MKUTANO wa 20 wa Bunge la Bajeti kwa mwaka wa fedha 2015/16,
umelazimika kupanga kikao chake kufanyika keshokutwa Jumapili ili kwenda
na ratiba.
Kwa mujibu wa ratiba mpya ya Mkutano huo iliyotolewa jana na Ofisi ya
Bunge, keshokutwa Wizara ya Fedha itawasilisha bajeti yake kuanzia saa
tano asubuhi.
Awali, Wizara ya Fedha ilipangwa kuwasilisha bajeti yake kesho,
lakini ratiba ilivurugika Jumanne wiki hii baada ya kifo cha ghafla cha
Mbunge wa Jimbo la Ukonga mkoani Dar es Salaam, Eugen Mwaiposa (CCM).
Kutokana na kifo hicho, Bunge liliahirishwa Jumanne mchana ikiwa ni
saa chache baada ya kuwasilishwa kwa Bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi
wa Jamii.
Bunge lilirejea jana kwa kipindi cha Maswali ya Kawaida asubuhi bila
kuwapo kwa Maswali ya Papo kwa Hapo kwa Waziri Mkuu na baadaye mjadala
wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii uliendelea hadi jioni.
Leo itakuwa zamu ya Wizara ya Maji na kesho itakuwa Wizara ya Nishati
na Madini, wizara mbili ambazo hotuba zao zilitakiwa kuwasilishwa
Jumatano na Ijumaa.
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambayo hotuba yake
ilipangwa kuwasilishwa jana, sasa itawasilishwa Jumatatu wiki ijayo.
Aidha, ratiba hiyo inaonesha kuwa na siku tatu za Serikali na Kamati
ya Bajeti kufanya majumuisho kuzingatia hoja zenye maslahi kwa Taifa
zilizojitokeza wakati wa kujadili Bajeti za Wizara, sasa zimepunguzwa na
kuwa siku mbili, Jumanne na Jumatano ijayo.
Bajeti ya Serikali itasomwa kama ilivyopangwa Alhamisi ijayo
ikitanguliwa asubuhi na Taarifa ya Hali ya Uchumi itakayosomwa na Waziri
mwenye dhamana ya Mipango.
Chanzo HabariLeo
No comments:
Post a Comment