Serikali yapania kuboresha huduma ya maji Karagwe

Mheshimiwa Kassim Majaliwa
NI asilimia 48 tu ya wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe wanapata huduma ya maji, na serikali ipo mbioni kuhakikisha kwamba watu wengi zaidi wanakuwa na uhakika wa kupata maji.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Kassim Majaliwa, wakati akijibu swali la Mbunge wa Karagwe Gosbert Blandes (CCM) aliyetaka kujua utekelezaji wa ahadi ya Rais ya kupeleka maji kwa wananchi wa Karagwe.
Mbunge huyo alitaka kujua mradi huo wa kutoa maji kutoka Ziwa Rwakajunju kama ilivyoahidiwa na Rais mwaka 2013 utaanza na kukamilika lini.
Naibu Waziri Majaliwa alisema kwa kutambua kwamba idadi ya watu wanaopata maji ni ndogo, serikali imeanza kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa mradi wa maji kutoka Ziwa Rwakajunju umbali wa takribani kilomita 35 hadi Makao Makuu ya Wilaya ya Karagwe.
Aidha alisema kwamba mradi huo utahusisha maeneo yote yatakayopitiwa na mradi pamoja na mji wa Kayanga/Omurushaka. Alisema kazi ya upembuzi inafanywa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Maji na Mamlaka ya Maji ya Mji wa Bukoba ambayo imemwajiri Mtaalamu Mshauri.
Kazi hiyo inatarajiwa kukamilika mwaka ujao wa fedha. Mradi huo wa kuchukua maji katika Ziwa Rwakajunju unatarajia kunufaisha mji mdogo wa Kayanga/Omurushaka katika maeneo ya Ndama, Kayanga, Miti, Kagutu, Bujuruga, Kishao Bugene, Nyabwegira, Nyakahanga na Ihanda yenye jumla ya wakazi 81,591.
Vijiji vitakavyonufaika na mradi huo ni pamoja na Rukole, Chonyonyo, Kiruruma, Nyakagoyagoye, Nyamiel, Chabalisa, Sahakishaka, Nyakashenyi, Nyabiyonza, Nyakaiga na Kibondo. Alisema ni azma ya serikali kuhakikisha kwamba ahadi hiyo ya Rais inatekelezwa.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved