Bajeti yapita kwa kishindo

BUNGE jana limepitisha kwa kishindo bajeti ya Serikali ya Sh trilioni 22.5 kwa mwaka ujao wa fedha baada ya asilimia 83 ya wabunge kuipigia kura ya ndiyo.
Sambamba na kupitishwa kwa bajeti hiyo, Serikali pia imekubali kubadilisha kiwango cha pensheni kwa wastaafu kutoka Sh 85,000 ilizozipendekeza awali na kuwa Sh 100,000 kwa mwezi.
Marekebisho hayo yametokana na wabunge wengi kutaka kiwango hicho kibadilishwe. Awali, wastaafu walikuwa wakilipwa Sh 50,000 kwa mwezi.
Hata hivyo, Serikali imesisitiza kuwa ushuru mpya wa tozo ya bidhaa za mafuta ya dizeli, taa pamoja na petroli, utabaki kama ilivyopendekezwa kwenye bajeti na viwango hivyo vipya vitaanza kutumia kuanzia Julai mosi.
Miongoni mwa wabunge 219 waliopiga kura ya ndiyo kati ya 294, watatu ni wa vyama vya upinzani akiwemo Hamad Rashid (CUF), John Shibuda (CHADEMA) na John Cheyo (UDP).
Mbunge mmoja aliyekuwemo ukumbini hapo, Saidi Arfi hakusema ndiyo wala hapana, hivyo kuhesabiwa kuwa hakupiga kura kwa kutofanya uamuzi.
Hoja ya Wastaafu Akieleza marekebisho ya kiasi cha pensheni hiyo kwa wastaafu, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum alisema Serikali imetafakari kwa kina hoja za wabunge waliochangia hoja ya kuboreshwa kwa kiwango cha pensheni, hivyo kuridhia kuiongeza kwa asilimia 100 na kwamba kiwango kipya kitaanza kulipwa kuanzia mwaka mpya wa fedha 2015/16 bila usumbufu.
Tozo za Mafuta Kuhusu hoja za utetezi wa kodi ya mafuta ya taa, Waziri huyo alisema ni lazima zilipwe na kila Mtanzania anayeyatumia ili kuiwezesha Serikali kufanikisha mpango wake wa kusambaza umeme katika vijiji vyote nchini kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA).
Kwa mujibu wake, baadhi ya wabunge wamekuwa wakilichukulia suala hilo kuwa mtaji wa kisiasa bila kufahamu kuwa maendeleo ya wananchi yanapaswa kuchangiwa na wananchi wenyewe kwa kujengewa fursa mbalimbali zinazotokana na uwepo wa umeme kwenye maeneo yao.
“Baadhi ya watu wakiwemo wabunge wamekuwa wakilalamika kwamba kuwatoza wananchi Sh 100 katika mafuta ni kuwanyanyasa. Hao hao wamekuwa wakisema kuwa deni la taifa linaongezeka, sasa maendeleo yatafikiwaje endapo kukopa ni tatizo kwa baadhi yenu na kuchangisha wananchi ni tatizo pia?”
“Napenda kuwaeleza kuwa Serikali inafanya mikakati mbalimbali kupunguza deni hilo, ikiwa ni pamoja na kutoza kiasi hicho, kwa kila lita ya mafuta.Ufike wakati tuelezane ukweli na kutofanya kila jambo kuwa siasa, wananchi ni lazima wachangie maendeleo yao,” Mkuya alisema.
Alifafanua kuwa, mafuta ya petroli na dizeli nayo yanatozwa kodi ya kiasi hicho cha Sh 100 kwa lita, hivyo, kuanzisha tozo hilo kwenye mafuta ya taa ni kuweka ulinganifu tu kuwa kila mtanzania achangie japo kidogo.
Kutokana na maelezo yake, Serikali itapata kiasi cha Sh bilioni 276 zitakazokidhi haja kwa mwaka huu mpya wa fedha, kutokana na tozo hiyo itakayotumika kuendeleza miradi ya maendeleo, ambayo ni umeme na maji vijijini.
Alitoa mchanganuo wa matumizi ya fedha hizo kuwa; Sh bil 90 zitapelekwa kwenye mfuko wa maji na Sh bilioni 184, zitapelekwa kwenye mfuko wa REA, kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini.
Katika hatua nyingine, Mkuya alisema maelezo kuwa ongezeko la Sh 100 katika mafuta litawafanya watanzania, hasa walio vijijini waendelee au warudie kukata miti hovyo, kwa ajili ya kuni si ya kweli, kwa sababu, takwimu zinaonesha matumizi ya mafuta hayo yamepungua.
Faida ya umeme Mkuya alisema, watanzania hawana budi kuelewa na kuchangia kiasi hicho wafikishiwe umeme katika vijiji vyao, kwa sababu, ni fursa yenye faida nyingi tofauti na inavyofikiriwa.
Alisema, kwa kuwa na umeme, mtanzania anaweza kuanzisha viwanda na kuajiri watu wengi, huduma za benki zinaweza kusogezwa karibu zaidi na wananchi, pamoja na kuanzishwa kwa huduma nyingine ambazo ni vigumu kuzipata bila kuwa na nishati hiyo.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved