Kinana akerwa mafisadi kulindwa

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjrCYNrkp2PFpCe1rgp_IsJkf9ck-GKLefJo-6vSVtYBhitSRixoKfGX3XcfmulnHWns2TfZDek33UYirNLbptkF8j69pf42nFMboeb_G2TcImD3nbZi9kUvFqBvLUAF5jk-xIUri_200tN/s1600/14.jpgCHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimekemea watu wanaotumia siasa kama kichaka cha kuficha dhambi zao kwa kufanya ufisadi, lakini wanapobainika, hujitetea kwa kusema wanafanyiwa hivyo kutokana na siasa.
Aidha chama hicho kupitia viongozi wake wa juu, kimeshutumu matumizi mabaya ya utawala bora kutokana na kutumika kulinda wezi na mafisadi .
Hayo yalielezwa jana na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana pamoja na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye wakati wakihutubia kwa nyakati tofauti mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Bukoba na kuhudhuriwa na mamia ya watu.
Viongozi hao wa ngazi ya juu kitaifa, wako ziarani katika Mkoa wa Kagera kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya chama na pia kukiimarisha.
Katika ziara hiyo, wanapokea taarifa za utekelezaji, wanakagua miradi na pia kuzungumza na wananchi. Wanaosingizia siasa Akirejea mgogoro uliokumba Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba ukihusisha Mbunge wa Bukoba, Balozi Khamis Kagasheki na Meya wa Manispaa ya Bukoba , Anathory Amani (aliyevuliwa wadhifa huo), Nape alisema hali ya kusingizia siasa baada ya wezi kubainika, haiko kwenye halmashauri hiyo pekee bali hata ngazi za juu.
Akirejea mgogoro huo katika halmashauri ya Manispaa Bukoba, alisema licha ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu Hesabu za Serikali (CAG) kukagua na kubaini wizi kuwapo wizi, hata watu wanaopaswa kuchukua hatua dhidi ya wezi, pia nao wanasema tatizo ni siasa.
Mgogoro huo ulianza mwaka 2012 baada ya Mbunge Kagasheki kumtuhumu Amani kuiingiza manispaa hiyo kwenye miradi ya ufisadi hali iliyosababisha mgawanyiko ndani ya chama. Aidha, mgogoro ulikolezwa na kufunguliwa kwa kesi tatu ambazo zilizuia utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika halmashauri hiyo.
Baada ya mgogoro kuibuka katika manispaa hiyo, CAG alitumwa kukagua na kubaini upotevu wa fedha uliofanyika. Nape alisema inapaswa kueleweka kwamba, malengo ya siasa ni kusaidia watu na si kuwaibia.
"Wizi uitwe wizi na mwizi ashughulikiwe kama mwizi," alisema na kuhimiza kwamba jambo hilo linapaswa kushughulikiwa. Akizungumzia wizi wa mali za umma, alisema utamaduni huo umeharibu hadi vijana kiasi kwamba, mtu akipewa ofisi ya umma akaondoka bila kujilimbikizia mali, anaitwa mshamba kutokana na uadilifu wake.
Utawala bora Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CCM, Kinana, alieleza kuchukizwa na watu wanaohusishwa na ufisadi kutoshughulikiwa haraka kisheria kwa kigezo cha kuzingatia utawala.
Alisema imefika wakati, mtu anabainika ni mwizi na anahusika kwenye ufisadi, lakini inachukua muda kuhojiwa na wakati mwingine kuundiwa tume zisizoisha. Alisema kwa kutumia mwavuli huo wa utawala, mwizi badala ya kufunguliwa kesi, ndiye anakwenda kuifungulia serikali kesi kwa kutumia fedha alizoiba; Hatimaye anashinda na kudai fedha na wakati huo huo anaamuriwa alipwe mshahara aliokuwa halipwi wakati akiwa amesimamishwa kazi.
Kinana alieleza matamanio ya kuona mwizi wa mali za umma akichukuliwa hatua mara moja ikiwemo kufukuzwa kazi na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, badala ya kusimamishwa kazi kwa kigezo cha kufanya uchunguzi chini ya mwavuli wa utawala bora.
Katibu Mkuu huyo alisema wizi na ufisadi wa aina mbalimbali, ni kinyume na utawala bora hivyo kama wezi wa mali za umma wangekuwa wanafahamu dhana hiyo, wasingefanya vitendo husika.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved