Mbatia: NCCR-Mageuzi haitajiondoa Ukawa

CHAMA cha NCCR - Mageuzi kimesema hakitajitoa katika kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kwa vile lengo lake si mgawanyo wa madaraka bali Katiba.
Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia alisema hayo jana wakati akitoa Maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho iliyokaa jana na kusema wamedhamiria kutotoka katika kundi hilo na kwamba watavuka salama katika mgawanyo huo wa madaraka.
Alisema Ukawa ni zao lao, hivyo hawatatoka wala kuvunjika kama wanavyodaiwa na baadhi ya watu na kutaka vyama vingine kuendelea kuaminiana kwa kuwa NCCR ipo kwa moyo thabiti.
“Kikao chetu tumeazimia kwa malengo ya chama yatafikiwa ndani ya Ukawa kwani si lengo letu katika kugawa madaraka bali ni Katiba kwanza kwa kusimamia mawazo ya wananchi hivyo kwa umoja vyama vitahakikisha vinapigania mawazo ya Watanzania,” alisisitiza.
Alisema katika mgawanyo wa madaraka vyama hivyo vyenye lengo moja vitahakikisha vinavuka salama kwa kugawana vizuri kwa maelewano na jambo la msingi ni kuaminiana kwani hakuna linaloshindikana.
Akizungumzia Katiba pendekezwa, alidai kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba imefutika na imetupwa kwani hakuna mwenye uwezo wa kuitisha Kura ya Maoni tena hivyo serikali kushindwa kuwapatia Katiba mpya wananchi licha ya kutoa mawazo yao.
Kuhusu uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura alisema linaweza kusababisha vurugu wakati wa kuwekwa wazi huku kampeni zimeanza hivyo hatua zichukuliwe kudhibiti hali hiyo ikiwepo kujiandikisha mara mbili kutokana na kuwa mpaka sasa watu 5,000 wamegundulika kujiandikisha mara mbili.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved