HARAKATI
za kuwania ubunge katika Jimbo la Arusha Mjini zimeanza baada ya kada
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mustafa Abdulla Panju, kutangaza rasmi nia
ya kugombea nafasi hiyo akiwa na kauli mbiu ya chagua maendeleo,
usichague soda.
Panju
alitangaza rasmi nia hiyo jana katika mkutano wake na waandishi wa
habari uliofanyika jijini hapa, ambapo aliwataka wanachama wa CCM
kumuamini na kumpa nafasi ili apeperushe bendera ya chama hicho katika
uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Aidha,
alisema ameamua kujitokeza na hana mashaka yoyote kwamba yeye ndiye
mgombea pekee mwenye uwezo wa kumng’oa mbunge wa sasa wa Arusha Mjini,
Godbless Lema (Chadema) kutokana na sifa adhimu pamoja na uzoefu wa
uongozi alionao ndani na nje ya siasa kwa muda mrefu.
“Ninajiamini
nina uwezo wa kulikomboa jimbo, ni haki yangu kama raia wa Tanzania na
uongozi wangu utakuwa shirikishi. Tukishirikiana wananchi ninaamini
tutasukuma mbele gurudumu la maendeleo la wananchi wa Arusha.”
Aliwaasa
wanachama na wagombea wa chama hicho kuungana na kujenga undugu,
upendo, urafiki na mshikamano ili kuepuka kujenga makundi mabaya ndani
ya chama kwa misingi ya udini, ukabila na rangi.
Kada
huyo wa CCM na ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya utalii ya Bushbuck
Safaris ya jijini hapa, alitumia muda huo pia kuwaasa wananchi wa Arusha
kuepuka siasa za vurugu na ugomvi ambazo alisema hazina tija kwao
lakini pia tabia ya wagombea kuchafuana.
No comments:
Post a Comment