Yanga, Villa Taifa leo

KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm amesema anakiandaa kikosi chake kwa ajili ya michuano yote na siyo michuano ya Kombe la Kagame, huku leo akitarajiwa kuikabili SC Villa ya Uganda katika mechi ya kirafiki.
Pluijm alisema anaijua michuano ya Kagame inayoanza Julai 11, mwaka huu, lakini anaichukulia kama mazoezi yatakayowapa nguvu za kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara pamoja na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayoanza mapema mwakani.
“Maandalizi yetu siyo kwa ajili ya Kagame, bali ni michuano yote ambayo inatukabili mbele yetu lengo letu ni kufanya vizuri katika kila michuano ndio maana unaona tumeanza maandalizi mapema na hata zoezi la usajili tumefanya kwa haraka ili tuweze kutimiza kile ambacho tumekidhamiria,” alisema Pluijm.
Alisema anajua timu nyingi zitaka zoshiriki Kagame zitakuwa zimejiandaa kutokana na ubora waliokuwa nao kwa siku za karibuni, lakini hilo halimuumizi kichwa kwani ana matumaini ya kutwaa ubingwa huo na kujiwekea historia nyingine akiwa na Yanga.
Alisema anasema hivyo kwa sababu Yanga ndiyo timu pekee yenye kikosi bora Afrika Mashariki na Kati na hilo atalidhihirisha kwenye michuano ya mwaka huu itakayofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine, Pluijm ameweka wazi kuwa hamtamsajili kiungo Lansana Kamara wa Sierra Leone kutokana na kutoridhishwa na kiwango chake katika mazoezi ya wiki mbili aliyofanya na timu hiyo.
Alisema uwezo wa kiungo huyo hauna tofauti na baadhi ya wachezaji wazawa hivyo ameona nibora akaachana na mchezaji huyo kwa kuwa hana vigezo vya aina ya mchezaji aliyekuwa akimuhitaji kwa ajili ya kuisaidia timu yake katika michuano mikubwa ya Ligi ya Mabingwa watakayoshiriki mapema mwakani.
Katika hatua nyingine, Yanga leo wanashuka dimbani kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam kuchuana na Sports Club Villa ya Uganda ikiwa ni mchezo wa kwa wa kimataifa wa kirafiki.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda atakuwa mgeni rasmi katika pambano la miamba hiyo miwili ya Afrika Mashariki na Kati ambalo litakuwa ni maalumu kwa ajili ya kuwachangia watu wenye mahitaji maalumu.
Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha aliliambia gazeti hili kuwa katika mchezo huo watawashtukiza mashabiki kwa kuwaletea wachezaji ambao hawajaona.
Miongoni mwa wachezaji wanaotarajiwa ni Mzimbabwe Donald Ngoma ambaye Yanga ilimtaja siku za karibuni kuwa ni mchezaji wanayemhitaji.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved