Serikali yaahidi kuwalipa makandarasi

http://www.fullshangweblog.com/wp-content/uploads/2014/04/PICHA-ZA-KUKABIDHI-VIFAA-3-1.jpg
WAZIRI wa Fedha, Saada Mkuya
WAZIRI wa Fedha, Saada Mkuya amesema Serikali italipa madeni ya makandarasi na watumishi ambayo yamehakikiwa na pia itapeleka TAMISEMI orodha ya halmashauri ambazo zimetoa madeni hewa ili yalipwe.
Akijibu hoja za wabunge wakati wa kuwasilisha bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha, Mkuya alisema walipokea madeni ya takribani Sh trilioni 1.2, lakini baada ya kuhakiki wamebaini kuwa madeni hayo yana thamani ya Sh bilioni 856.
“ Baada ya kuhakiki, tunapigiwa simu na watendaji wa halmashauri kuwa deni hilo tulishalipa sasa tunaleta deni lingine, itawezekanaje kuwa mmelipa wakati tumehakiki na vielelezo vinaonesha hivyo. “ Sasa nasema tutalipa madeni ya wakandarasi na watumishi ambayo yamehakikiwa, na Hawa Ghasia (Waziri-TAMISEMI) nitakuletea orodha ya halmashauri zilizowasilisha madeni hewa ili tuwaone namna ya kushughulikia tatizo hilo,” alisema.
Alisema kuanzia jana, Serikali italipa madeni hayo na kuwa ndani ya bajeti ya mwaka huu, wanatarajia kulipa madeni yenye thamani ya Sh bilioni 57 na kuwa bajeti ijayo Serikali italipa zaidi ya Sh bilioni 200 kwa ajili ya madeni mwaka unaoishia 2014 na kuagiza kuhakikiwa madeni ya kuanzia Julai 2014 hadi sasa.
Awali wakichangia, wabunge walilalamikia mrundikano wa madeni ya wazabuni na watumishi na kuitaka serikali kuweka fungu kwa ajili ya kulipia madeni hayo.
Mbunge wa Ole, Rajab Mbarouk (CUF) alisema kumekuwa na shida katika ukusanyaji wa mapato hususani katika halmashauri kutokana na mawakala wanaotumiwa kukusanya kodi kubaki na fedha nyingi ambazo zingesaidia kuongeza pato la serikali. “ Mpaka sasa mawakala hawajawasilisha serikalini zaidi ya Sh bilioni 6.4, hizi ni fedha nyingi ambazo zingeisaidia serikali,” alisema na kuongeza kuwa hata TRA imekuwa haikusanyi fedha ipasavyo kutokana na baadhi ya watendaji kutokuwa waadilifu.
Aidha, Mbarouk aliitaka TRA, kuharakisha kesi za kodi ili fedha zinazodaiwa ziingie serikalini na kwamba mpaka sasa kuna kesi za kodi za trilioni 1.7.
Pia aliitaka Serikali kutumia mashine za EFD katika malipo na manunuzi na kutoa mfano kuwa serikali imelipa na kununua bila EFD manunuzi ya thamani ya Sh bilioni 4.4 wakati kwa halmashauri ni Sh bilioni 4.6.
Naye Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) aliitaka serikali kuhakikisha kampuni zinazowekeza hapa nchini zinajiorodhesha katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) jambo ambalo litasaidia pia kubaini mapato halisi ya makampuni hayo.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved