“Ufumbuzi wa kila kitu utegemee uwezo wa ndani”
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhma Sayyid Ali
Khamenei amesema misimamo ya nyuklia ya Iran ni ile ile iliyotangazwa
mara kadhaa hadharani. Ayatullah Khamenei ametoa sisitizo hilo leo mbele
ya hadhara ya Spika na wawakilishi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu
alipoashiria kadhia ya nyuklia na kubainisha kwamba “misimamo yetu
katika masuala ya nyuklia ni maelezo yale yale ambayo tumewaeleza
wananchi hadharani na ndio hayo hayo tuliwaeleza kama yalivyo viongozi
kwa mdomo na kwa maandishi.” Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
amesisitiza kuwa viongozi na wawakilishi wa Iran kwenye mazungumzo
wanafanya kazi ngumu na kwa jitihada kubwa na kuongeza kwamba wao
wanapaswa kuchachamaa na kusimamia misimamo ile ile iliyotangazwa; nasi
tuna matumaini kwamba wataweza kudhamini maslahi ya nchi na Mfumo.
Ayatullah Khamenei ameeleza pia kwamba kuna njia kadhaa za ufumbuzi wa
kadhia ya nyuklia ambazo zote zinategemea jinsi tutakavyozingatia zaidi
uwezo wa ndani na kuimarisha uzalishaji. Amesema katika masuala yaliyopo
baina ya Iran, Marekani, Magharibi na Uzayuni, mbali na kadhia ya
nyuklia kuna masuala mengine mtawalia likiwemo la haki za binadamu
yanayotarajiwa kuibuka; lakini kama uwezo uliopo utaelekezwa ndani na
kutatua matatizo, utatuzi wa masuala hayo pia utakuwa rahisi. Katika
sehemu nyengine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya
Kiislamu ametilia mkazo maelewano baina ya Bunge na mihimili mingine ya
dola hususan Serikali na kusisitiza kwamba ufunguo wa utatuzi wa
matatizo ya kiuchumi ya Iran na vilevile kadhia ya nyuklia ni kutegemea
uwezo wa ndani na kuukubali kwa dhati uchumi wa muqawama. Ameongeza kuwa
hakuna mkwamo wowote nchini na dawa ya matatizo ni kuimarisha
uzalishaji wa ndani na kuchunga utumiaji wa fedha. Ayatullah Khamenei
aidha amesema serikali ni kiunganishi kati ya mihimili ya dola na vyombo
vingine; na utendaji wake wa mafanikio utakuwa na taathira njema katika
harakati ya vyombo vingine, kwa hivyo kuwa na maelewano na serikali ni
lazima na ni dhihirisho halisi la kuwa kitu kimoja na kuwa na kauli
moja…/
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment