Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuanzia mwaka huu wa fedha
itawalipa pensheni wazee wote bila kujali kama waliajiriwa ama hapana.
Watakaonufaika na pensheni hiyo ni wazee waliofikisha miaka 70 na
kuendelea lengo la kufanya hivyo ni kuwawezesha kujikimu kimaisha.
Waziri wa Uwezeshaji Ustawi wa Jamii vijana Wanawake na Watoto Zainab
Omar Mohamed akizungumza wakati akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo
alisema mchakato wa kufahamu idadi ya wazee wote Unguja na Pemba
wanaostahiki kulipwa pensheni hiyo umekamilika.
Alisema SMZ imechukuwa uamuzi huo ukiwa na lengo la kupambana na hali
ngumu ya maisha inayowakabili wazee ambao baadhi yao hawakuajiriwa
serikalini au na taasisi zake.
“Mheshimiwa Spika napenda kuwajulisha wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi (BWW)kwamba kwa mwaka wa fedha tutaanza kulipa pensheni kwa
wote.”alisema.
Aidha Waziri huyo aliwaambia wajumbe wa BWW kwamba juhudi za
kupambana na matukio ya udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto
zinaendelea ikiwamo kazi ya uzinduzi wa kampeni hizo iliyofanywa na
Rais wa Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein.
Alisema kampeni hiyo ni muhimu kwa ajili ya kuhakikisha kwamba
udhalilishaji unatokomezwa kwa kuzishirikisha taasisi mbali mbali pamoja
na vyombo vya kusimamia haki na sheria.
Alieleza kuwa imebainika kwamba mapambano dhidi ya vitendo vya
udhalilishaji wa kijinsia yanahitaji ushirikiano baina ya wizara ikiwamo
ya Katiba na Sheria, Elimu pamoja na Wanawake na Watoto.
Aidha alizitaka mahakama za Unguja na Pemba kuchukuwa juhudi ya
kuharakisha hukumu kwa kesi za ubakaji kwani wananchi wameanza kuvunjika
moyo kutokana na kesi hizo kuchukuwa muda mrefu hadi kutolewa kwa
hukumu zake kwa kuwepo visingizio mbali mbali ikiwemo kukosekana kwa
ushahidi.
“Tabia ya nenda rudi kesho imeanza kuwakatisha tamaa wananchi ambao
wengine wanatoka vijijini kuja mjini kwa ajili ya kusikiliza kesi yake
ambapo bila ya kupewa taarifa za uhakika kesi inaahirishwa”alisema.
Alisema baadhi ya kesi zinalazimika kufutwa na nyingine majalada yake
kufungwa moja kwa moja kwa sababu zinakosa ushahidi muhimu ambao ndiyo
utakaoweza kuwatia hatiani watuhumiwa wa makosa ukiwamo ubakaji.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment