Mufti Shaban Ramadhan Mubajje wa Uganda amelalamikia vikali mauaji yanayofanywa mara kwa mara dhidi ya masheikh nchini humo.
Gazeti
la kila siku la New Vision la nchini Uganda limemnukuu Mufti Mubajje
akisema kuwa, kuna watu wana nia ya kueneza fitna na mizozo kati ya
Waislamu na kuongeza kwamba, mauaji hayo yalianza kama "mchezo," lakini
sasa yamekuwa ni hatari kwa Waislamu. Amesisitiza kwamba, inasikitisha
kuona kuwa Waislamu wa Uganda wameshapoteza masheikh zaidi ya watano.
"Ilianza kama mchezo lakini sasa imekuwa ni tishio kubwa. Tunapaswa kuwa macho na kuguswa na suala hilo kama Waislamu," amesema.
Sheikh
wa karibuni kabisa kuuawa nchini Uganda alikuwa ni Sheikh Abdul Rashid
Wafula aliyepigwa risasi tano kifuani na kuuawa katika mji wa Nakalole
huko Mbale, mwezi uliopita.
Sheikh Mustafa Bahiiga aliuawa mwezi
Disemba mwaka jana katika msikiti wa Bwebajja, katika barabara ya
Entebbe, wakati Sheikh Abdul Qadir Muwaya naye aliuwa nyumbani kwake
huko Mayuge kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.
Mwaka 2012 pia,
viongozi wawili wakubwa wa Waislamu, Sheikh Abdul Karim Ssentamu na
Hajj Abubakar Kiweewa waliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.
Mufti
wa Uganda amemlaumu Mkuu wa Polisi wa nchi hiyo Jenerali Kale Kayihura
akisema kuwa amekataa kuonana naye akikwepa kujadiliana naye suala hilo
hilo la kuuawa viongozi wa Kiislamu.
Sheikh Mubajje ameitaka mahakama
ya Uganda ifanye haraka kuwapandisha kizimbani watu waliotiwa mbaroni
kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo na adhabu kali itolewe kwa watu
watakaopatikana na hatia ili iwe funzo kwa watu wengine.
No comments:
Post a Comment