Nape Amshambulia Freeman Mbowe, Amtaka AJIUZULU Maana Amekiabisha Chama Kwa Hukumu Aliyopewa.

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye amemtaka Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe kujiuzulu uenyekiti kwa kile alichosema amekiaibisha chama kwa hukumu aliyopewa hivi karibuni.
 
Mbowe alihukumiwa hivi karibuni kwenda jela mwaka mmoja au kulipa faini ya Sh milioni moja baada ya kutiwa hatiani na mahakama mkoani Kilimanjaro kwa kosa la kumpiga Msimamizi wa Uchaguzi mwaka 2010.
 
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika Kata ya Karumwa, wilayani Nyang’hwale mkoani Geita, Nape alisema miongoni mwa sifa za kiongozi, ni kuzuia hasira na kuwa na kifua kigumu.
 
Alisema kwa kulinda heshima yake na ya chama chake, Mbowe anapaswa kujiuzulu.
 
“Jana (juzi) Mahakama ya Hai mkoani Kilimanjaro ilitoa hukumu ya kumfunga jela mwaka mmoja Mbowe au alipe faini ya Sh milioni moja. Yeye na chama chake waliamua kulipa faini ili asiende jela,” alisema Nape.
 
Akisisitiza kuwa alichofanya Mbowe ni aibu, Nape alisema, “mtu mzima ukiwa umejifunga taulo na mtoto akaja kuichukua hutakiwi kumkimbiza mtoto badala yake unatakiwa kuchutama. 
 
“Ukiamua kumkimbiza mtoto na wewe unaonekana akili yako kama mtoto. Yeye ni kiongozi wa chama, alitakiwa kuonesha uwezo wake kama kiongozi, kutumia hekima na busara dhidi ya msimamizi huyo wa uchaguzi badala ya kumpiga hadharani.”
 
Nape alishutumu siasa za vurugu sanjari na kutumia vijana kwa maslahi ya viongozi wa juu. Alitaja Chadema kwamba kimejijenga kwenye misingi ya ubabe jambo alilotakavijana kuwa macho na kujihadhari na maandamano.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved