SERIKALI imetoa kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM)
na Sekondari (MMES) Sh bilioni 13.9 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za
walimu nchini kati ya mwaka 2009 hadi mwaka 2013.
Kati ya fedha hizo, Sh milioni 168.6 zilipelekwa katika Halmashauri zilizopo katika mkoa wa Dar es Salaam.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi), Kassim Majaliwa alisema jana kuwa Serikali kupitia
MMEM na MMES imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za
walimu kwa halmashauri zote.
Aidha, alisema serikali kupitia mpango wa kuboresha makazi kwa
watumishi, imeunda kampuni ya ujenzi wa nyumba za watumishi (Watumishi
Housing Company).
Alisema kampuni hiyo inamilikiwa kwa ubia na mifuko ya hifadhi ya
jamii, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Mfuko wa Taifa wa Bima ya
Afya (NHIF) ambayo inatoa nafuu ya ujenzi kwa nyumba hususan kwa
watumishi wenye kipato cha chini.
“Hivi sasa watumishi wa mikoa 12 wameshaanza kupata huduma hii
ikiwemo Dar es Salaam, Morogoro, Arusha, Lindi na Pwani,” alisema
Majaliwa.
Alisema serikali kupitia mfuko wa mikopo ya nyumba kwa watumishi
uliopo Wizara ya Ardhi inawakopesha watumishi wa umma wakiwemo walimu
fedha za ujenzi kwa riba ya asilimia tatu kwa ajili ya ujenzi wa nyumba.
Naibu Waziri alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Mariam
Kisangi (CCM), lililoulizwa kwa niaba yake na Mbunge wa Masasi, Mariam
Kasembe (CCM).
Katika swali hilo, Kisangi alitaka kufahamu kwa nini serikali isiwape
kipaumbele walimu katika mpango wa kuboresha makazi na isiwaunganishe
moja kwa moja na benki zinazotoa mikopo ya nyumba kwa gharama nafuu.
Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Susan Lyimo
(Chadema), Naibu Waziri alisema kila Halmashauri hupewa Sh milioni 500
kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu nchini na wataendelea kutenga
fedha.
Chanzo Habarileo
No comments:
Post a Comment