TIMU ya Taifa ‘Taifa Stars’ jana asubuhi ilionja adha ya kuzomewa na
mashabiki kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam ilipokwenda
kufanya mazoezi kwa ajili ya kujiandaa ma mchezo wa kufuzu fainali za
Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) dhidi ya
Uganda.
Taifa Stars iliwasili uwanjani hapo saa 3:30 asubuhi na kukuta
mashabiki wakiangalia mazoezi ya Yanga iliyokuwa ikijifua kwa ajili ya
maandalizi ya mashindano ya Kagame yanayotarajia kuanza Julai 9.
Baada ya kuwasili meneja wa timu hiyo, Boniface Clemence alianza
kushusha vifaa vya mazoezi na wachezaji kuanza kushuka, mashabiki
walipowaona ndipo wakaanza kupiga kelele za kuzomea, huku wengine
wakiwaita watalii hali iliyofanya kocha kuamuru vifaa virudishwe ndani
ya gari ili kusubiri hali itulie. “Buuuh watalii hao, buuu watalii hao,”
walizomea mashabiki hao.
Kelele hizo ziliongezeka kwani mashabiki waliokuwa kwenye jengo la
Machinga Complex nao walipowaona walizomea zaidi. Baadae zomeazomea hiyo
ilikuja kutulizwa na meneja Clemence pamoja msaidizi wa rais wa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, Juma Matandika
waliowataka mashabiki kuwa wazalendo kwani hiyo ni timu yao ya taifa
hakuna haja kuizomea.
“Jamani mnapozomea haisaidii kwani hii ni timu yetu sote Watanzania,
ni kweli tumefungwa, lakini angalia rekodi ya Misri, hakuna timu ambayo
imekwenda kucheza pale ikatoka bila kufungwa tena kwa idadi kubwa ya
mabao,” alisikika akisema Clemence.
Baada ya hali kuwa shwari wachezaji na benchi la ufundi walitoka
wakaingia uwanjani kuanza mazoezi huku wakipishana na Yanga ambao nao
walikuwepo kwenye Uwanja wa Karume wakifanya mazoezi.
Taifa Stars inatarajiwa kuondoka leo kwenda visiwani Zanzibar kwa
ajili ya mchezo dhidi ya Uganda utakaochezwa keshokutwa Jumamosi kwenye
Uwanja wa Amaan.
Akizungumzia mchezo huo, kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij alisema
anaamini watashinda kwani wachezaji wake wapo vizuri kuanzia mbinu,
akili na morali ipo juu kwani wanajua wana deni kwa Watanzania.
“Naamini tutashinda kwani tumejiandaa kwa ajili ya mchezo huo na
wachezaji wameshasahau yaliyopita tunachoomba ni ushirikiano kwa
Watanzania wote,” alisema Nooij.
Aidha, rais Malinzi amemwambia kocha huyo kuwa akishindwa kuivusha
timu katika michuano ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN), kibarua
chake kitaota mbawa. Baada ya mchezo huo wa Jumamosi, mchezo wa
marudiano dhidi ya Uganda utachezwa Julai 4, mwaka huu nchini Uganda.
Juzi basi la Taifa Stars lilipigwa mawe na mashabiki na kuvunjwa kioo
baada ya timu hiyo kupokea kichapo cha mabao 3-0 na Misri Jumapili
katika mchezo wa kufuzu kwa Afcon 2017.
Timu hiyo ilirejea Jumanne na jana walianza mazoezi kwa ajili ya
maandalizi ya mchezo huo wa Chan. Tangu aanze kuifundisha Taifa Stars,
timu hiyo imecheza mechi 17 na kushinda tatu, sare mechi sita na
kufungwa mara nane.
No comments:
Post a Comment