Redcross Yatoa Mafunzo Kwa Wanachama Wake Mbeya..

CHAMA cha Msalaba mwekundu nchini (Redcross) kimetoa mafunzo kwa wanachama wake  Mkoani Mbeya ya kujiandaa ili kuweza kukabiliana na dharula mbali mbali zinazojitokeza(EPR).
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mikoa  na Matawi wa Chama cha Msalaba mwekundu, Julius Kejo, alisema mafunzo hayo yanayofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Mbeya Paradise yatadumu kwa muda wa siku nne yenye lengo la kuwakumbusha wananchama kuwa tayari wakati wowote.
Kejo alisema katika mafunzo hayo yaliyojumuisha Wanachama 20 watajifunza Historia ya Msalaba mwekundu duniani, Historia ya msalaba mwekundu Tanzania na shughuli zake, vipaumbele vya msalaba mwekundu pamoja na vitendea kazi vyake.
Alisema Chama cha Msalaba mwekundu Tanzania kilikuwepo tangu kabla ya uhuru lakini kilianzishwa rasmi kwa mujibu wa sheria ya Bunge  namba 71 ya mwaka 1962 ambapo mwaka 1963 Tanzania ilijiunga na Shirikisho la Msalaba mwekundu duniani pamoja na Kamati ya kimataifa.
Alisema dhamira ya Chama cha Msalaba mwekundu nchini ni kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali kwa kutumia nguvu ya ubinadamu kwa ajili ya kuboresha maisha ya watu wenye madhila mbali mbali.
Aliongeza kuwa dira ya Chama hicho ni kuwa na chama imara chenye ubora na kinachotegemewa katika kusaidia serikali kufikia malengo yake ya kijamii, kiuchumi na maendeleo katika kutoa huduma bora za kibinadamu nchini.
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa majukumu ya Chama cha Msalaba mwekundu nchini wakati wa vita ni kusaidia wagonjwa, majeruhi na wafungwa wa kivita na raia wengine walioathiriwa na madhara ya vita pia kushiriki katika shughuli za kuboresha afya ya jamii, kuzuia magonjwa  na kupunguza madhila yake.
Alisema shughuli zingine ni pamoja na kushiriki katika kazi zingine muhimu na zenye manufaa kwa jamii kadri hali inavyojitokeza na namna kadri hali inayoruhusu.
Kwa upande wake mwezeshaji wa mafunzo hayo, Ubwa Suleiman ambaye pia ni Mratibu wa Redcross Zanzibar alisema ni kosa la jinai kwa baadhi ya taasisi kutumia nembo za Chama cha Msalaba mwekundu bila utaratibu.
Alisema nembo za Chama hicho hutumika kutambulisha wakati wa amani na wakati hakuna vita pia hutumika kama ulinzi na kinga ambapo mwenye alama hizo haruhusiwi kushambuliwa wakati wa vita.
Alisema alama zinazotumika na Chama hicho na ambazo hutambuliwa kimataifa ni pamoja na msalaba mwekundu(Redcross), Hilali nyekundu (Red crescent), alama ya jua na samba mwekundu pamoja na alama ya fuele nyekundu(Red crystal).

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved