Malengo yaliyo nyuma ya pazia ya safari ya rais wa Ufaransa barani Afrika
Usiku wa Ijumaa sawa na tarehe tatu Julai, Rais François Gérard Hollande
wa Ufaransa alimaliza duru ya safari yake barani Afrika kwa kuondoka
mjini Yaoundé, mji mkuu wa Cameroon na kurejea nchini kwake Ufaransa.
Safari yake ya kiduru barani humo, ilianzia nchini Benin, Angola na
kisha Cameroon. Mazungumzo ya Hollande na viongozi wa nchi hizo tatu za
Kiafrika, yalijikita juu ya mahusiano yao katika kupambana na ugaidi,
kuimarisha usalama na kupanua wigo wa kiuchumi na kisiasa. Baada ya
kumalizika kipindi cha ukoloni barani Afrika watawala wa Ufaransa, na
kwa kutumia jumuiya ya nchi zinazozungumza Kifaransa ' Francophone',
waliweza kuendeleza minasaba ya kitamaduni, kiuchumi na kisiasa kama
ilivyokuwa enzi za ukoloni wa zamani barani humo. Pamoja na hayo tajriba
chungu waliyoipata raia wa nchi hizo za Kiafrika zinazozungumza lugha
ya Kifaransa kama vile Benin na Cameroon kutoka kwa wakoloni hao wa
Ulaya dhidi yao, imepelekea kuibua hali ya mpasuko mkubwa baina ya
serikali ya nchi hizo na Paris. Safari ya Rais François Hollande nchini
Cameroon, inahesabiwa kuwa safari ya kwanza rasmi kuwahi kufanywa na
rais wa Ufaransa ndani ya kipindi cha miaka miaka 14 ya hivi karibuni
nchini humo. Weledi wa masuala ya kisiasa wa Afrika wameitaja safari ya
rais huyo wa Ufaransa nchini Cameroon siku ya Ijumaa kuwa yenye maana
ya kufuliwa muhula mpya wa mahusiano ya pande mbili za Yaoundé na Paris.
Mwaka 2001 rais wa wakati huo wa Ufaransa, Jacques René Chirac alifanya
safari nchini Cameroon kwa lengo la kushiriki kikao cha pamoja baina ya
Ufaransa na viongozi wa Afrika na kusisitiza kuwa, nchi mbili hizo
zingeshuhudia uhusiano bora wa kuheshimiana na kuaminiana katika miaka
ya baadaye. Hivi sasa na baada ya kupita miaka 14, Rais François
Hollande amekutana na rais mwenza wa Cameroon Paul Biya na kusisitizia
udharura wa kupambana na kundi la kigaidi la Boko Haram la nchini
Nigeria. Mashambulizi ya kikatili ya kundi hilo la kigaidi na kitakfiri
katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa Nigeria na kupenya kwa
wanachama wake hadi katika nchi jirani kama vile, Niger, Cameroon, Chad
na Benin, kumetoa mwanya kwa serikali ya Paris kwa mara nyingine na
kupitia kauli mbiu yake ya kupambana na ugaidi, kuweza kufungua upya
uhusiano wake na mataifa hayo ya Kiafrika. Hii ni katika hali ambayo
hapo nyumba, viongozi wa nchi hizo jirani na Nigeria, zilikwishaunda
kikosi cha pamoja na kuanzisha operesheni kali zenye lengo la
kulitokomeza kabisa kundi hilo la kigaidi la Boko Haram, operesheni
ambazo zimetajwa kuwa zenye mafanikio. Hakuna shaka kwamba, safari ya
Rais Francois Hollande nchini Benin na kisha Cameroon, ni kuitafutia
nchi yake ubia katika vita hivyo dhidi ya kundi hilo la Boko Haram,
ambalo kwa sasa limegeuka na kuwa tatizo kubwa kwa nchi jirani na
Nigeria. Ni kwa ajili hiyo ndio maana rais huyo wa Ufaransa akatangaza
utayarifu wa Paris kuwa mwenyeji wa kikao cha viongozi wa nchi za
Kiafrika kwa ajili ya kuchukua hatua kali za pamoja dhidi ya kundi hilo.
Ama malengo ya safari ya Francois Hollande nchini Angola ambayo
inazungumza lugha ya Kireno huko kusini mwa bara la Afrika,
inatofautiana sana na safari yake katika nchi za magharibi mwa Afrika.
Angola ni nchi yenye utajiri mwingi wa mafuta ambayo baada ya Nigeria,
inahesabiwa kuwa nchi ya pili mzalishaji wa nishati hiyo muhimu barani
Afrika. Uhusiano wa nchi mbili hizo uliingia doa baada ya serikali
zilizopita za Paris kuziunga mkono harakani za kupigania kujitenga eneo
la Cabinda, kaskazini mwa nchi hiyo. Hata hivyo mahusiano hayo
yaliboreka kufuatia safari ya rais wa zamani wa Ufaransa, Nicolas
Sarkozy nchini Angola hapo mwaka 2008. Aidha Ufaransa inahesabika kuwa
mshirika wa tatu wa Angola kibiashara na hadi sasa imekwishatia saini
mikataba kadhaa ya kibiashara na kiuchumi na serikali ya Luanda. Hivyo
uwekezaji katika sekta ya uwekezaji wa mafuta ndio lengo kuu la safari
ya Rais François Gérard Holland nchini Angola.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment