Wakenya 4 mbaroni kwa wizi wa magari

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Fulgence Ngonyani
POLISI Mkoa wa Kilimanjaro, inawashikilia wezi wanne wa magari akiwamo mwanamke mmoja wote raia wa Kenya, kwa tuhuma za wizi wa gari na kutaka kulificha nchini Tanzania.
Wezi hao wanadaiwa kufanikisha mbinu zao za wizi baada ya kuwanywesha dawa za kulevya wamiliki au madereva wa magari yanayolengwa kuibwa.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Fulgence Ngonyani alisema watuhumiwa hao wamekamatwa Juni 3 saa 1.30 usiku katika eneo la Kamakota katika hifadhi ya taifa ya Mkomazi iliyopo Same.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Lucy Saimon (32), Francis Mtinda (34), Geofrey Matuku (50) na Daniel Muzuki (38) wote wafanyabiashara wa Machakosi nchini Kenya.
Alisema watuhumiwa hao walikamatwa na askari wa doria wakiwa na gari aina ya Nissan URVAG ambayo haina namba za usajili ambayo waliiba nchini Kenya.
Kamanda Ngonyani alisema watuhumiwa hao walikuwa wakitokea Mombasa wakielekea Mnanzi Lushoto wakiwa wamebeba vifaa vya baiskeli, meza na viti viwili vya plastiki.
Aidha Kamanda Ngonyani amesema baada ya mahojiano watuhumiwa hao walikiri kuiba gari hilo baada ya kumuwekea dawa za kulevya dereva wa gari hilo, Masai Mtuku (39) mnamo Juni mosi, mwaka huu saa 2 usiku.
Hata hivyo, Kamanda alisema Mtuka alipata matibabu katika hospitali ya Voi nchini Kenya na hali yake imetajwa kuwa siyo mbaya huku watuhumiwa wakiendelea kuhojiwa kabla ya kufikishwa mahakamani.
Chanzo Habari leo

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved