TIMU za Taifa za soka za wanawake ile ya vijana chini ya umri wa
miaka 20, Tanzanite na ile ya wakubwa Twiga Stars, zipo kambini kwa kwa
wiki mbili ikiwa ni programu maalumu ya kila mwezi ambayo huandaliwa na
Kocha Rogasian Kaijage na kutekelezwa na TFF.
Timu hizo zimeweka kambi kwenye hosteli za Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) na kufanya mazoezi kila siku asubuhi na jioni.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kocha Mkuu wa timu hizo Kaijage, alisema
anafurahi kuona programu yake inatekelezwa japo si kwa kiwango kikubwa
kutokana na timu hizo kukosa wafadhili.
“Wachezaji wapo vizuri na wana ari japo tunakosa kambi nzuri kama
ilivyo kwa timu za wanaume kutokana na timu hizi kukosa wafadhili japo
TFF wanajitahidi kwa upande wake hivyo naomba wadau waone haja ya
kuisaidia timu hizi za wanawake,” alisema Kaijage.
Twiga Stars ina kibarua kigumu cha kupeperusha vema bendera ya Taifa
kwenye mashindano ya wanawake Afrika yatakayofanyika nchini Congo
Brazaville, Septemba mwaka huu na Tanzanite inajiandaa na mchezo wa
kutafuta kufuzu fainali za kombe la dunia kwa vijana wa umri huo dhidi
ya Zambia, mchezo utakaochezwa Julai mwaka huu.
Kwa mujibu wa CAF, timu zitakazochuana pamoja na Twiga ni wenyeji
Congo, Cameroon, Ivory Coast (ambayo imefuzu baada ya Guinea Bissau
kujitoa), Ghana, Misri, Nigeria, Afrika ya Kusini na Tanzania.
Timu hizo zimefuzu baada ya kupata matokeo yafuatayo: Nigeria 8-0
Mali (1-1- matokeo ya mechi ya kwanza), Tanzania 2-3 Zambia (4-2),
Senegal 1-2 Egypt (0-0), Afrika ya Kusini 5-0 Botswana (0-1), Cameroon
2-1 Ethiopia (2-1) na Zimbabwe 2-2 Ghana (1-2).
No comments:
Post a Comment