CCM yatamba kuwavusha Watanzania Uchaguzi Mkuu


https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjUPIhBOEOnkFwToY08PY4S5DpKYcXu5VKu7CvX6Vt-7s1pIKSiqeftwQwUvawYmy452NN4OP96zbh9q5QsYZOZRKedMTcknqOfAxGGC2gl7A_oMf6kpi7oHmNUHp5LaiVPOdZ3tPtv544/s1600/IMG_1017.JPG
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mahamudu Madenge
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mahamudu Madenge, amesema chama hicho kinahitaji mgombea Urais atakayewavusha salama Watanzania katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Alitaja sifa za mgombea anayetakiwa kuwa ni mpenda watu, asiye mbinafsi, mwenye uwezo na anayekubalika na wapiga kura wengi ndani na nje ya chama hicho.
Aliyasema hayo hivi karibuni mjini hapa, mara baada ya kuzindua albamu ya mwimbaji wa nyimbo za injili, Tabitha Massawe, wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God of Tanzania (EAGT) katika hafla iliyohudhuriwa pia na mwimbaji maarufu wa nyimbo hizo nchini, Bahati Bukuku.
Wakati akizindua albamu hiyo ya nyimbo tisa, inayojulikana kwa jina "Yesu ni Commando", Madenge alimchangia mwimbaji huyo Sh milioni moja, alipoelezwa kuwa inahitajika Sh milioni 10 zaidi kusogeza huduma hiyo ya kutangaza injili kwa nyimbo, kwa watu.
Kati ya kiasi hicho kilichoombwa, Sh milioni saba ni kwa ajili ya kulipa gharama za utengenezaji wa albamu hiyo na Sh milioni tatu ni kwa ajili ya kununua kinanda.
Mbali na mchango huo wa Madenge, mamia ya waumini waliojitokeza katika uzinduzi huo walimchangia mwimbaji huyo jumla ya Sh milioni tatu, huku Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu na Bahati Bukuku wakitoa Sh 500,000 kila mmoja.
Huku akiwataka waimbaji hao kutunga na kusambaza nyimbo zitakazosaidia kusisitiza amani, Madenge alisema, Watanzania wanahitaji kuvuka katika uchaguzi huo wakiwa salama, wenye umoja na si vinginevyo. "Lengo ni kuwafanya waishi kwa upendo na utulivu katika maisha yao yote," alisema na kuongeza kuwa nyimbo za injili zina nafasi yake katika kuhakikisha amani inadumu katika jamii.
Alionya kuwa wanaochezea amani ni wale wenye uhakika kuwa baya likitokea watakimbilia katika nchi nyingine pamoja na familia zao. "Tulio wengi nchi yetu ni Tanzania, tunaitaka iendelee kuwa na amani kwa sababu ndipo tunapotegemea kuwepo wakati wote, hatukimbilii kwingine," alisema.
Akizungumzia wagombea Urais wanaoendelea kujitokeza ndani ya chama hicho kutangaza nia na kuchukua fomu za kugombea nafasi hiyo, alisema; “Wala msishangae idadi yao na vijembe wanavyopigana, hiyo ndio demokrasia hasa kwa chama kikubwa kama CCM." Alisema, pamoja na vipaumbele anavyokuja navyo kila mgombea, mwisho wa siku atakayekuwa mgombea na hatimaye kuchaguliwa kuwa Rais wa Tanzania, atalazimika kuitekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Katika hatua nyingine, alieleza kuwa CCM ina uhakika wa kushinda nafasi hiyo ya urais ikiwa ni pamoja na kurudisha kwa chama hicho jimbo la Iringa Mjini linaloshikiliwa na Mchungaji Peter Msigwa, tangu mwaka 2010.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved