Wa urais CCM sasa wafikia 40

KATIKA hali isiyo ya kawaida, kada anayeomba nafasi ya kuwania kuteuliwa na CCM kuwa mgombea wa urais wa chama hicho, Helena Elinewinga jana alichukua fomu huku akikataa kuzungumza na waandishi wa habari.
Anakuwa mwanachama wa 40 wa CCM kuchukua fomu kwa ajili ya kuwania kuteuliwa, huku akiwa mwanamke wa sita kuchukua fomu.
Ametanguliwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro, Balozi wa Umoja wa Afrika (AU) nchini Marekani, Amina Salum Ally, aliyekuwa Mbunge wa Iringa na Naibu Waziri wa Fedha wa zamani, Monica Mbega, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk Mwele Malecela na Ritha Ngowi.
Akiwa amevalia suruali nyeusi, shati la rangi ya zambarau na kubeba mfuko ulioshonwa kwa kitambaa cha kitenge na kuvaa kofia yenye rangi ya bendera ya taifa, alipotakiwa kuvua kofia ili aonekane vizuri kwenye picha alikataa kufanya hivyo.
Mara baada ya kutoka kuchukua fomu na kupelekwa moja kwa moja kwenye chumba cha mkutano kwa ajili ya kuzungumza na waandishi wa habari, alikataa kuzungumza kwa kile alichoeleza hayuko tayari kuzungumza na waandishi wa habari.
Kutokana na hali hiyo ilibidi waandishi wa habari wamzunguke ili kumhoji. Alipohojiwa kwa nini alikataa kuvua kofia alisema hakuwa amechana nywele zake vizuri.
Pia alipohojiwa akiwa kama mwanachama wa CCM ambaye amekuja kuchukua fomu kwa ajili ya kuwania kiti cha ukuu wa nchi, jambo gani lililofanya ashindwe kuvaa sare za chama, alisema nguo ni nguo na kila nguo ina hadhi yake.
Kutokana na hali hiyo, wengi walivutika na kutaka kufahamu kulikoni, hali iliyofanya mgombea huyo kuzingirwa na watu wengi hali iliyolazimu kubaki kwanza ndani ambapo baada ya watu waliomzunguka kupungua ndipo alipotoka nje.
Akizungumza huku akicheka mara kwa mara huku akizungumza kwa lugha ya Kiswahili na wakati mwingine kuzungumza kwa Kiingereza, alisema umri wake ni miaka 40 na amesoma shule ya msingi na sekondari katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, kisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye Marekani kwa ajili ya masomo zaidi.
“Chukueni vipeperushi hivi nimekuja navyo vingi tu,” alisema huku akitoa vipeperushi ambavyo vilikuwa havihusiani kabisa na nafasi aliyoomba au wasifu wake kama ilivyo kwa wagombea wengine.
Alipohojiwa zaidi alisema mkakati wake mkubwa utakuwa ni kupambana na adhabu za vifo. Alipohojiwa kama siku saba zinatosha kutafuta wadhamini katika mikoa 15 alisema atajitahidi.
Aidha alisema yeye ni mtafiti wa kilimo ambaye anashirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA).

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved