RAIS Jakaya Kikwete ambaye amekuwa katika ziara za kuaga wadau wa
maendeleo, ameendelea kuelezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Nne,
aliyoiongoza kwa miaka kumi sasa katika sekta mbali mbali, ambapo mara
hii amezungumzia mapambano dhidi ya rushwa.
Akizungumza na Watanzania wanaoishi India kwenye Hoteli ya Taj
Palace, amesema Watanzania wamepata uelewa mkubwa wa rushwa na athari
zake baada ya Serikali kuchukua hatua zenye lengo hilo.
“Kuna mwamko mkubwa zaidi kuhusu vita dhidi ya rushwa kwa sababu
Serikali imeongeza sana uwezo wa taasisi zinazoongoza mapambano dhidi ya
rushwa,” alisema Rais Kikwete.
Amesema Serikali iliamua kuchukua hatua nyingi za kujenga uwezo wa
taasisi zinazokabiliana na rushwa nchini Tanzania kwa kiasi kikubwa na
kuweka misingi thabiti ya kisheria ya kukabiliana na jambo hilo.
Moja ya hatua hizo, Rais Kikwete alikumbusha namna Serikali
ilipoazimia kuweka hadharani ripoti za kila mwaka za Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali na kuimarisha Mamlaka ya Ununuzi wa Umma,
ambayo inasimamia matumizi ya karibu asilimia 70 ya fedha zote za
bajeti.
“Tumeimarisha sana uwezo wa Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa), tumeongeza sana nguvu ya PPRA (Mamlaka ya Ununuzi wa Umma).
“Tumepanua uwezo wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) na kuhakikisha kuwa ripoti ya CAG inajadiliwa, tena kwa
uwazi, ndani ya Bunge.
Haya yote yameongeza uelewa na mwamko wa wananchi kupigana kwa nguvu
zaidi na rushwa. “Kisheria vivyo hivyo taasisi hizo zimeongezewa nguvu.
Hata makosa yenyewe ya ulaji rushwa yameongezwa kisheria kutoka manne
ya mwaka 2005 hadi kufikia 24. Hili nalo la sheria limeziongezea
taasisi zetu nguvu ya kufanya kazi ya kukabiliana na rushwa.
Rushwa sasa inatambuliwa kwa urahisi zaidi kuliko zamani,” alisema
Rais Kikwete. Rais Kikwete amesema kazi ya kukabiliana na rushwa haiwezi
kuwa ya mtu mmoja; ya Rais pekee kwa kutoa maagizo na maelekezo, bali
kazi hiyo itafanikiwa vizuri zaidi kama itafanywa na taasisi ambazo
zinazidi kuongezewa nguvu kila wakati.
Matumizi ya dola Akijibu swali kuhusu matumizi ya dola ya Marekani
katika ununuzi wa huduma na bidhaa nchini, Rais Kikwete alisema ni kosa
la jinai kutoza malipo ya huduma mbali mbali nchini kwa fedha za kigeni
na hasa dola. “Kwa wageni sasa, wanakuja na dola zao wakitaka kununua
bidhaa mbali mbali nchini.
Wao kulipa kwa dola ni barabara.” “Lakini kwa Watanzania hapana. Hawa
wanastahili kulipia huduma mbali mbali kwa sarafu ya Tanzania. Huwezi
kumtoza mzazi Mtanzania malipo ya ada ama karo ya mtoto wake katika
fedha za kigeni.
Lakini kwa mgeni, kwa nini tusimtoze kwa dola?” Kuhusu ongezeko la
ajali nchini, Rais Kikwete alisema kuwa ni kweli ajali zimeongezeka
nchini kwa sababu mbalimbali, ikiwamo ongezeko kubwa la magari katika
barabara pamoja na uzembe na ulevi wa madereva.
“Mwaka 2005, Tanzania nzima ilikuwa na magari yaliyokadiriwa kufikia
milioni 1.72. Lakini katika miaka 10 tu iliyopita, yameongezeka magari
milioni 1.5.
Hili ni ongezeko kubwa sana pamoja na jitihada zetu za kujenga na
kupanua barabara zetu nchini. “Ni kweli tunahitaji kupanua barabara
zetu, lakini madereva nao wanachangia sana ajali kwa ulevi na uzembe.
Kwetu pale Chalinze, madereva wa malori wanasimamisha magari makubwa
kunywa pombe, viroba. Baada ya kulewa kabisa ndiyo wanaingia katika
magari yao wakidai kuwa pombe inawaongezea ufanisi wa kuendesha malori.
Upuuzi gani huu?” Alihoji.
No comments:
Post a Comment