Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe |
Mbeya City iliyomaliza ligi msimu uliopita katika nafasi ya nne, imesema lengo ni kuhakikisha kuwa hairudii makosa ya msimu uliopita kwa kufanya vizuri katika michuano ijayo.
Akizungumza na gazeti hili, Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe alisema siku za karibuni wanatarajia kuwatangaza wachezaji watakaowaacha kulingana na mapendekezo ya kocha wao.
“Tunaangalia mapendekezo ya kocha wetu wakati tukiendelea kuangalia ni aina gani ya wachezaji tutawapata kulingana na kile kilichopendekezwa, mashabiki waendelee kufuatilia siku sio nyingi tutaweka wazi,” alisema Kimbe.
Mbeya City tayari imeshafanya usajili wa wachezaji watatu ambao ni Gideon Brown kutoka Ndanda FC, Haruna Shamte kutoka JKT Ruvu na Joseph Mahundi kutoka Coastal Union.
Wachezaji hao na wengine watakaosajiliwa wanatarajiwa kuziba nafasi zilizoachwa wazi na Deus Kaseke aliyesajiliwa Yanga, Peter Mwalyanzi aliyekwenda Simba na Paul Nonga aliyejiunga na Mwadui FC baada ya mikataba yao kumalizika.
Kuondoka kwa wachezaji hao kuliacha pengo kubwa, kwani wachezaji hao walikuwa wakifanya vizuri katika timu hiyo na kuiwezesha timu kuwa katika nne za juu.
Kimbe alisema anaamini watapata wachezaji wengine wazuri ambao watafanya vizuri zaidi ya walioondoka. Alisema malengo yao msimu ujao ni kuendelea kutisha kwa kufanya vizuri kuanzia mwanzo wa msimu hadi mwisho.
Katika hatua nyingine, mshambuliaji wa Stand United, Abasalim Chidiebele amesaini mkataba wa kuitumikia Coastal Union ya Tanga kwa mkataba wa miaka mmoja katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Chidiebele alisaini makubaliano juzi jijini Tanga ambapo utiliaji saini huo ulishuhudiwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Katibu wa Coastal Union, Kassim El Siagi, Meneja Akida Machai na viongozi wengine.
Akizungumza baada ya kusaini, Chidiebele ambaye ni raia wa Nigeria alisema amefurahi kusajiliwa na Coastal Union na kuahidi kutumia uwezo wake kuipa mafanikio timu hiyo katika Ligi Kuu.
Aling’ara Stand United ambako aliibuka mfungaji bora wao msimu uliomalizika akiwa na mabao 11.
No comments:
Post a Comment