MICHUANO ya Umoja wa Michezo ya Shule za Sekondari Tanzania
(UMISSETA) Taifa imemalizika jana jijini Mwanza kwa mchezo wa fainali
kati ya Dar es Salaam dhidi ya Nyanda za Juu Kusini wavulana huku
fainali nyingine kwa upande wa wasichana ikipigwa kati ya Dar es Salaam
dhidi ya Kanda ya Mashariki.
Katika fainali ya wasichana, Dar es Salaam walitawazwa mabingwa baada
ya kuwatandika bila huruma Mashariki kwa mabao 7-1 kwenye mchezo
uliokuwa na msisimko mkubwa kwa Dar es Salaam kuonesha uwezo mkubwa.
Dar es Salaam ilitinga fainali baada ya kuisukumiza nje Kanda ya Ziwa
mabao 4-1 huku Mashariki ikitinga katika fainali baada ya kuifunga
Kaskazini kwa mabao 3-1.
Kwa upande wa fainali ya wavulana, Nyanda za Juu Kusini walitawazwa
mabingwa baada ya kuifunga Dar es Salaam bao 1-0, wakijifunga baada ya
mabeki wa Dar es Salaam kujichanganya katika harakati za kuokoa hatari
langoni mwao.
Nyanda za Juu Kusini walitinga fainali baada ya kuifunga Kanda ya
Ziwa kwa mabao 3-0 huku Dar es Salaam wakitinga hatua hiyo baada ya
kuifunga Zanzibar ambao ndio walikuwa mabingwa watetezi kwa mabao 4-3.
Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) chini ya Mwenyekiti wake
Almas Kasongo, kimeelezwa kufurahishwa kwake na mafanikio yaliyooneshwa
na vikosi hivyo vilivyo katika himaya yake.
Imeziomba klabu za ligi mbalimbali kujitokeza kuangalia mashindano ya vijana ili kupata wachezaji wao wa baadaye.
No comments:
Post a Comment