Milioni 6 waandikishwa vitambulisho vya Taifa

WATU zaidi ya milioni 6.1 wameshaandikishwa kwa ajili ya kupatiwa vitambulisho vya Taifa na kati yao milioni 2.5 wameshapatiwa vitambulisho tangu zoezi hilo lizinduliwe mwezi Februari 2013.


Taarifa ilitolewa na Wakala wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA) wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Vitambulisho vya Kielektroniki, unaofanyika jijini Dar es Salaam.
Akifungua Mkutano wa Kimataifa wa Vitambulisho vya Taifa vya Kielektroniki, Mkurugenzi wa Mfumo wa Kompyuta wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Joseph Makani alisema bado wanaendelea na uandikishaji huo mkoani Tanga.
Makani alitaja mikoa ambayo tayari uandikishaji huo umefanyika na idadi hiyo ya watu kusajiliwa na wengine kupatiwa vitambulisho kuwa ni Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara, Morogoro, Tanga na Visiwani Zanzibar.
“Bado tunaendelea na zoezi la usajili, na utoaji wa vitambulisho hivi na hadi sasa tumeshaona mafanikio ya vitambulisho hivi vya kisasa vya utaifa vilivyo katika mfumo wa kielektroniki hasa katika taasisi za fedha,” alisema Makani.
Aidha Makani alisema NIDA inakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwepo la watu ambao wanakuja kufanyiwa usajili ni vigumu kuwatambua wazawa na wageni.
Akifungua mkutano huo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima alisema kuwa nchi za Afrika zinaweza kukabiliana na vita dhidi ya uhalifu wa ndani, ugaidi, na mambo mengine, endapo tu nchi hizo zitaamua kutumia vitambulisho vya Taifa vilivyo katika mfumo wa kisasa wa kielektroniki.
Silima alisema teknolojia ya utambuzi, itasaidia mataifa mengi Afrika kukabiliana na masuala mbalimbali ya kihalifu, kutambua wafanyakazi na mengine mengi.
Alisema kitambulisho cha Taifa cha Mtanzania, kinaweza kutumika katika mambo mengi na sio tu katika utambuzi pekee, lakini pia kitatumika katika malipo.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved