BARAZA la Vyama vya Soka Ulaya (UEFA), lipo kwenye njama za kujitoa
katika Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na kuandaa mashindano
pinzani, ikiwa ni jitihada za nguvu za kufanya mageuzi kwa kumwangusha
Sepp Blatter, imeelezwa.
Njama hizo za Uefa zinatokana na rushwa ya Dola za Kimarekani milioni
100 inayoikabili Fifa, zilizolipwa kwa haki ya matangazo ya
televisheni, mikataba ya udhamini na kura wa Kombe la Dunia.
Hongo hiyo inadaiwa ilitumika kufanikisha uenyeji wa fainali za Kombe
la Dunia kwa Russia (2018) na Qatar (2022), huku England na Marekani
zilizoonekana vigogo kwenye uombaji zikitoswa, hadi sasa maofisa saba wa
Fifa wanashikiliwa na vyombo vya usalama vya Marekani kuhusu rushwa
hiyo.
Inaelezwa kuwa Uefa, yenye wanachama 54, imepanga kuandaa mashindano
ya Ulaya kila baada ya miaka miwili na kualika mataifa makubwa mengine
nje ya bara hilo, hiyo yote wakitaka kupambana na kashfa ya rushwa ya
Fifa.
Mpango huo wa kujitoa Fifa ulijadiliwa kwenye mkutano wa Uefa
uliofanyika Ijumaa iliyopita kabla ya Uchaguzi wa Fifa uliomsimika tena
madarakani Blatter (79) kwa awamu ya tano.
Uefa itafanya kikao cha Kamati Tendaji jijini Berlin baadaye wiki hii
na majadiliano yatahusisha nchi zote 54, ambapo watatoka na jambo
jingine kuhusu suala hilo kabla ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya
baina ya Barcelona na Juventus Jumamosi hii.
Wakati huo huo, Waziri wa zamani wa Qatar, Sheikh Hamad bin Jassim
bin Jaber al-Thani, amekana madai kuwa nchi yake ilitoa rushwa kubwa
iliyowafanya kushinda uenyeji wa fainali za Kombe la Dunia 2022.
Alisema madai hayo yametengenezwa na nchi ambazo hazitaki ‘ushindani
wa haki’. “Angalia jinsi zisivyoiongelea Russia, wamekuwa wakiishutumu
Qatar,” aliuambia mtandao wa Fox News juzi.
“Tunaiunga mkono bila shaka Russia, kwa uandaaji wao 2018. Lakini
tunaona mazungumzo …yanaizungumzia Qatar, kwa sababu imetokea kwenye
nchi ndogo ya Kiarabu, nchi ya Kiislamu. Hivyo ndivyo watu
wanavyojisikia.”
Chanzo Mtanzania
No comments:
Post a Comment