Gharama za kupima ardhi kupunguzwa

SERIKALI imesema katika mwaka ujao wa fedha itapunguza gharama za upimaji ardhi kwa zaidi ya nusu ili kuwawezesha wanachi kupima maeneo yao, hali ambayo inaonekana itapunguza migogoro ya ardhi.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi wakati wa ziara mkoani hapa kwa ajili ya kutatua migogoro ya ardhi ambayo imedumu kwa miaka mingi.
Akizungumza na watendaji wa sekta mbalimbali wa mkoa wa Tabora, Waziri Lukuvi alisema Wizara itapunguza kwa zaidi ya nusu, gharama za upimaji ardhi ili kila mwananchi aweze kupima eneo lake na kupata hati ya umiliki.
Lukuvi aliongeza kuwa serikali pia itaweza kukusanya kwa wingi kodi ya pango la ardhi, hivyo kuongeza mapato ambayo yataisaidia serikali katika kufanikisha shughuli za maendeleo.
Pamoja na kupunguza gharama hizo, Lukuvi aliwaonya maofisa ardhi kuacha tabia ya kuendesha shughuli za serikali kwa kukiuka taratibu, akitolea mfano wa maofisa hao kupima viwanja juu ya viwanja suala ambalo limekuwa linaleta usumbufu mkubwa kwa wananchi.
“Maofisa ardhi lazima mfanye kazi kwa kuzingatia taratibu ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima ambayo inatokea miongoni mwa wananchi na kuwasababisha kuichukia serikali yao,” alisema Lukuvi.
Alibainisha kwamba mtumishi yeyote wa idara hiyo atakayebainika kukiuka taratibu atashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu na sheria za kazi na zile za nchi.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved