Kumekucha CCM: Baraza la Ushauri la Wazee( Mkapa, Mwinyi na Wengine) Kukutana Wiki Hii Kujadili Jinsi Ya Kumpata Mgombea Urais

Hatimaye kile kikao cha Baraza la Ushauri la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachowahusisha pia marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa, kinatarajiwa kufanyika wakati wowote wiki hii kujadili mwenendo wa mchakato wa kumpata mgombea urais wa Tanzania kupitia chama hicho.

Taarifa kutoka chanzo kimoja ndani ya CCM kimeeleza kuwa Mwinyi, Mkapa na wazee wengine wanaounda Baraza la Wazee la Ushauri, watapasua kichwa wiki hii kujadili mwenendo wa urais ikiwa ni siku chache kabla ya kufikia Julai 2, mwaka huu, inayoonyeshwa katika ratiba ya uchaguzi ya CCM kuwa ndiyo siku ya mwisho ya kurejesha fomu kwa wanaowania urais.

Lengo la kikao cha Wazee ni kujadili kwa kina mwenendo wa mchakato wa kumpata mgombea urais na mwishowe kutoa mapendekezo yao juu ya namna bora ya kumpata mgombea kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM (CC)
 
"Kikao hiki ni muhimu kwa hatma ya mchakato wa uchaguzi... baada ya kutofanyika wiki iliyopita, sasa kitafanyika wiki hii, tena wakati wowote kuanzia kesho (leo)," chanzo kilieleza.

Awali, kikao hicho kilitarajiwa kufanyika Jumatano iliyopita jijini Dar es Salaam lakini kikaahirishwa na Katibu wa Baraza la Ushauri la Wazee, Pius Msekwa, kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni baadhi ya viongozi wakuu wa CCM kuwa safarini.
 
Alipoulizwa  jana iwapo watakutana kaunzia leo, Msekwa hakuwa tayari kueleza kiundani na badala yake alimjibu mwandishi kwa kifupi: "Just pay attention (wee jiweke tayari tu) kama umesikia juu ya kikao chetu."

Kikao cha Baraza la Ushauri la Wazee ni mahususi kwa ajili ya ushauri juu ya watia nia 42 wa urais waliojitokeza kutaka kuteuliwa na CCM kupeperusha bendera yake katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Wanaounda baraza la wazee
Wanaounda Baraza la Ushauri la Wazee kwa mujibu wa mabadiliko yaliyofanywa na CCM mwaka 2012 katika katiba yake ni marais wastaafu Mwinyi (Mwenyekiti), Mkapa (Mjumbe), Amani Abeid Karume (Mjumbe) na Dk. Salmin Amour (Mjumbe).

Wengine ni Waziri Mkuu mstaafu na Makamu wa Kwanza wa Rais, John Malecela (mjumbe) na Pius Msekwa (Katibu).
 
Mkutano huo wa Baraza la Wazee CCM ni utangulizi wa mfululizo wa vikao vingine vya chama hicho vitakavyoanza Julai 5, mwaka huu.

Vikao vingine ambavyo viko katika maandalizi ya kukutana ni Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa itakayokutana Julai 7 na Kamati Kuu (CC) itakayokutana Julai 8, chini ya Rais Kikwete, ikifuatiwa na kikao cha NEC Julai 9, mwaka huu.

Jina la mgombea urais atakayepeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu litajulikana Julai 12 baada ya kupigiwa kura na Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM, ambao ni maalum kwa ajili kuchagua jina la mgombea mmoja kati ya watatu..

Lowassa Awaburuza Wenzake Urais CCM...... Ni matokeo ya utafiti kwenye wilaya 20

Waziri Mkuu mstaafu, Monduli, Edward Lowassa ametajwa kuongoza katika kutaja vipaumbele vya maendeleo ikiwamo kupunguza tatizo la Ajira nchini na kuinua Elimu, miongoni mwa kundi la wanasiasa waliotangaza nia ya kuwania Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

 Kadhalika, Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, ametajwa kuwa ndiye kiongozi wa siasa aliyeshuhudiwa na wananchi wengi katika hotuba zake kuliko wanasiasa wengine waliokwisha kutangaza nia.
Hayo yamo katika ripoti ya utafiti uliofanywa na Shirika la Maendeleo la Utafiti la Elimu (Tedro), iliyozinduliwa jijini Dar es Salaam jana.
 
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Jacob Katerri, alisema ripoti hiyo ilijumuisha Wilaya 20 na kuwahoji watu 2,000 kutoka vijijini na mijini.

 Alisema katika ripoti hiyo kipengele cha watangaza nia walioshuhudiwa na watu wengi katika hotuba, Lowassa anaongoza kwa kushuhudiwa kwa asilimia 54, akifuatiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe (46), Naibu Waziri wa Fedha ,  Mwigulu Nchemba (44), Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira (40) na Jaji Mkuu mstaafu Augustino Ramadhani(39).

 Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba(34), Waziri Nchi Ofisi ya Rais, Profesa Mark Mwandosya (31), Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki,  Makongoro Nyerere (27), Waziri wa Ujenzi, John Magufuli (23), na Mbunge wa Sengerema, Willium Ngeleja (19) na wengine wakifuata.

Katika Kipengele cha kupunguza tatizo la ajira, ripoti hiyo ilieleza kuwa wananchi walipohojiwa walieleza kuwa wana imani na Lowassa kwa asilimia 19,  Nchemba (14), Magufuli (13).

 Makamba (13), Membe (12), Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (10), Mwandosya (7), Dk. Harrison Mwakyembe (7), Wassira (2) na wengine (3).

“Utafiti huu umebaini kuwa watangaza nia wengi pamoja na mambo mengine walijikita sana katika kusema watatatua tatizo la ajira kwa vijana,” alisema  Kaserri.

Kadhalika ripoti hiyo ilizungumzia kipengele cha kuinua elimu nchini, ambacho wananchi waliohojiwa walitoa nafasi kubwa ya uwezekano wa kutekelezewa kwa kipaumbele hiki kwa Lowassa kwa asilimia 25.

Nchemba (18), Membe (16),  Makamba (13), Magufuli (12), Mizengo Pinda (12), Wasira (3) na wengine (9).

 Pia ripoti hiyo ilizungumzia kipengele cha Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo waka 2025, na wananchi walikuwa na imani na Nchemba kwa asilimia 13.4 kuwa ataweza kulipeleka taifa kufikia kipato cha kati.

Lowassa (11), Wasira (9), Membe (9.20),   Magufuli (9.0), Makamba (5.3), Mwandosya (4.60),  Pinda (3.5) na Dk.  Mwakyembe (1.40).

Hata hivyo, utafiti huo ulielezea kipengele cha kuinua sekta ya Kilimo na Mifugo nchini ambacho kwa watangaza nia hao, wananchi walikuwa na imani kwa Pinda kwa asilimia 23.

Lowassa (17), Nchemba (16), Membe (11) Wasira (9),  Makamba (7), Magufuli (5), Waziri wa Maliasili na Utalii,  Lazaro Nyalandu (3.3), Mbunge wa Nzega, Hamisi Kigwangala(3.2) na Mwakyembe (2.6).

Katerri alisema utafiti huo pia ulihusu kipengele cha Utawala bora na vita dhidi ya ufisadi ambapo ulionyesha kuwa Mwigulu Nchemba amepata asilimia 17.4 ya uwezo wa kupambana na tatizo hilo.

Wengine waliomfuata ni Magufuli (14.2), Membe (11), Lowassa (6.10), Jaji Ramadhani (6) na Mwandosya (5).

Wengine ni Mizengo Pinda (8),  Mwakyembe (8),  Makamba (7), Samuel Sitta (6), Dk. Kigwangala (3).

Katika kipengele za Uadilifu usiotiliwa shaka katika utumishi Nchemba alipata asilimia 15, Membe (13), Mwandosya (13), Pinda (8), Makamba (8) Jaji Ramadhani (7),  Lowassa (10%).

Katika kipengele cha hotuba iliyo bora, Katerri alisema Nchemba alipata alama (A), Wasira( B+), Membe (B+),  Mwandosya (B+) Lowassa (B) na Membe (B). Katerri Alisema lengo la utafiti huo ni  kutathmini Elimu katika Nyanja ya uraia kwa watanzania kupitia vipaumbele katika hotuba za waliokwisha kutangaza nia kupitia CCM.

Alizitaja wilaya ambako utafiti huo ulifanyika kuwa ni  Kinondoni, Kibaha Vijijini, Kilombero, Rombo, Arumeru, Mbulu na Babati, Lindi, Mtwara, Njombe mjini, Njombe Vijijini, Mbeya Mjini, Nyamagana, Biharamulo, Tabora, Nzega, Bahi, Chamwino na Kasulu.

MAPOKEZI YA STEVE NYERERE ALIVYOTANGAZA KUGOMBEA UBUNGE WA KINONDONi,,

Kwenye list ya mastaa wa TZ waliotangaza kugombea Ubunge kwenye Uchaguzi wa 2015 lipo pia jina la mastaa wa Bongo Movie, Steve Mengere aka Steve Nyerere.
Jamaa alikuwa anamaanisha kabisa kuhusu safari yake kwenye Siasa, hapa nina pichaz kutoka kutoka viwanja vya CCM Bwawani ambapo Steve alikuwa akitangaza nia hiyo.
“Mama zangu, baba zangu, vijana wenzangu.. jitokezeni kujiandikisha ni haki yenu ya msingi hasa katika Uchaguzi Mkuu ujao… Mimi Steve Nyerere nimeamua kwa dhati kujitoa na kutangaza nia ya kuwania Ubunge wa Kinondoni“– Steve Nyerere.

Madereva wameipongeza serikali kwa utatuaji wa mgogoro wao na wamiliki wa mabasi.

Hatimaye umoja wa madereva umeipongeza serikali kwa hatua yake ya utatuaji wa mgogoro wa kimaslahi kati ya madereva na waajili wao ambapo pia umeahidi kutokugoma tena.
Inatajwa kuwa kikao kilichofanyika june 23 mwaka huu kati ya madereva, serikali na wamiliki wa mabasi ndicho kilichozika mgogoro wa muda mrefu wa kimaslahi ambao ulisababisha uwepo wa migoma ya mara kwa mara.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa katika kikao cha madereva zaidi ya 4000 msemaji wa umoja huo Bw Rashid Saleh anasema hatimaye dereva wa kitanzania amesaminiwa kwa kupatiwa mkataba ambao utamfanya afurahiye kazi yake.
 
Aidha katika mkutano huo pia ambao ulitumika kutangaza uanzishwaji wa chama cha wafanyakazi madereva nchini, madereva walitakiwa kuhakikisha wanakuwa mstali wa mbele katika kuhakikisha maslahi yao yanatekelezeka.
 
Kwa mujibu wa madereva waliozungumza na ITV licha ya kuahidi kufanya kazi hiyo kwa ustadi mkubwa wamesema kuwa rasimu hiyo ya mkataba itawawezesha kukidhi mahitaji yao muhimu ambayo wanadai kuyakosa kwa kipindi cha miaka 50 ya uhuru sasa.

Mh.Mkapa ameziasa nchi za Afrika kuacha kutegemea misaada ya wahisani.

Rais mstaafu wa serikali ya awamu ya tatu Mh.Benjamin Mkapa amezitaka nchi za kiafrika kuacha kutegemea zaidi misaada ya wahisani toka ng’ambo kwani baadhi ya nchi hizo zimeanza kuchoka kutokana na kuelewemewa na madeni makubwa, badala yake amezishauri nchi za Afrika kujiwezesha kwa mambo yaliyo ndani ya uwezo wa waafrika wenyewe ikiwemo kufanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa.
Mh. Mkapa ametoa changamoto hiyo wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 19 tangu kuanzishwa kwa radio maria Tanzania, sherehe zilizofanyikia katika kanisa katoliki parokia ya madhabahu ya bikira maria kawekamo jijini Mwanza ambapo rais huyo mstaafu pia ameongoza harambee kwa ajili ya kuchangia kiasi cha shilingi milioni 60 zinazohitajika kuendesha radio hiyo na kufanikisha kupatikana kwa zaidi ya shilingi milioni 40 zilizochangwa kwa njia mbalimbali na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.
 
Rais huyo mstaafu Benjamin Mkapa pia amegusia suala la uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika oktoba 25 mwaka huu kwa kutoa tahadhari kwa baadhi ya wanasiasa wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi.
 
Awali akihubiri katika ibada ya misa takatifu iliyohudhuriwa na mamia ya waumini pamoja na mahujaji 400 waliotoka hija katika eneo la nyakibeho nchini Rwanda askofu mkuu wa kanisa katoliki jimbo kuu la Mwanza mhashamu Thadeus Rwaichi amesema kuwa taifa na kanisa la mungu linapoelekea kwenye uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani zipo changamoto nyingi zinazolikabili na ambazo zinahitaji waumini kusimama katika imani ya kweli na dhabiti.
 

RAIS KIKWETE AWAPOKEA WAPANDA BASIKELI WALIOSAFIRI KILOMITA 830 KUTOKA MBEYA KUJA KUMPONGEZA IKULU, DAR ES SALAAM‏




Kinda mwingine kutoka Brazil anayetua Chelsea huyu hapa…

Wakati klabu mbalimbali barani Ulaya zikiendela na harakati zake za kufanya usajili ili kuimarisha timu zao kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu ya Engalnd, tayari kuna taarifa kuwa klabu ya Chelsea ipo katika hatua za mwisho kunasa saini ya  mchezaji wa Brazil Robert Kenedy Nunes do Nascimento.
Licha ya klabu mbalimbali zimeonyesha nia ya kutaka saini ya mchezaji huyo ikiwemo Manchester United na Barcelona lakini tayari klabu ya Chelsea imewazidi ujanja.
Kennedy mwenye miaka 19 atajiunga na wabrazil wenzake Willium, Oscar, Fillipe Luis na Diego Costa.

Kwa mara ya kwanza video ya Ali Kiba inaoneshwa kesho kwenye TV

Ali Kiba  ni staa mwingine mkali wa muda mrefu kwenye Bongo Fleva… Hit ya Chekecha Cheketua ni moja ya single ambazo mtaani wanaisubiri video yake kwa hamu sana.
Sasa good news ninayotaka kukusogea ni kwamba video hiyo mpya iliyotayarishwa Afrika Kusini inatarajiwa  kutambulishwa kesho June 29 kama ‘Exclusive’ kupitia kituo cha TV cha ufaransa maarufu kama Trace TV  kinachoonekana Africa kwa huduma ya kulipia kikiwa na nafasi yake kwenye upande wa burudani hususani muziki wa kizazi cha sasa.
Kupitia kwenye ukurasa wa instagram #TraceTV ya nigeria wamepost cover ya utambulisho wa video hiyo mpya na kuandika…’Catch the Video Premiere of ‘Chekecha Chekatua’ by Alikiba (@officialalikiba) on TRACE Urban on Monday at 9:23 am!!! #tanzania #worldpremiere #newvideo..

WAZIRI LUKUVI AFANYA ZIARA MKOANI IRINGA KUTATUA MIGOGORO YA ARDHI

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mh. William Vangimembe Lukuvi ameanza ziara ya siku tatu Mkoani Iringa ambapo aliongea na watendaji wa Mkoa wa Iringa kuhusiana na migogoro ya ardhi inayoukumba Mkoa huo . Aidha, Waziri Lukuvi alipata fursa ya kukagua shughuli za Shirika la Nyumba la Taifa na kusikiliza migogoro ya ardhi inayowakabili wananchi wa Manispaa ya Iringa na wilaya za jirani za Kilolo na Mufindi. Katika ziara hiyo, Waziri Lukuvi amerejea kauli yake aliyoitoa katika mikoa aliyokwishafanya ziara kwa kuwaonya na kuwaagiza Maafisa ardhi, wapima, wathamini na maafisa mipango miji kuacha mara moja kujinufaisha kwa kuwadhulumu wananchi haki zao za ardhi. Aidha ameutaka Uongozi wa Mkoa wa Iringa kuharakisha upimaji wa ardhi ya wananchi na utoaji wa hati na kutenga muda wao ili kuweza kusikiliza kero za wananchi ili kupunguza migogoro ya ardhi.

RAIS JK AFAGILIA MAGEREZA DAY..;

Rais Dk. Jakaya Kikwete akipokea heshima ya Wimbo wa Taifa mara baada ya kuwasili katika Viwanja  vya Chuo cha Maofisa Magereza kilichopo Ukonga jijini Dar.

Rais JK akimpandisha cheo mwanafunzi bora katika kozi ya 21 kutoka Inspekta na kuwa ASP.

RAIS  wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Amiri Jeshi  Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amelisifia Jeshi la Magereza kwa jitihada zao nzuri katika utendaji kazi pamoja na chagamoto nyingi walizonazo.
JK aliyasema  hayo  jana  katika shereha za Siku ya Magereza nchini ambapo  sherehe hizo kitaifa  zilifanyika kwenye Viwanja  vya Chuo cha Maofisa Magereza kilichopo Ukonga jijini Dar es Salama na  rais ndiye alikuwa mgeni rasmi.
Katika sherehe hizo,  Rais JK aliwapandisha maofisa 104 ambao walikuwa wakifanya mafunzo kutoka cheo cha Inspekta na kuwa ASP ambapo kati ya hao 82 walikwa wanaume huku 22 wakiwa maofisa wa kike  kati ya hayo 10  wakitoka  Chuo  cha Mafunzo,  Zanzibar.
Rais  aliahidi  kushughulikia changamoto zinazolikabili jeshi hilo la magereza kabla hajaondoka madarakani na kumwagiza Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, Kamishna Jenerali John Minja kumwandikia barua Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani mahitaji yao yote ili aweze kuyashughulikia kabla ya kuondoka madarakani.

Membe: Pinda ananinyima usingizi

WAZIRI wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ambaye pia anaomba CCM impitishe kuwa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu baadaye mwaka huu, Bernard Membe amekiri kwamba katika kinyang’anyiro cha urais ndani CCM, mtu anayemnyima usingizi ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Akizungumza na wanachama waliojitokeza kumdhamini jana, Membe alisema Pinda asingechukua fomu ya urais ndani ya CCM, angefurahia ushindi tu na tayari angekuwa ameshona suti na kushangilia ushindi.
Alisema kuwa Waziri Mkuu Pinda ni mchapakazi, asiye mbinafsi, mwadilifu, mvumilivu sana mwenye hekima na busara ya hali juu, mwanasheria aliyebobea na ndiye mwalimu aliyemfundisha kazi.
“Wengine wote hawanitishi nitawagonga lakini nikifika kwa Pinda itabidi nipumue kwanza...kwa hiyo mimi na Pinda ni pacha nikishindwa mimi nitamuunga mkono lakini akishindwa naamini ataniunga mkono, ndio maana hata wakati nakuja huku nimewasiliana naye akanieleza nenda na amenisaidia nimepata wadhamini wa kutosha,” alisema.
Membe amesema kuwa Mungu akimjaalia kuteuliwa na CCM kushinda urais atahakikisha baadhi ya miradi inayotumia fedha za ndani ambayo inasuasua ikiwemo ujenzi wa barabara ya Sumbawanga hadi Mpanda unakamilika, lakini pia bonde la Ziwa Rukwa linatumika kuzalisha chakula ambacho kitalisha nchi nzima kwa kuwa ardhi yake ina rutuba na inafaa kwa kilimo.
Pia, Membe aliwaasa baadhi ya wanaCCM kuacha kuwashangilia kila mgombea anayepita kuomba udhamini kwa kuwa si wote wana sifa kwani wenye sifa stahiki ni yeye na Waziri Mkuu Pinda.
Awali, Katibu Mwenezi wa Mkoa huo, Clement Bakali alisema kuwa mgombea huyo amepata wadhamini 855 kutoka wilaya zote za mkoa wa Rukwa.

Mbatia: NCCR-Mageuzi haitajiondoa Ukawa

CHAMA cha NCCR - Mageuzi kimesema hakitajitoa katika kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kwa vile lengo lake si mgawanyo wa madaraka bali Katiba.
Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia alisema hayo jana wakati akitoa Maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho iliyokaa jana na kusema wamedhamiria kutotoka katika kundi hilo na kwamba watavuka salama katika mgawanyo huo wa madaraka.
Alisema Ukawa ni zao lao, hivyo hawatatoka wala kuvunjika kama wanavyodaiwa na baadhi ya watu na kutaka vyama vingine kuendelea kuaminiana kwa kuwa NCCR ipo kwa moyo thabiti.
“Kikao chetu tumeazimia kwa malengo ya chama yatafikiwa ndani ya Ukawa kwani si lengo letu katika kugawa madaraka bali ni Katiba kwanza kwa kusimamia mawazo ya wananchi hivyo kwa umoja vyama vitahakikisha vinapigania mawazo ya Watanzania,” alisisitiza.
Alisema katika mgawanyo wa madaraka vyama hivyo vyenye lengo moja vitahakikisha vinavuka salama kwa kugawana vizuri kwa maelewano na jambo la msingi ni kuaminiana kwani hakuna linaloshindikana.
Akizungumzia Katiba pendekezwa, alidai kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba imefutika na imetupwa kwani hakuna mwenye uwezo wa kuitisha Kura ya Maoni tena hivyo serikali kushindwa kuwapatia Katiba mpya wananchi licha ya kutoa mawazo yao.
Kuhusu uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura alisema linaweza kusababisha vurugu wakati wa kuwekwa wazi huku kampeni zimeanza hivyo hatua zichukuliwe kudhibiti hali hiyo ikiwepo kujiandikisha mara mbili kutokana na kuwa mpaka sasa watu 5,000 wamegundulika kujiandikisha mara mbili.

BreakingNews Breaking News: Taarifa za ‘magaidi’ Morogoro na picha za walivyokamatwa navyo.

Ripoti hii ni ya ITV June 27 2015 kutoka Morogoro inahusu watu watatu kufariki katika mapambano na Polisi, huku wawili kati yao wakihisiwa kuwa na uhusiano na kundi la kigaidi la Al Shabaab.
Breaking News nyingine kuhusu tukio hilihili iliyoripotiwa na Gazeti la Mwananchi inahusu watu sita kukamatwa na wengine 50 wanatafutwa, walikutwa wakiwa na sare za majeshi pamoja na silaha kama majambia kwenye msitu Mvomero.
Kwenye taarifa iliyofatia kutoka Mwananchi, imesema Mkulima Cassian Peter amefariki mchana wa June 27 2015 kwenye Hospitali ya Bwagala ambapo Polisi mmoja amelazwa na hii ni baada ya kujeruhiwa na hao watuhumiwa wa Ugaidi kabla hawajakamatwa.
Mtangazaji na Mwandishi wa habari wa Radio One Maulid Kambaya kwenye page yake ya Facebook alipost picha za walivyokamatwa navyo ‘Magaidi’ hawa.

P Square wafunguka kitu kinachowapa hofu zaidi?

Peter na Paul Okoye kwa pamoja tunawajua kama P Square, ukubwa wa jina lao sio ndani ya Africa pekeyake… wana hits kibao ambazo zimewaweka kwenye ramaniya dunia pia.
Mafanikio yao yalianzia pale ambapo waliweka nguvu yao nyingi kwa kufanya muziki wakitumia lebo yao ya Square Records… December 2011 milango mingine mikubwa ikafunguka kwenye muziki wao, waliingia Mkataba kufanya kazi na lebo ya Akon Konvict Muzik.. kazi kama Beautiful Onyinye waliyomshirikisha Rick Ross na Chop My Money zilipenya sana nje ya Afrika, watu wakazidi kuwajua !!
Safari yao haikuwa rahisi, lakini unajua siri ya wao kuifungua milango yote ya mafanikio? Kuna kitu chochote wanachokihofia kwa sasa?
>>> “Siri ya mafanikio yetu ni kazi. Tunafanya sana kazi.. Juhudi zote tunazowekeza katika kazi yote ni hofu ya umaskini, tumeshaonja maisha ya umaskini mkubwa na tunaogopa sana umaskini, ndio maana utasikia tumewekeza hapa na kule yote ni kujikinga na umaskini.
Tumeshuhudia wasanii waliopata umaarufu na utajiri kabla yetu lakini leo hawana chochote cha kuonesha kwa juhudi zao, kitu hiki kinatuogopesha sana… Tuliwahi kuishi maisha ya kubanana baba, mama na watoto nane kwenye nyumba ya kupanga yenye vyumba viwili, chakula, ada, mavazi vilikuwa ni tatizo sana kwetu na kipindi hicho baba yetu alitusihi sana tuje kuwa viongozi wa maisha yetu wenyewe tusiopenda kufanya kazi chini ya mtu na ndio maana unawaona P Square wanafanya biashara zao wenyewe leo”.>>> Nukuu ya walichokisema P Square kwenye moja ya Interview.

Steve Nyerere atangaza rasmi kuwa anautaka Ubunge 2015..

Aliyekuwa mwenyekiti wa Bongo Movie Unit, Steve Nyerere ameingia kwenye list ya wagombea ubunge mwaka 2015
Kwenye interview na millardayo.com Steve amesema ‘Kwanza ninataka kuwahakikishia watanzania sijakurupuka, nimekuwa  mwanachama wa chama cha Mapinduzi  umoja wa vijana almost miaka 25 na sasa hivi nina miaka 29 naelekea 30 lakini vilevile nimekuwa kamanda wa vijana miaka 10 tawi la bwani kinondoni, nimekuwa muhamasishaji  wa chama cha mapinduzi kitaifa kwa muda wa miaka 10′
‘Sijakurupuka na wala sijatamkia sifa kwasababu labda nimeona mtu fulani amegombea, kinondoni kuna matatizo kadhaa  nani anaweza kuyatetea hayo matatizo? nitakuwa mtetezi pamoja na matatizo ya wasanii wetu, kuhusu kazi zangu za filamu nitakuwa nafanya kama kawaida huku nikiwa natumikia kazi za Bungeni’
ATAACHA KUIGIZA?!
Amejibu >>> ‘Kazi yangu ya sanaa sitoweza kuiacha nadhani naweza kuwa ndio Mbunge wa kwanza yuko ndani ya Bunge na bado yuko kwenye sanaa anacheza filamu’

Kingunge anusa mchezo mchafu urais ndani ya CCM


Mwanasiasa mkongwe na kada wa CCM, Kingunge Ngombare Mwiru (Pichani) amesema anahisi kuna mchezo mchafu unapangwa kwenye mchakato wa kupata mgombea wa urais wa chama hicho tawala, akitaja idadi kubwa ya waliojitokeza kuwa ni ishara mbaya.
Mwanasiasa huyo mkongwe aliyefanya kazi na marais wa awamu zote nne, pia, bila kumtaja jina, alitumia muda mwingi kwenye hotuba yake kujibu kauli ya makamu mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula aliyekaririwa akisema kuwa mgombea wa chama hicho hatakiwi kujinadi.
Kingunge, ambaye amejitokeza hadharani kumpigia debe Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa alionyesha hofu hiyo jana wakati mbunge huyo wa Monduli alipokuwa akihitimisha kazi ya kusaka wadhamini mkoani Dar es Salaam kwenye ofisi za CCM Mkwajuni wilayani Kinondoni.
Hadi sasa, makada waliochukua fomu kuwania urais kwa tiketi ya CCM ni 41 baada ya mwanachama mmoja kuchukua fomu jana akisema atamudu kupata wadhamini kwa njia ya mtandao katika siku tano zilizosalia. Akizungumza katika mkutano wa kusaka wadhamini ulioandaliwa kwa ajili ya Lowassa wilayani Kinondoni jana, Kingunge alipingana na kauli ya Mangula kuwa mgombea wa CCM atanadiwa na chama, si kujinadi mwenyewe akisema chama hicho kinataka mgombea anayekubalika ndani na nje.
Siku tatu zilizopita, Mangula alihojiwa na kituo cha televisheni cha Shirika la Utangazaji Tanzania(TBC) na kusema mgombea wa chama hicho hatakiwi kujinadi mwenyewe, kusisitiza kuwa anatakiwa kunadiwa na chama.
Lakini Kingunge aliikosoa kauli hiyo jana akisema chama hicho kimeweka utaratibu na hakuna sababu ya kuuacha na kuanza kuwahukumu wagombea kabla ya vikao na kusisitiza kuwa CCM haikuwahi kuwahukumu wagombea kabla katika chaguzi zilizopita.
“Mchakato ufuate taratibu zilizowekwa,” alisema Kingunge ambaye aliibuka Kinondoni ambako Lowassa alimalizia shughuli zake jijini Dar es Salaam.
“Nimemsikia kiongozi wetu mmoja tena juzi juzi hapa, nikamuona kwenye televisheni anasema mtu hawezi kwenda kujinadi yeye binafsi, ananadiwa na chama.
“Nikasema eh! hilo hilo. Lakini nataka nimweleze yeye na wenye fikra kama hizo kuwa kuna ngazi mbili katika utaratibu wetu; kwanza, mwanachama anayetaka kuwania ubunge, udiwani, urais lazima ajinadi ndani ya chama, ndivyo tulivyofanya miaka yote kwa mujibu wa katiba na taratibu zetu. Ndivyo wanavyofanya sasa wakina Lowassa.”
Alisema pili, wagombea wakishajinadi chama kitamteua mmoja ambaye kitamnadi na yeye ataendelea kujinadi.
“Si vizuri watu ambao tumewapa vyeo katika chama wakaanza ama wakaendelea kukitumia chama chetu kwa mambo yao binafsi. Kama wana mashaka tupo tunaojua mambo ya chama,” alisema Kingunge huku akishangiliwa na mamia ya watu.
Kingunge alisema mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akiwa Dodoma alisema chama kinatafuta mgombea anayekubalika ndani na nje ya chama hicho ili kuweza kushindana na vyama vingine

Greencity Stand Up:Chukua nafasi hii kumpigia kura mwanambeya kuleta ushindi Nyumbani


PAMOJA TUSAIDIANE KUFANIKISHA NDOTO ZETU!?

Bonyeza HAPA na Ku'like' Ukurasa wetu wa Facebook kwa taarifa za haraka na moja kwa moja.

Stars ya Mkwasa yaanza mazoezi

TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars imeanza mazoezi jana kwenye Uwanja wa Boko Veterani kujiandaa na mchezo wa marudiano kuwania kufuzu kwa fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) dhidi ya Uganda wiki ijayo, huku wachezaji wawili, Vincent Barnabas na Mudathir Yahya wakiongezwa.
Stars inayonolewa na makocha wazawa, Charles Mkwasa na msaidizi wake Hemed Morocco, itakuwa ikifanya mazoezi asubuhi na jioni uwanjani hapo huku timu ikiweka kambi yake katika hoteli ya Kiromo mjini Bagamoyo.
Wachezaji wote walioitwa wameripoti kambini tangu juzi na jana walifanya mazoezi asubuhi isipokuwa Aggrey Morris ambaye ni majeruhi na nafasi yake imekuchukuliwa na Vicent Andrew (Mtibwa Sugar) na Jonas Mkude aliyekwenda kufanya majaribio Afrika Kusini nafasi yake ikizibwa na Mudathir Yahya (Azam FC).
Katika hatua nyingine, mshambuliaji Rashid Mandawa wa Kagera Sugar ambaye ni mmoja kati ya wachezaji walioitwa kwa mara ya kwanza, amesema amefurahishwa kuitwa kwenye kikosi hicho na kuanza mazoezi vyema.
Mchezaji huyo ni alikuwa mmoja wa wachezaji wengine waliojitokeza jana kwenye kikosi cha timu ya taifa kilichoanza mazoezi jana katika Uwanja wa Boko Veterani, Dar es Salaam.
Mandawa ambaye amehamia Mwadui FC ya Shinyanga akitokea Kagera Sugar ya Missenyi, alisema kwa upande wake inampa moyo na kuwa ni hatua nzuri ya kukuza kipaji chake na kuahidi kufanya makubwa zaidi.

Kocha mpya Simba anadi sera zake

KOCHA mpya wa Simba, Muingereza Dylan Kerr amesema ataendeleza wachezaji chipukizi ili kuwa na timu bora kwa sasa na baadaye.
Kerr aliyasema hayo baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kulakiwa na wajumbe wa Kamati ya Simba, Collin Frisch na Said Tully.
“Nimefurahi kuja Tanzania na nawaahidi viongozi na mashabiki kuwa nitahakikisha naendeleza wachezaji chipukizi ili Simba iweze kutamba sasa na baadaye,” alisema Kerr.
Kocha huyo, ambaye amerithi mikoba ya Mserbia Goran Kopunovic, amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuifundisha Simba ambapo atakuwa anasaidiwa na kiungo wa zamani wa timu hiyo, Suleman Matola.
Wakati Kerr akiwasili pia alikutana na kocha mpya wa makipa Idd Salim kutoka Kenya, aliyewasili tayari kwa kazi mpya kwenye klabu ya Simba.
Simba waliamua kuachana na Kopunovic na kusaka kocha mpya baada ya Mserbia huyo kuhitaji Simba imlipe kiasi cha Dola za Marekani 50,000 (Sh milioni 100) kama ada ya usajili na mshahara wake ambapo kila mwezi atakuwa analipwa dola za Marekani 14,000 (Sh milioni 28).
Baada ya kushindwana kwenye malipo ndipo uongozi uliamua kumsaka kocha mpya na kumpata Kerr ambaye inasemekana atalipwa mshahara wa dola za Marekani 9,000 sawa na Sh milioni 18 kwa mwezi.
Dylan Kerr mwenye umri wa miaka 47, aliwahi kuwa mchezaji, alicheza beki wa kulia kwenye klabu za Leeds United, Reading, Blackpool na nyingine nyingi za Uingereza, huku akihudumu kama kocha msaidizi kwenye timu mbalimbali katika nchi za Vietnam ambako ametoka kwenye timu ya Hai Phong F.C. ambako alimaliza mkataba 2014.

Yanga, Villa Taifa leo

KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm amesema anakiandaa kikosi chake kwa ajili ya michuano yote na siyo michuano ya Kombe la Kagame, huku leo akitarajiwa kuikabili SC Villa ya Uganda katika mechi ya kirafiki.
Pluijm alisema anaijua michuano ya Kagame inayoanza Julai 11, mwaka huu, lakini anaichukulia kama mazoezi yatakayowapa nguvu za kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara pamoja na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayoanza mapema mwakani.
“Maandalizi yetu siyo kwa ajili ya Kagame, bali ni michuano yote ambayo inatukabili mbele yetu lengo letu ni kufanya vizuri katika kila michuano ndio maana unaona tumeanza maandalizi mapema na hata zoezi la usajili tumefanya kwa haraka ili tuweze kutimiza kile ambacho tumekidhamiria,” alisema Pluijm.
Alisema anajua timu nyingi zitaka zoshiriki Kagame zitakuwa zimejiandaa kutokana na ubora waliokuwa nao kwa siku za karibuni, lakini hilo halimuumizi kichwa kwani ana matumaini ya kutwaa ubingwa huo na kujiwekea historia nyingine akiwa na Yanga.
Alisema anasema hivyo kwa sababu Yanga ndiyo timu pekee yenye kikosi bora Afrika Mashariki na Kati na hilo atalidhihirisha kwenye michuano ya mwaka huu itakayofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine, Pluijm ameweka wazi kuwa hamtamsajili kiungo Lansana Kamara wa Sierra Leone kutokana na kutoridhishwa na kiwango chake katika mazoezi ya wiki mbili aliyofanya na timu hiyo.
Alisema uwezo wa kiungo huyo hauna tofauti na baadhi ya wachezaji wazawa hivyo ameona nibora akaachana na mchezaji huyo kwa kuwa hana vigezo vya aina ya mchezaji aliyekuwa akimuhitaji kwa ajili ya kuisaidia timu yake katika michuano mikubwa ya Ligi ya Mabingwa watakayoshiriki mapema mwakani.
Katika hatua nyingine, Yanga leo wanashuka dimbani kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam kuchuana na Sports Club Villa ya Uganda ikiwa ni mchezo wa kwa wa kimataifa wa kirafiki.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda atakuwa mgeni rasmi katika pambano la miamba hiyo miwili ya Afrika Mashariki na Kati ambalo litakuwa ni maalumu kwa ajili ya kuwachangia watu wenye mahitaji maalumu.
Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha aliliambia gazeti hili kuwa katika mchezo huo watawashtukiza mashabiki kwa kuwaletea wachezaji ambao hawajaona.
Miongoni mwa wachezaji wanaotarajiwa ni Mzimbabwe Donald Ngoma ambaye Yanga ilimtaja siku za karibuni kuwa ni mchezaji wanayemhitaji.

NEC yaahirisha uandikishaji wa BVR Dar es salaam

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji jijini Dar es salaa pamoja na mkoa wa Pwani kwa kutumia mashine za BVR lililokuwa linategemewa kuanza rasmi tarehe 4.7.2015 jijini Dar es salaam na  25.06.205 kwa mkoa wa Pwani.
 
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo Habari, NEC imesema imeahirisha zoezi hilo kutokana na kuchelewa vifa vya uboreshaji kutoka mikoani ambako zoezi  hilo linaendelea pamoja na vifaa  vilivyokuwa vinakusudiwa kuanza kutumia Dar es salaam kupelekwa katika mikoa ambayo wananchi wamejitokeza kwa idadi kubwa kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.
 
Hata hivyo tume hiyo imewataka wananchi kuwa watulivu wakati vifaa vikisubiriwa kutoka mikoani.
 
Kwa habari zaidi soma hapa taarifa kutoka Tume ya Taifa ya uchaguzi

Mwakyembe, Jaji Ramadhani wagongana Tanga



WAZIRI wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe na Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani, jana walikuwa mkoani Tanga kwa ajili ya kusaka wadhamini ili waweze kukamilisha sharti la kuomba ridhaa ya kugombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza wakati akiwashukuru wanachama wa chama hicho waliojitokeza kumdhamini, Dk Mwakyembe  alizungumzia wingi wa wagombea waliojitokeza kuchukua fomu kwa ajili ya kugombea nafasi ya urais kupitia CCM, akisema umeonyesha ukuaji wa demokrasia.

 “Wenzetu wanatushangaa na wengine wanahoji kwanini nafasi moja inagombewa na watu wengi, lakini niwaambie huku ndio kukua kwa demokrasia ndani ya chama chetu,” alisisitiza Dk. Mwakyembe.

Alisema yeye kwa upande wake anatamani wagombea urais kupitia CCM wafike 50 ili chama kiweze kufanya mchujo ambao utakuwa ni wa haki kwa wanachama wote waliojitokeza katika kinyang’anyiro hicho.

Aidha Mwakyembe alisema ameamua kugombea nafasi hiyo ili kuleta maendeleo, kwani anajua vema changamoto na mafanikio yalipatikana katika serikali ya awamu ya nne.

“Nazijua fursa zilizopo ambazo zitasaidia kutufikisha kwenye mafanikio na maendeleo wakati wa awamu ya tano, hivyo sikuona sababu ya kuingia kinyonge kwenye kinyang’anyiro hicho, kwani mimi ni chaguo sahihi,” alisema.

Kwa upande wake, Jaji Augustino Ramadhani alisema Tanzania si maskini, kwani ina rasilimali nyingi ambazo zikitumika vizuri kwa manufaa ya wananchi zitaleta maendeleo makubwa.

“Ifike mahali wananchi wazinduke pamoja na viongozi rasilimali zilizopo kama madini, utalii, mito na mabonde viwekwe kwenye mfuko wa taifa kwa ajili ya kusaidia watu wote,” alisisitiza.

Aliongeza kuwa nia ya kugombea nafasi hiyo ni kuhakikisha anawatokomeza kabisa maadui watatu, ambao nchi inapambana nao toka enzi ya uhuru, ambao ni umaskini, ujinga na maradhi.

ACT-Wazalendo yalia na rasilimali nchi



CHAMA cha ACT- Wazalendo kimesema kitaleta sera  mahususi na zenye mapinduzi kuhusu utajiri wa nchi unavyopaswa kuwa na faida kwa wananchi wake.

Hayo yalisemwa na Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe, alipokuwa akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Nkanaredi, mkoani Mtwara.

“Tuna utajiri wa madini, mafuta na gesi. Hapa Mtwara ni kituo kiongozi cha harakati za wananchi kufaidi maliasili zao.  Mliumizwa katika harakati hizo muhimu sana za kuhakikisha kuwa utajiri wa nchi unatumika kwa ajili ya wananchi,” alisema.

Alisema Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imetangaza miswada ya sheria ya kurekebisha sekta ya mafuta na gesi, ambapo wamepeleka miswada hiyo bungeni kwa ajili ya kujadiliwa, huku ikiwa haijawahusisha wananchi.

 “Miswada hii ni miswada muhimu sana kuhusu namna utajiri wa mafuta na gesi ya nchi yetu unapaswa kusimamiwa. Serikali imepeleka miswada hii chini ya hati ya dharura. Kama kuna wadau wakubwa katika sekta ya mafuta na gesi hakuna wadau zaidi ya watu wa Mtwara na Lindi.

“Miswada hii inapelekwa bungeni bila kupata maoni yenu. Haikubaliki, ACT Wazalendo inataka miswada hii iondolewe bungeni ije kwa wananchi ipate maoni na kujadiliwa na Bunge la 11 litakalopatikana baada ya uchaguzi mwaka 2015.

“Muswada wa Mafuta umetungwa bila ya kuzingatia mchakato wa Katiba ya nchi. Rasimu ya Katiba imeondoa suala la mafuta na gesi kwenye orodha ya mambo ya Muungano. Sheria iliyopelekwa bungeni inatamka kuwa sheria hiyo itatumika Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar,” alisema.

Zitto alisema muswada wa usimamizi wa mapato ya mafuta na gesi pia umetamka kutumika pande zote za Muungano kinyume na nia ya kuondoa masuala ya mafuta na gesi  katika orodha ya mambo ya Muungano.

“Ni kichekesho na Serikali kuahidi kwa Wazanzibari kuwa mafuta na gesi si suala la Muungano halafu inatunga sheria za mafuta na gesi za kutumika Zanzibar. Miswada hii haikufikiriwa vizuri na hivyo iondolewe."

Alisema muswada wa mapato ya mafuta na gesi imeandikwa haraka haraka na umeacha kabisa kushughulikia suala la mgawo wa mapato ya mrabaha kwa maeneo yenye utajiri huo.

Jk, Babu Seya Kuonana Uso Kwa Uso.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete ‘JK’, leo katika Viwanja vya Chuo cha Magereza ya Ukonga jijini Dar, ana ratiba ya kuzungumza na maafande na maafisa wa jeshi la magereza na wafungwa katika Siku ya Magereza Tanzania 2015 ambayo huadhimishwa kila mwaka.
Kwa mujibu wa chanzo cha ndani ya jeshi hilo, pia Rais Kikwete atatumia nafasi hiyo kuliaga jeshi hilo kwa vile Oktoba, mwaka huu, nchi itamchagua rais atakayepokea kijiti chake cha urais kwa awamu ya tano.
Msingi wa habari hii ni wafungwa wanaotumikia kifungo cha maisha jela kwa makosa ya ulawiti na ubakaji, wanamuziki Nguza Vicking ‘Babu Seya’ na mwanaye, Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ kwani katika hafla kama hiyo, mwaka jana, walimtumia salamu JK wakimwomba awasamehe kwani walishatambua makosa yao.
“Je, rais hawezi kuitumia nafasi hiyo kuwaachia huru wanamuziki, Nguza Vicking na mwanaye, ‘Papii Kocha’ ambao wanatumikia kifungo cha maisha jela?
Chanzo: “Mh! Sina hakika sana. Maana kama hilo lipo ina maana ni jukumu la rais mwenyewe na mipango yake kwa mujibu wa katiba, rais ana mamlaka ya kumsamehe mfungwa kwa kosa lolote lile.”

Mashine ya BVR Yaibiwa Jijini Mwanza, wawili watiwa mbaroni

Watu wasiojulikana usiku wa kuamkia jana, waliiba mashine moja inayotumika kwa ajili ya kuandikishia vitambulisho katika daftari la kudumu la wapiga kura (BVR) katika kata ya Kayenze wilayani Magu mkoa wa Mwanza.
 
Akizungumza na mwandishi wetu, kamanda wa polisi wa mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo, amesema mashine hiyo pamoja na nyingine 13, zilienda kuchajiwa katika nyumba ya kulala wageni ya BM Lodgei, lakini asubuhi zilipofuatwa haikuweza kupatikana.
 
Kamanda Mkumbo amesema baada ya kupata taarifa ya kuibiwa mashine hiyo, msako mkali ulifanyika ukiwamo wa kuwahoji wasimamizi wa mashine hizo.
Anasema baada ya kufanyika msako mkali kwa kuweka vizuizi sehemu mbalimbali, walifanikiwa kuikuta ikiwa imetelekezwa njiani ikiwa salama bila kuharibiwa, lakini hakuna mtu aliyeweza kukamatwa.
 
Hata hivyo, kamanda Mkumbo amesema polisi wamefanikiwa kuwashikilia watu wawili wa nyumba hiyo ya kulala wageni kwa mahojiano ili kufahamu mashine hiyo ilivyoweza kutoweka katika mazingira ya kutatanisha.
 
Aidha, ametoa wito kwa waandikishaji kuwa makini pale wanapohifadhi mashine hizo ili zisiweze kuharibiwa ama kuibiwa na watu wengine.

Mkuu wa Wilaya Akiri "NIMESHINDWA"......Amuomba Rais Kikwete Amfute Kazi

Imeripotiwa kutoka mkoani Simiyu katika Wilaya ya Bariadi kuwa Mkuu wa Wilaya (DC) hiyo Bw. Ponsian Nyami amemuomba Rais Jakaya Kikwete asimwonee huruma na badala yake atengue uteuzi wake kwa maana ameshindwa kusimamia ujenzi wa maabara katika wilaya yake.


Aliyasema hayo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Elaston Mbwilo katika kikao cha majumuisho baada ya kutembelea maabara hizo na kubaini utekelezaji wake ni asilimia 10 tu.

Kabla ya kauli ya Nyami, Mbwilo alitoa lawama kwa DC kwa kushindwa kusimamia ipasavyo agizo la Rais na kueleza kuwa ndani ya Mkoa, Wilaya hiyo ndiyo ya mwisho katika utekelezaji wa agizo husika.

Hata hivyo Mkuu huyo mkoa alisema kuwa viongozi pamoja na watendaji wameshindwa kutekeleza agizo hilo ikiwa pamoja na miundombinu hasa barabara ndani ya wilaya hiyo kuwa chini ya kiwango, ambapo alimtaka Mkuu wa wilaya kuwachukulia hatua watumishi wote walisababisha hali hiyo.

Hata hivyo, Katibu Tawala wa Mkoa naye aliutupia lawama uongozi wa Wilaya hiyo kwa kushindwa uwajibka, huku akieleza kuwa maabara zilizojengwa ziko chini ya kiwango.

Baada ya viongonzi hao kuongea, Mkuu wa Wilaya, Nyami alisema:

“Namuunga mkono Mkuu wa Mkoa na Katibu Tawala Mkoa. Ni kweli tumefanya vibaya, makosa haya ni makosa yangu mimi na wala sina haja ya kuomba msamaha. Niko tayari kuwajibishwa kwa lolote lile na kwa wakati wowote maana nilipoteuliwa nilihaidi kuwa nitaisimamia na kuiheshimu, sasa naona nimeshindwa na usinionee huruma. Nakiri nimeshindwa.”

Nyami alibainisha kuwa yeye kama kiongozi Mkuu ndani ya wilaya hiyo haoni haja ya kuonewa huruma, kutokana na kushindwa kusimamia ujenzi huo ikiwa pamoja na kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Godbless Lema Aahirisha Maandamo Kukutana na Jaji Mutungi



MBUNGE wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema, amesitisha maandamano ya kuishinikiza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuongeza muda katika vituo vya uandikishaji, kufuatia mazungumzo yake na msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi.

Akizungumza jana Arusha na waandishi wa habari, Lema, alisema juzi alipokea ushauri kutoka kwa Jaji Mtungi asitishe maandamano na kuahidi kuja Jijini hapa kufanya kikao na wadau wa vyama vya siasa, pamoja na waandaaji wa zoezi hilo la uandikishaji, ili kuondoa sintofahamu inayoendelea.

Alisema maandamano hayo waliyokuwa wayafanye Juni 25 waliyasitisha kwa barua, baada ya Lema kuongea na Jaji Mtungi, ambaye yeye ni mdau wa jambo hilo, kwa sababu yeye ni mlezi wa vyama vya siasa, ambaye alimuahidi atakuwa Arusha hivi karibuni.

Lema alisema sababu nyingine iliyowafanya waahirishe maandamano hayo ni kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Daudi Ntibenda,aliyoitoa juzi ya kuongeza siku za kuandikishwa, katika kata za Muriet, Olsunyai,Sokoin One, Sinoni na Moshono, ambapo ziliongezwa siku mbili.

Alisema katika siku za nyongeza, wananchi zaidi ya 7,000 wameandikishwa, huku wengine zaidi ya 30,000 wakiwa bado hawajajiandikisha katika kata hizo ambazo zoezi hilo limeisha.

Zoezi hilo Mkoani hapa lilianza katika kata sita ambazo ni Moshono, Terrat, Muriet, Osunyai, Sokoni 1 na Sinoni ambapo kata hizo zilikuwa na jumla ya vituo 55.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Juma Idd mara baada ya siku saba kuisha zoezi hilo, litaendelea Juni 24 katika Kata ya Sekei, Olasiti, Olomoti, Elerai, Sakina na Unga limited, ambapo kutakuwa na jumla ya vituo 44.

Awamu ya tatu itakuwa katika Kata ya Kimandolu, Baraa, Olorien, Themi, Moivaro, Engutoto na Lemara ambapo kutakuwa na jumla ya vituo 55.

Awamu ya Nne ni Kata ya Levolosi, Daraja Mbili, Ngarenaro, Kaloleni, Sombetini na kata ya kati itakayokuwa na vituo 34.

Maamuzi ya Mahakama Kuu Dar kuhusu ishu ya Chenge na ESCROW

Ishu ya ESCROW ni kama kuna watu wengi walianza kuisahau hivi. Jana  imerudi  tena   kwenye masikio ya watu ambapo tunakumbuka kuna orodha ya Mawaziri na Wenyeviti wa Kamati za Bunge walisimamishwa baada ya kutajwa kuhusika na mgao wa Bil. 300 zilizokuwa kwenye account ya ESCROW.
 

Mbunge Andrew Chenge alikuwa mmoja ya waliotajwa kuhusika pia, ishu ikapelekwa Kamati ya Maadili na baadae Mbunge huyo akapeleka ombi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ili kuzuia kuhojiwa na Kamati hiyo.
 
Jana June 26 2015 ripoti kutoka Mahakamani inasema Mahakama hiyo imetupilia mbali Ombi hilo kwa kuwa imeona haikuwa na Mamlaka ya kuzuia Shauri hilo, na walichokiona ni kwamba Chenge alikuwa na njia mbadala kushughulika na ishu hiyo badala ya kukimbilia Mahakamani.
©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved