Kocha mpya Simba anadi sera zake

KOCHA mpya wa Simba, Muingereza Dylan Kerr amesema ataendeleza wachezaji chipukizi ili kuwa na timu bora kwa sasa na baadaye.
Kerr aliyasema hayo baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kulakiwa na wajumbe wa Kamati ya Simba, Collin Frisch na Said Tully.
“Nimefurahi kuja Tanzania na nawaahidi viongozi na mashabiki kuwa nitahakikisha naendeleza wachezaji chipukizi ili Simba iweze kutamba sasa na baadaye,” alisema Kerr.
Kocha huyo, ambaye amerithi mikoba ya Mserbia Goran Kopunovic, amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuifundisha Simba ambapo atakuwa anasaidiwa na kiungo wa zamani wa timu hiyo, Suleman Matola.
Wakati Kerr akiwasili pia alikutana na kocha mpya wa makipa Idd Salim kutoka Kenya, aliyewasili tayari kwa kazi mpya kwenye klabu ya Simba.
Simba waliamua kuachana na Kopunovic na kusaka kocha mpya baada ya Mserbia huyo kuhitaji Simba imlipe kiasi cha Dola za Marekani 50,000 (Sh milioni 100) kama ada ya usajili na mshahara wake ambapo kila mwezi atakuwa analipwa dola za Marekani 14,000 (Sh milioni 28).
Baada ya kushindwana kwenye malipo ndipo uongozi uliamua kumsaka kocha mpya na kumpata Kerr ambaye inasemekana atalipwa mshahara wa dola za Marekani 9,000 sawa na Sh milioni 18 kwa mwezi.
Dylan Kerr mwenye umri wa miaka 47, aliwahi kuwa mchezaji, alicheza beki wa kulia kwenye klabu za Leeds United, Reading, Blackpool na nyingine nyingi za Uingereza, huku akihudumu kama kocha msaidizi kwenye timu mbalimbali katika nchi za Vietnam ambako ametoka kwenye timu ya Hai Phong F.C. ambako alimaliza mkataba 2014.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved