
Aidha wametakiwa kutotoa fursa kwa baadhi ya wanasiasa watakaotaka kutumia nyumba hizo za ibada kufanya kampeni zao, kwa kuwa nyumba hizo takatifu zipo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.
Akizungumza wakati wa kufungua semina kuhusu majukumu ya kijamii na kisiasa kwa walimu wa madrasa wa mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki alisema, hata kama ni kiongozi wa dini ana chama chake anachokipenda hana nafasi ya kukipigia kampeni katika nyumba za ibada kwani kwa kufanya hivyo italeta mkanganyiko kwa waumini.
“Kama kiongozi wa dini una chama chako, kuna mahala sahihi kwenye majukwaa, lakini si kwenye nyumba za ibada. Kila muumini ana chama chake sasa wewe utakapopiga kampeni ya chama chako unaweza ukakuta waumini wanakimbia au kila mmoja anakuja na sare ya chama chake, hivi itakuwaje?” alihoji Sadiki.
Kwa upande wake, Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Walimu Wasomeshao Quran nchini (JUWAQUTA), alisema, lengo la semina hiyo ni kuwakumbusha walimu hao wajibu wao katika masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Alisema walimu hao ni wadau wakubwa katika masuala ya usalama, upendo, mshikamano wa dini na dini, hivyo serikali iwatazame walimu hao kuwa ni watu wanaohitaji kushirikishwa katika mambo mbalimbali nchini.
Aidha, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Konrad Adenauer Stiftung la Ujerumani, Stefan Reith alisema, wanafanya kazi kwa karibu na Juwaquta hasa katika kuhamasisha masuala ya amani.
Chanzo Habari leo
No comments:
Post a Comment