WAKATI msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam ukiwa moja
ya changamoto zinazozungumzwa zaidi na watangaza nia ya urais, huku
wengi wakizungumzia ujenzi wa barabara za pete kuwa suluhisho, Rais
Jakaya Kikwete amekuja na wazo jipya na ameanza kulifanyia kazi.
Akizungumza na Serikali ya India, Rais Kikwete amesema suluhisho la
changamoto hiyo, ni ujenzi wa reli katika Jiji la Dar es Salaam, ambapo
ameiomba Serikali hiyo kukubali kugharamia ujenzi huo.
Rais Kikwete ametoa ombi hilo jana asubuhi, wakati alipokutana kwa
mazungumzo rasmi na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, ikiwa ni sehemu
ya shughuli za Rais kwenye ziara yake rasmi ya Kiserikali ya siku nne
nchini India kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Pranad Mukherjee.
Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete amemweleza Waziri Mkuu Modi
namna wingi wa magari ulivyoongeza misongamano mikubwa ya magari na
kupunguza ufanisi wa usafiri kwa wakazi wa jiji hilo, wanaokadiriwa
kufikia milioni nne.
Ingawa amebakia muda mfupi kuondoka madarakani, Rais Kikwete ameiomba
Serikali ya Modi, kufikiria uwezekano wa kugharamia ujenzi wa reli ya
juu ya ardhi, badala ya chini ya ardhi, ili itoe suluhisho la uhakika
zaidi la kupunguza misongano.
Rais Kikwete amemwambia Waziri Mkuu kuwa tayari amezungumza na
Kampuni ya Infrastructure Leasing and Financial Services (IFLS) ya
India, ambayo imeonesha hamu ya kushiriki katika ujenzi wa reli hiyo kwa
nia ya kuongeza ufanisi wa usafiri kwa wakazi wa Dar es Salaam.
Juzi jioni miongoni mwa watu wengine, Rais Kikwete alifanya
mazungumzo na Mwenyekiti wa ILFS, Ravi Parthasarathy kuhusu ujenzi wa
reli hiyo na Mwenyekiti huyo akaonesha hamu kubwa ya kufanya hivyo, ili
mradi Serikali ya India ishauriwe na kukubali kugharamia mradi huo.
Kwa hatua hiyo, Serikali ya Tanzania itakuwa imejiweka katika hatua
nzuri ya kuendeleza mazungumzo hayo na kufanikisha mradi huo, ambayo
tayari yameanzia katika ngazi ya wakuu wa Serikali.
Tayari manufaa ya usafiri wa reli yameshaanza kuonekana wakati wa
uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne, chini ya Rais Kikwete, ambapo
wakazi wengi wa Dar es Salaam, wamekuwa wakiokoa muda kwa kusafiri ndani
ya jiji hilo kwa kutumia usafiri huo, maarufu ‘Treni ya Mwakyembe.’
Nchi ya India, ni miongoni mwa nchi kubwa katika Bara la Asia, ambayo
ripoti za kimataifa zimethibitisha kuwa ukuaji wa uchumi na utajiri
katika nchi hiyo na China, vimechangia Bara la Asia, kupiku Bara la
Ulaya kwa utajiri.
Kwa sasa Bara la Asia ndilo linaloshika nafasi ya pili kwa utajiri
uliotokana na kazi za binadamu, likitanguliwa na Amerika ya Kaskazini
inayoundwa na Marekani na Canada na kufuatiwa na Bara la Ulaya ambalo
sasa ni la tatu, kutoka nafasi ya pili lililokuwepo kwa muda mrefu sasa.
No comments:
Post a Comment