MBOZI MASHARIKI: HUDUMA MBOVU ZA KIJAMII BADO NI TATIZO.

Mbozi ni moja kati ya wilaya nane zinazounda Mkoa wa Mbeya. Upande wa kaskazini, imepakana na Wilaya ya Chunya, mashariki kuna Wilaya ya Mbeya Mjini na Ileje, kusini kuna Nchi ya Zambia na magharibi kuna Mkoa wa Rukwa.
Ndani ya wilaya hiyo, kuna majimbo mawili ya uchaguzi, Mbozi Mashariki na Mbozi Magharibi. Mwishoni mwa wiki iliyopita, Uwazi lilifunga safari hadi kwenye Jimbo la Mbozi Mashariki linaloongozwa na Mheshimiwa Godfrey Weston Zambi kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
MATATIZO YA WANANCHI
Katika ziara hiyo, Uwazi lilibaini matatizo mbalimbali yanayowasumbua wananchi, kubwa likiwa ni ubovu wa miundombinu na upatikanaji wa huduma za kijamii.“Maji huku kwetu ni tatizo kubwa, zamani kulikuwa na mabomba ya DANIDA yaliyojengwa kwa msaada wa wahisani, angalau yalikuwa yanatusaidia maji lakini hivi sasa hayatoi tena maji, kwa kweli ni shida sana, tunaomba serikali itusaidie,” alisema Daudi Mgode, mkazi wa Mlowo jimboni humo.
“Shida yetu kubwa ni huduma mbovu za afya. Yaani sisi huku vijijini tunapata sana shida kwa kweli, zahani na vituo vya afya havina dawa wala wauguzi, ukizidiwa mpaka upelekwe Mbozi Mission au kwenye Hospitali ya Wilaya ya Vwawa.
“Kule nako ukifika unaweza kushangaa unaambiwa hakuna dawa, tunaomba serikali itusaidie,”
Kuporomoka kwa bei ya zao la kahawa lililokuwa likilimwa sana jimboni humo, kumesababisha wananchi wengi kuamua kung’oa miti ya zao hilo na kuanza kujishughulisha na kilimo cha mazao mengine, jambo linalotajwa kuwarudisha nyuma wananchi wengi waliokuwa wakitegemea kahawa kama zao la biashara.
“Miaka ya nyuma kahawa ilikuwa inalipa sana, yaani ukiwa na heka zako kadhaa za kahawa, msimu wa mavuno ukifika inakuwa neema kwelikweli. Kilo moja ya kahawa iliyokobolewa ilikuwa inauzwa mpaka shilingi 2,500/= lakini sijui nini kimetokea.
“Siku hizi bei ya kahawa imeporomoka mno mpaka inasikitisha. Mimi mwenyewe nimeshakata miti yote ya kahawa shambani kwangu, naona bora nilime mahindi tu,” Sikudhani Shombe, mkazi wa Londoni jimboni humo aliliambia Uwazi.
Matatizo mengine yaliyolalamikiwa na wananchi ni pamoja na kuchangishwa michango ya mara kwa mara kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na maabara kwenye shule za sekondari za kata.
“Kwa kweli hili suala limekuwa ni mzigo mzito kwetu sisi wananchi, kila siku michango, halafu hata ukiuliza hiyo michango ripoti zake za mapato na matumizi zikoje huwezi kupewa majibu, tunaomba serikali ituangalie sisi wananchi wa hali ya chini,” alisema Getruda Simkoko, mkazi wa Ichenjezya jimboni humo.
Baada ya kusikia malalamiko hayo, Uwazi liliamua kumtafuta Mheshimiwa Zambi ili atoe majibu ya kero zinazowasumbua wapiga kura wake lakini jitihada hizo hazikuzaa matunda baada ya kumkosa ofisini kwake kwa maelezo kuwa alikuwa safarini kikazi.
Hata alipotafutwa kupitia namba za simu zake za kiganjani alizoziorodhesha kwenye Mtandao wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, hakuwa akipatikana hewani. Jitihada za kumtafuta zinaendelea na atakapopatikana atatoa ufafanuzi wa kero za wananchi wake.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved