na kuifanyia kazi mikataba inayohusiana na suala zima la usalama na amani, hususan azimio la kidemokrasia na uchaguzi ndani ya nchi za Kiafrika. Aidha bunge hilo limezitaka pande hasimu katika machafuko ya Burundi, kuhitimisha mwenendo huo, na badala yake kuupatia ufumbuzi mgogoro huo ili kuwatumikia wananchi. Limesisitiza kuwa, matatizo hayo yanaweza kutatuliwa tu kwa njia za amani. Mbali na Burundi The Pan-African Parliament pia limeitaka jamii ya kimataifa kuingilia kati mgogoro wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram nchini Nigeria, kurejesha usalama na amani katika maeneo yaliyoathirika na hujuma za kundi hilo na kumaliza matatizo ya waathirika wa mgogoro huo. Roger Ankodo Dang, Spika mpya wa Bunge la Afrika ametangaza kuwa, mbali na matatizo ya ugaidi, bara la Afrika linakabiliwa pia na matatizo mengine yakiwemo mabadiliko ya hali ya hewa, hali mbaya ya wanawake, afya na masuala ya elimu, ambayo bila ya kuimarishwa demokrasia ya kweli katika nchi za bara hilo, itakuwa vigumu kuyatatua. Mwishoni mwa kikao cha bunge hilo kilichofanyika nchini Afrika Kusini, nchi wanachama zimetakiwa pia kukabiliana na magendo ya silaha, suala ambalo limetajwa kuwa sababu ya kuendelea kwa machafuko katika bara hilo.
©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved