SERIKALI leo inatazamiwa kujibu hoja mbalimbali zilizoibuka wakati wa mjadala wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2015/16.
Mbali na Wizara ya Fedha ambayo itakuwa na mengi ya kufafanua au
kurekebisha kutokana na mapendezo yake mbalimbali yaliyomo kwenye
Bajeti, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Dk Mary
Nagu, naye atakuwa na ‘kibarua’ cha kujibu hoja za wabunge kutokana na
taarifa yake ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa katika mwaka ujao wa fedha
alioiwasilisha bungeni siku ambayo Bajeti ilisomwa, Juni 11, mwaka huu.
Moja ya hoja inayotarajiwa kutolewa ufafanuzi au kufanyiwa
marekebisho na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya pamoja na manaibu wake,
Adamu Malima na Mwigulu Nchemba kabla ya Bejeti ya Serikali kupitishwa
kwa kupigiwa kura, ni ongezeko la tozo ya nishati ya mafuta.
Katika bajeti ijayo, Serikali inapendekeza kuongeza tozo ya mafuta ya
dizeli kutoka Sh 50 kwa lita hadi Sh 100 kwa lita; petroli kutoka Sh 50
hadi Sh 100 kwa lita na mafuta ya taa kutoka Sh 50 kwa lita hadi Sh
150. Kuhusu mafuta ya taa ilielezwa kwamba ongezeko hilo litasaidia pia
kuondoa uchakachuaji.
Tozo hiyo ambayo fedha zitakazopatikana zinatarajiwa kupelekwa kwenye
Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini (REA) iliwagawa wabunge katika
makundi mawili; moja likiipinga na lingine likiiunga mkono.
Wale wanaopinga wanasema itaongeza mzigo kwa wananchi kwa kuwa
nishati hizo zinapoguswa zina athari nyingi za kuendelea lakini wale
wanaounga mkono tozo hiyo wanasema ni ndogo kulinganisha na umuhimu wake
na kwamba maendeleo hayawezi kuja bila kuyatolea jasho. Suala la
nyongeza pensheni nalo linatarajiwa kutolewa ufafanuzi wa Wizara.
Serikali katika mwaka ujao wa fedha inapendekeza kiwango cha pensheni
kupanda kutoka Sh 50,000 za sasa hadi Sh 85,000. Hata hivyo, wabunge
wengi walitaka kiwango hicho kiongezeke hadi kufikia Sh 100,000 au zaidi
huku wachache wakisema hizo zilizopendekezwa zinatosha.
Wizara hiyo ya Fedha pia itajaribu kujibu hoja kwamba bado kuna
vyanzo vya mapato vingi kama uvuvi kwenye bahari kuu ambako tumeshindwa
kwenda na kwamba kwenye migodi na utalii tungeweza kupata mapato mengi
zaidi kuliko ilivyo sasa.
Wizara hiyo pia itajaribu kueleza namna itakavyodhibiti matumizi
katika mwaka ujao wa fedha kwani baadhi ya wabunge walilalamikia
kukosekana kwa nidhamu ya pesa kwenye taasisi nyingi za umma huku hatua
za kuwawajibisha watuhumiwa zikiwa legelege.
Mbali na mikakati iliyopo katika kuimarisha Shilingi, serikali
itatakiwa pia kujibu namna takavyoshughulikia madeni yake kama vile
makandarasi, mifuko ya hifadhi ya jamii hadi wakulima wanaoidai serikali
takribani Sh bilioni 22.
Waziri Nagu naye atatakiwa kujibu hoja kwamba ingawa uchumi
unaonekana kukua kwa asilimia 7 na hivyo kuifanya Tanzania kuwa kati
nchi 20 duniani zenye mwelekeo mzuri wa uchumi, hali hiyo haijitafsiri
vyema katika mifuko ya wananchi.
Wizara ya Viwanda nayo, kati ya hoja kadhaa zilizoelekezwa huko,
italazimika kueleza ni jinsi gani imejizatiti katika kuimarisha viwanda
nchini na kuhamasisha wawekezaji zaidi wa viwanda vya kuzalisha bidhaa
zenye uhitaji mkubwa nchini kama pikipiki na bajaji na hivyo kukuza
uchumi na kutengeneza ajira zaidi.
Baadhi ya wabunge walikuwa na hoja kwamba ni wakati sasa wa
kuimarisha na kujenga viwanda nchini, ili tusiendelee kuwa nchi ya
kuagiza kila kitu hadi madodoki, hali ambayo inatufanya tuhitaji sana
matumizi ya dola na hivyo kuyumbisha thamani ya Shilingi yetu.
Wizara ya Kilimo nayo itatakiwa kujibu hoja zilizoelekezwa kwake,
hususani namna itakavyojipanga kuhakikisha Tanzania inakuza kilimo chake
ikiwa ni pamoja na kuuza mchele katika nchi jirani ikiwemo Kenya ambayo
inapeleka pesa zake za kigeni Pakistan ili kupata zaidi ya kilo laki
mbili za mchele kila mwaka.
Wakati karibu kila wizara iliguswa na mjadala, Ofisi ya Waziri Mkuu
pia itatakiwa kujibu namna itakavyosimamia ulipaji wa fidia kwa
halmashauri zilizopata ‘maafa’ kama ile ya Masasi iliyochomwa moto na
wahuni pamoja na upatikanaji wa rasilimali fedha katika halmashauri
mbalimbali nchini utakaokuwa unakwenda kwa wakati.
Wakati akiahirisha Bunge Ijumaa iliyopita, Sipika Anne Makinda
alivitaka vyama vyote vya siasa kuhakikisha wabunge wao wanakuwepo leo
ili kusikia majibu ya serikali. Wiki iliyopita wakati wa majadiliano ya
Bajeti ya Serikali na Hali ya Uchumi kulikuwa na mahudhurio
yasiyoridhisha ya wabunge na mawaziri.
No comments:
Post a Comment