Balozi afurahi Tanzania kupaa kiuchumi duniani

http://www.fullshangweblog.com/wp-content/uploads/2014/09/Screen-Shot-2014-09-17-at-11.21.47-AM.png
BALOZI wa Tanzania nchini Uholanzi, Wilson Masilingi
BALOZI wa Tanzania nchini Uholanzi, Wilson Masilingi ameelezea kufurahishwa na jinsi fursa mbalimbali za kiuchumi zilivyofunguka kiasi cha kuifanya `Dunia’ kuizungumzia Tanzania huku wengine wakitafuta kwa nguvu fursa za uwekezaji.
Aliyasema hayo jana mjini hapa na kuongeza kuwa, ushahidi wa hayo ni jinsi Shirika la Ndege la Uholanzi (KLM) linavyojaza abiria wa kwenda moja kwa moja Dar es Salaam wakitokea katika Jiji la kibiashara la Amsterdam, nchini hapa.
Kila siku, ndege ya KLM husafirisha takribani abiria 400 wanaosafiri kati ya Dar es Salaam na Amsterdam.
Kutokana na hali hiyo, Balozi Masilingi ameelezea kufurahishwa na juhudi za Rais Jakaya Kikwete za kuimarisha uhusiano baina ya Tanzania na mataifa mbalimbali duniani, huku akipongeza kitendo cha kurejesha Ubalozi wa Tanzania nchini hapa uliokuwa umefungwa kwa takribani miaka 20.
“Hakika kwa kuufungua tena ubalozi huu, Serikali imezidi kuongeza chachu ya wawekezaji wanaotaka kuja nchini. Taarifa nyingi wanazipata hapa, huduma za viza zimerahisishwa, ndiyo maana unaona kasi ya wageni kuja Tanzania. Angalia pale KLM, kila siku ndege zao ambazo ni kubwa kabisa zinagombewa na watu wanaotaka kwenda Tanzania. “Hizi ni dalili njema kwa ukuaji uchumi wa nchi yetu. Hiyo ndiyo dhamira ya nchi na pia ya Rais Kikwete ambaye moja ya maagizo yake ni kutaka sisi mabalozi tuzinadi nchi zetu ili watu waje kuwekeza, hii ni kwa faida ya uchumi wetu,” alisema.
Aliongeza kuwa, moja ya maeneo anayoyafanyia kazi ni kuangalia jinsi ya kuimarisha sekta ya kilimo na ufugaji, kwa kujifunza kutoka kwa Waholanzi ambao licha ya nchi yao kuwa ndogo, imepiga hatua kubwa katika kilimo kiasi cha kuwa nchi ya kupigiwa mfano duniani.
“Inawezekana kwa sababu tumetenga mashamba ya mfano kule Sao Hill (Iringa) na Kitulo (Njombe) kwa kutumia utaalamu wa hawa ndugu zetu Waholanzi,” alisema.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved