Mangula ataja vigezo 13 vya urais

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEiFm1FUtVRMOyt8_WsuEROh83mT1BRrbJT3cSERVi54Gn8VI3WJHsAcYWFDFy1A5hSmdhgOIge8_AjDK4AlHL8gjTveNVafBio13FxYWy8yrEEGKgoh8fIWfRJZpqgQ9Hi-0RS23JlO4Qzr/s1600/IMG_7478.JPG
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Philip Mangula
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Philip Mangula amesema vigezo 13, vitatumika kuwachuja wanachama wa chama hicho ambao wameomba kugombea urais CCM.
Alisema hayo jana mjini hapa wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya CCM mjini Dodoma.
Aliwakumbusha watangaza nia kuwa hawaruhusiwi kutoa rushwa, kushawishi au kushawishika kuwapa rushwa wale wanaowadhamini.
Vigezo vyenyewe
Alitaja vigezo 13 vitakavyotumika kuwachuja wagombea kuwa ni uwezo mkubwa na uzoefu katika uongozi, uadilifu, unyenyekevu na busara.
Pia, kuwa na elimu ya chuo kikuu au inayolingana na hiyo, mtu mwenye upeo mkubwa wa kuimarisha na kuendeleza Muungano, umoja na amani.
“Anatakiwa kuwa na upeo mkubwa usiotiliwa mashaka kuhusu masuala ya kimataifa, asiye na hulka ya kidikteta au mfashisti, awe tayari kulinda kanuni, sheria na utawala bora,” alisema Mangula.
Alitaja vigezo vingine ni kuwa mtetezi wa wanyonge na haki za binadamu na asiwe na tamaa ya kujipatia umaarufu, kuzifahamu, kuzitetea, kutekeleza sera na Ilani ya CCM, mpenda haki na ajue kupambana na dhuluma, asiwe mtu anayetumia nafasi ya uongozi kujilimbikizia mali.
“Awe ni mtu makini anayezingatia masuala ya uongozi,” alisema.
Alisema katika kipindi hiki cha mchakato wa uteuzi, kanuni zitakazotumika ni zile Kanuni za Uteuzi wa Wagombea katika Vyombo vya Dola, zilizotolewa na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM ya mwaka 2010.
Pia, katika kipindi hiki cha mchakato wa uteuzi wa wagombea wa CCM katika vyombo vya dola, ni sehemu ya kazi za chama ndani ya chama. Alisema vikao vya uchujaji, vitazingatia pia Kanuni za Uongozi na Maadili Toleo la mwaka 2012.
Alisema kipindi ambacho CCM hudhihirisha dhana ya kazi ya msingi na muhimu katika kujenga uongozi mmoja katika chama, kazi ya kutekeleza kwa dhati kanuni na demokrasia na nidhamu ndani ya chama.
Alisema kanuni hiyo, ndiyo inakiwezesha chama hicho kuwa cha demokrasia na papo hapo kuwa chombo cha kuongoza mapinduzi kutokana na nidhamu yake inayokipa uongozi moja katika vitendo.
Alisema miiko ya shughuli za uchujaji na uteuzi wa wagombea, itazingatiwa. maadili na nidhamu ya chama katika kusimamia na kutekeleza shughuli za uteuzi wa wagombea wa CCM katika vyombo vya dola, lazima vizingate na wale wote wanaohusika.
“Ni mwiko kwa kiongozi yeyote kwa maneno au vitendo kumpendelea au kumsaidia kupata kura nyingi mwombaji mmoja dhidi ya mwingine.”
Alisema Chama kinakataza mgombea kutumia au kuhusisha ukabila, dini, rushwa, rangi, hila na eneo analotoka katika shughuli yoyote ya uchaguzi.
Alisema ni mwiko kwa mgombea kufanya kampeni ya kupakana matope na ya aina nyingine yoyote ile dhidi ya mgombea mwingine.
Aidha, alisema ni mwiko kwa kiongozi yeyote au mwombaji yeyote wa nafasi ya uongozi, aliyekabidhiwa dhamana ya usimamizi, uangalizi, uchujaji na uteuzi, kufanya vitendo vya ukiukaji wa kanuni ambazo ni Katiba ya CCM, sheria, ratiba na taratibu za uteuzi.
Mangula alisema kwa mujibu wa kanuni za uteuzi wa wagombea wa CCM katika vyombo vya dola, kutangaza nia kunaruhusiwa kwa masharti, ikiwemo bila kuathiri haki ya mwanachama ya kutangaza nia wakati wowote nia yake ya kutaka kugombea nafasi fulani ya uongozi katika vyombo vya dola, lakini kwa kuwa nafasi hizo zimewekwa muda maalumu wa miaka mitano.
Alisema wakati wa kutafuta wadhamini 450, kila anachokifanya mwana CCM anayetafuta wadhamini, kitaingia katika kumbukumbu za tathmini ya mgombea mtarajiwa.
Pia, alisema kamati za maadili za wilaya, zikutane mara baada ya wagombea watarajiwa kujaza majina ya wadhamini wilayani. Alisema mpaka sasa wagombea urais waliojiandikisha wamefikia 22 na wengine bado wanakwenda.
Membe akana undugu na Rais Waziri wa Mambo ya Ndani na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amesema hana undugu wa damu na Rais Jakaya Kikwete licha ya kuwa wanafanana kwa sura.
Hata hivyo, alikiri mara kadhaa kufananishwa na kuhusishwa na undugu wa damu na Rais Kikwete. Membe alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) makao makuu mjini baada ya kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya urais kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi.
“Sina undugu wa damu na Rais Kikwete, ni watu tuliofanana tu ; na sioni sababu ya kulificha taifa jambo la kibaiolojia, kama kweli ningekuwa na undugu wa damu na Rais Jakaya Kikwete ningesema tu,” alisema na kuongeza.
“Ingekuwa ni aibu gani kukubali kuwa ni ndugu yangu na kwa nini nifiche jambo hilo, ningepata hasara gani kama mimi na Rais Kikwete ni ndugu wa damu? Alihoji.
Alisema hata Rais Bingu wa Mutharika wa Malawi, aliwahi kumfananisha na Rais Kikwete. “Kuna wakati nilienda safari ilikuwa ni ziara ya kikazi Marekani, nilijikuta nalazimika kupiga picha na zaidi ya watu 160 wakidhani mimi ni Rais wa Tanzania,” alisema.
Membe alisema amechukua sura na rangi kwa mama yake mzazi na Rais Kikwete naye amefanana na mama yake mzazi pia.
Alisema duniani ni wawili wawili, kwani wazazi wake wameshafariki na wazazi wa Rais Kikwete wameshafariki na kuwataka Watanzania kuwaombea na kuwaacha ili marehemu hao wapumzike.
Mahiga ajitosa, kutangaza leo
Mwanadiplomasia maarufu, Balozi Dk Augustine Mahiga leo atatangaza kuwania urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Habari ambazo zilipatikana jana zilieleza kuwa Balozi Mahiga atazungumzia azima yake hiyo kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) saa 4.00 asubuhi.
Tayari mwanadiplomasia huyo, ameshalipa ada ya ukumbi huo, kuashiria kwamba amedhamiria kutangaza azma yake ya kujitosa kwenye kinyang’anyiro hicho ambacho kimewakusanya vigogo wengi wa CCM.
Balozi Mahiga ni miongoni mwa wanadiplomasia wa Tanzania ambao wamefanya kazi kwa miaka mingi katika Umoja wa Mataifa na baadaye akawa mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika suala la mgogoro wa Somalia, wadhifa alioushikilia hadi anastaafu.
Mpina achukua fomu
Mbunge wa Kisesa wilayani Meatu, Luhaga Mpina (CCM) jana alichukua fomu ya kuwania urais na kuwataka Watanzania kuchagua mtu mwenye uwezo kuongoza ; na si kuchagua mtu mwenye jina kubwa.
“Watu wanataka majina makubwa sijui alikuwa waziri mkuu, kikubwa ni kutatua matatizo waliyonayo Watanzania, hapa sio jina kubwa,” alisema.
Alisema kipaumbele chake cha kwanza kitakuwa ni usimamizi wa fedha na mali za umma. Pia, ukusanyaji wa kodi na kuimarisha miundombinu ya elimu, afya na maji.
Alisema hospitali zitakuwa na hadhi na watu hawatakuwa na haja ya kukimbilia hospitali za kulipia. Alisema hata hali za shule sio nzuri na atahakikisha anaboresha sekta ya elimu.
“Unapitisha sera za elimu wakati watoto wenu hawasomi mle,” alisema.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved