Sababu ya kukwama reli Arusha-Musoma yatajwa

UGUNDUZI wa madini ya red nickel pamoja na kilometa 13 zinazohitaji daraja katika Ziwa Victoria, ni miongoni mwa mambo yaliyochelewesha ujenzi wa reli mpya ya kutoka Arusha hadi Musoma, imefahamika.
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta alisema jana kuwa mradi huo umechelewa hasa katika upembuzi na usanifu wake kutokana na sababu hizo na nyinginezo.
Sitta alisema pamoja na hayo, pia iligundulika kuwa reli hiyo ingepita katika mbuga ya Serengeti, jambo ambalo hata hivyo imebidi lisiwepo na sasa itapita mkoani Simiyu.
“Ni kweli upembuzi yakinifu umechukua muda mrefu, lakini zipo sababu nyingi. Kwanza, ilionekana kuwa reli ingepita katika mbuga ya Serengeti, hivyo ikabidi kuipitisha mkoa wa Simiyu,” alisema Sitta.
“Lakini pia katika eneo la Dutwa, tukagundua kuwa kuna madini ya red nickel ambayo yana thamani kubwa sana. Lakini zaidi kuna kilometa 13 ambazo reli inatakiwa kupita juu ya Ziwa Victoria, kwa hiyo kunahitajika daraja la kilometa 13. Haya ndio mambo yaliyojitokeza.”
Sitta alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Umbulla (CCM), aliyehoji kwa nini upembuzi yakinifu na usanifu wa reli hiyo umechukua muda mrefu.
Awali, akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Makilagi (CCM), Naibu Waziri wa Ujenzi Gerson Lwenge, alisema Mshauri Mwelekezi Kampuni ya COWI ya Denmark atakamilisha kazi ya kufanya usanifu wa kiwango cha kimataifa cha reli kutoka Tanga hadi Arusha pamoja na kuunganisha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro mwezi huu.
Aidha, alisema kuhusu reli ya Arusha hadi Musoma, kazi ya upembuzi yanikifu na usanifu wa awali wa ujenzi wa reli hiyo kwa kiwango cha kimataifa inafanywa na Mshauri Mwelekezi H.P.Gauff Ingenieure Consultant ya Ujerumani.
“Kazi ya usanifu inatarajiwa kukamilika Oktoba mwaka huu,” alisema Naibu Waziri akijibu swali hilo lililoulizwa na Umbulla kwa niaba ya Makilagi.
Kuhusu ujenzi wa bandari ya Mwambani Tanga, alisema zabuni ilitangazwa Machi 27, 2014, lakini hadi siku ya ufunguzi Juni 27, 2014, hakukuwa na mzabuni yeyote aliyejitokeza kuleta zabuni yake.
“Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania inakamilisha taratibu mpya za kuutangaza mradi huu ili kuyapata makampuni yenye nia ya kuendeleza mradi,” alisema Naibu Waziri wa Ujenzi.
Katika maswali yake, Makilagi alitaka kufahamu lini serikali itajenga reli hiyo ya Arusha hadi Musoma na bandari ya Mwambani mkoani Tanga.
Chanzo habarileo

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved