Kumekucha CCM: Baraza la Ushauri la Wazee( Mkapa, Mwinyi na Wengine) Kukutana Wiki Hii Kujadili Jinsi Ya Kumpata Mgombea Urais

Hatimaye kile kikao cha Baraza la Ushauri la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachowahusisha pia marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa, kinatarajiwa kufanyika wakati wowote wiki hii kujadili mwenendo wa mchakato wa kumpata mgombea urais wa Tanzania kupitia chama hicho.

Taarifa kutoka chanzo kimoja ndani ya CCM kimeeleza kuwa Mwinyi, Mkapa na wazee wengine wanaounda Baraza la Wazee la Ushauri, watapasua kichwa wiki hii kujadili mwenendo wa urais ikiwa ni siku chache kabla ya kufikia Julai 2, mwaka huu, inayoonyeshwa katika ratiba ya uchaguzi ya CCM kuwa ndiyo siku ya mwisho ya kurejesha fomu kwa wanaowania urais.

Lengo la kikao cha Wazee ni kujadili kwa kina mwenendo wa mchakato wa kumpata mgombea urais na mwishowe kutoa mapendekezo yao juu ya namna bora ya kumpata mgombea kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM (CC)
 
"Kikao hiki ni muhimu kwa hatma ya mchakato wa uchaguzi... baada ya kutofanyika wiki iliyopita, sasa kitafanyika wiki hii, tena wakati wowote kuanzia kesho (leo)," chanzo kilieleza.

Awali, kikao hicho kilitarajiwa kufanyika Jumatano iliyopita jijini Dar es Salaam lakini kikaahirishwa na Katibu wa Baraza la Ushauri la Wazee, Pius Msekwa, kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni baadhi ya viongozi wakuu wa CCM kuwa safarini.
 
Alipoulizwa  jana iwapo watakutana kaunzia leo, Msekwa hakuwa tayari kueleza kiundani na badala yake alimjibu mwandishi kwa kifupi: "Just pay attention (wee jiweke tayari tu) kama umesikia juu ya kikao chetu."

Kikao cha Baraza la Ushauri la Wazee ni mahususi kwa ajili ya ushauri juu ya watia nia 42 wa urais waliojitokeza kutaka kuteuliwa na CCM kupeperusha bendera yake katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Wanaounda baraza la wazee
Wanaounda Baraza la Ushauri la Wazee kwa mujibu wa mabadiliko yaliyofanywa na CCM mwaka 2012 katika katiba yake ni marais wastaafu Mwinyi (Mwenyekiti), Mkapa (Mjumbe), Amani Abeid Karume (Mjumbe) na Dk. Salmin Amour (Mjumbe).

Wengine ni Waziri Mkuu mstaafu na Makamu wa Kwanza wa Rais, John Malecela (mjumbe) na Pius Msekwa (Katibu).
 
Mkutano huo wa Baraza la Wazee CCM ni utangulizi wa mfululizo wa vikao vingine vya chama hicho vitakavyoanza Julai 5, mwaka huu.

Vikao vingine ambavyo viko katika maandalizi ya kukutana ni Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa itakayokutana Julai 7 na Kamati Kuu (CC) itakayokutana Julai 8, chini ya Rais Kikwete, ikifuatiwa na kikao cha NEC Julai 9, mwaka huu.

Jina la mgombea urais atakayepeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu litajulikana Julai 12 baada ya kupigiwa kura na Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM, ambao ni maalum kwa ajili kuchagua jina la mgombea mmoja kati ya watatu..

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved