Masenza ataka vyama vya siasa vidumishe amani

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza.
MKUU wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza ameviomba vyama vya siasa mkoani hapa vidumishe amani na utulivu, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu ili wananchi waendelee kushikamana kama ilivyo sasa.
Aliyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akifunga kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), kilichofanyika mjini hapa. Alisema anaamini kuwa vyama vya siasa vina uwezo na sababu ya kufanya hivyo, hivyo visirudi nyuma katika kutekeleza jambo hilo.
Kwa mujibu wa Masenza, Watanzania wanaelekea katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani hivyo wanapaswa kushawishiwa waendeleze utulivu walionao na si kuuvuruga kwa sababu ya maneno na chokochoko za wanasiasa na vyama vyao.
"Ninapenda kuwaomba viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa vilivyopo mkoani hapa kuwa hatuhitaji machafuko ya aina yoyote, hasa katika kipindi hiki ambacho wananchi wanapaswa kutulia kutafakari nani anafaa kuweza kuwaongoza.
"Waelezeni wafuasi wenu nao wadumishe amani na utulivu.Tunahitaji Iringa yenye amani hii siku zote na wananchi nchini kote wanafurahia kuwa na utulivu walionao pia,” Masenza alisema.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved