Kodi, ada za ardhi zapunguzwa

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEg3JuzbW_dVzTsuWAn2AAkfK0K0aIjh4-3cgzz1mbzjUuaoKi8EUGjTYWxKFXbY5_bUcf9hX1Uh8Xrbp2NoNpJq2EvbyVMJSBsBlPPFCR5_fPUPc6X2L_xuU0yil0cLGG3HeqXFWgAxEaI/s1600/IMG-20141114-WA0005.jpg
Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya MakaziWilliam Lukuvi
SERIKALI imepunguza viwango vya kodi, ada na tozo mbalimbali za ardhi ili kuzifanya ziwe rafiki zaidi kwa wananchi.
Kwa hatua hiyo, wamiliki wote wa ardhi nchini wametakiwa kulipa kodi hizo kwa hiari na kwa wakati kwa kuwa baadhi ya kodi na tozo zimepungua hadi asilimia 30.
Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka 2015/16, Waziri mwenye dhamana ya wizara hiyo, William Lukuvi, alisema jana kuwa hatua hiyo imetokana na ahadi ya wizara hiyo iliyoitoa katika mwaka wa fedha 2014/2015 kwamba itahuisha viwango hivyo.
“Baada ya kuhuisha viwango vya tozo mbalimbali, wananchi wa kipato cha chini watamudu kulipa kodi, tozo na ada hizo,” alisema Lukuvi.
Akifafanua kuhusu kodi hizo zitakazoanza Julai 1 mwaka huu, Lukuvi alisema kodi ya pango la ardhi imepungua kwa wastani wa asilimia 30 na kwamba viwango vingine vinavyomgusa mwananchi wa kawaida vimepungua kwa asilimia 50 au zaidi.
Akiorodhesha namna kodi zilivyopunguzwa, Waziri Lukuvi ambaye alipongezwa na wabunge wengi kwa kazi nzuri aliyofanya katika kipindi kifupi, alisema kodi ya kupima mashamba imepunguzwa kwa asilimia 60 kutoka Sh 1,000 hadi Sh 400 na ile ya mashamba ya biashara imepunguzwa kwa asilimia 50 kutoka Sh 10,000 hadi Sh 5,000 kwa ekari.
Alisema ada ya upimaji ardhi, imepungua kutoka Sh 800,000 hadi Sh 300,000 kwa hekta, sawa na asilimia 62.5 na kwamba tozo ya nyaraka za tahadhari na vizuizi imepunguzwa kutoka Sh 120,000 hadi Sh 40,000.
Gharama pia zimepunguzwa kwenye ubadilishaji wa majina, usajili wa nyaraka, nakala za hukumu kutoka kwenye mabaraza ya ardhi, ada ya maombi ya kumiliki ardhi na ada ya maandalizi ya hati.
Kwa upande wa viwango vya tozo ya mbele, Waziri alisema itapungua kwa asilimia 50 kutoka asilimia 15 ya sasa hadi asilimia 7.5 ya thamani ya ardhi.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved