Basi la Taifa Stars. |
Basi la Stars lilikumbwa na tatizo hilo juzi Jumatatu jioni maeneo ya Kariakoo lilipokuwa likiwapeleka wachezaji wa U-23 kambini kwenye Hoteli ya Tansoma baada ya kutoka kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Karume, Dar.
Mashuhuda walioshuhudia tukio hilo walieleza kwamba, basi hilo lilirushiwa chupa na mawe yaliyosababisha kuvunjika kwa kioo kimoja cha basi lakini zaidi hakuna aliyedhurika.
Chanzo cha vurugu hizo imeelezwa kuwa ni mashabiki wa soka kuchukizwa na kipigo cha Stars dhidi ya Misri.
Inadaiwa kuwa, gari hilo lilipofika maeneo ya Kariakoo, mashabiki kadhaa walianza kuzomea, lilipoendelea mbele zaidi, wengine wakafikia hatua ya kulirushia mawe na chupa.
Wakati huohuo, imefafanuliwa kuwa Stars iliyowasili jana inatarajia kuelekea visiwani Zanzibar siku chache zijazo kwa ajili ya kuweka kambi ya mchezo wao wa kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan) dhidi ya Uganda. Mchezo huo unatarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar Juni 20, mwaka huu.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto, alisema: “Tunashukuru timu imewasili salama na sasa kikosi kipo kwenye mchakato wa kuelekea Zanzibar kwa ajili ya kuweka kambi ya mchezo dhidi ya Uganda utakaopigwa Zanzibar.”
No comments:
Post a Comment