JK: Sifa yangu ni kutekeleza ahadi.

  HUKU akikaribia kukabidhi madaraka kwa Rais wa Awamu ya Tano baadaye mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete amesema moja ya sifa yake na ya chama tawala, CCM, ni kutekeleza ahadi walizowaahidi Watanzania wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2010.
Amesema ahadi nyingi alizowaahidi wananchi ambazo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, zimetekelezwa. Aidha, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli alisema utawala wa Rais Kikwete umekuwa na mafanikio makubwa kwenye sekta ya ujenzi.
Amesema katika kipindi cha miaka 10, serikali imenunua vivuko vipya 15 na kukarabati vivuko saba na kwamba hayo yote yamefanikiwa kwa kuwa Watanzania walimuamini Rais Kikwete na kumpa nafasi ya kutekeleza ahadi kwa vitendo. Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, aliyasema hayo jana mjini hapa wakati akizindua kivuko cha Mv Mafanikio kinachofanya safari zake kati ya Mtwara na Msangamkuu.
Alisema wakati wa kampeni mwaka 2010, aliwaahidi wananchi wa Msangamkuu kuwapatia kivuko ambapo ahadi hiyo imetekelezwa. “Hiyo ndio sifa yangu pamoja na chama chetu, tunapoahidi tunatekeleza kwa vitendo na leo hii wananchi wa Msangamkuu wameondokewa na kero ya usafiri waliokuwa wanapata,” alisema.
Alisema kivuko hicho ni fursa nzuri kwa kukuza uchumi wa wananchi na amewataka waitumie vizuri fursa hiyo. Rais Kikwete alisema wananchi wa Msangamkuu walikuwa wanapata shida ya usafiri na kwamba walikuwa wanalazimika kuzunguka umbali wa kilomita 21 hadi kufika Mtwara mjini, hivyo adha hiyo kwa sasa itakuwa historia.
Kwa upande wake, Dk Magufuli alisema katika kipindi cha miaka 10 ya utawala wa Rais Kikwete amefanikiwa kununua vivuko vipya 15 na kukarabati saba ambavyo hivi sasa vinafanya kazi kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Alisema tangu serikali ya awamu ya kwanza mpaka serikali ya awamu ya tatu, kulikuwa na vivuko 13 na kwamba hivi sasa vipo zaidi ya 28. “Hatuna budi kukushukuru Mheshimiwa Rais kwa kuboresha huduma mbalimbali za usafiri, utawala wako umeweza kununua vivuko vipya 15 na kukarabati saba hilo si jambo dogo, tunakushukuru sana na rais ajae ataendeleza zaidi ya hapo ulipoishia,” alisema huku akishangiliwa na mamia ya wananchi waliojitokeza.
Alisema kivuko hicho kimegharimu Sh bilioni 3.3, ambazo zimetolewa na serikali. Dk Magufuli ambaye ni mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, alisema wanafunzi na walemavu watavuka bure katika kivuko hicho na kwamba watu wazima watalipia Sh 300, watoto Sh 100.
Dk Magufuli alisema Rais Kikwete aliahidi barabara kutoka Dar es Salaam mpaka Mtwara ambayo hivi sasa imekamilika. “Watanzania wana kila sababu ya kukushukuru Rais Kikwete umewafanyia mambo mengi, wewe ni kiongozi mwenye upendo, imani na kubwa zaidi umetekeleza kwa vitendo uliyoahidi,” alisema.
Aidha alitumia fursa hiyo kujitambulisha kwa wananchi waliojitokeza kwa wingi kuwa ndiye mgombea urais wa CCM. Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Marcelin Magessa, alisema mkoa wa Mtwara kuna vivuko viwili kikiwemo cha Mv Kilambo na Mv Mafanikio.
Alisema kivuko cha Mv Mafanikio kilitengenezwa na mkandarasi wa hapa nchini na kwamba kilianza kutoa huduma mwaka jana. Alisema kivuko hicho kina uwezo wa kubeba abiria 100, tani 50 na magari matatu kwa wakati mmoja.
Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia, alisema wananchi walikuwa wakipata shida ya usafi ambapo baadhi yao walipoteza maisha kutokana na kukosa usafiri wa uhakika. Alisema ujenzi wa kivuko hicho unatokana na juhudi kubwa zilizofanywa na Dk Magufuli na kwamba wananchi wa jimbo hilo wanampongeza.
Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendegu, alisema kata ya Msangamkuu ina wakazi zaidi ya 1,200, ambapo kivuko hicho ni mkombozi mkubwa kwa wakazi hao. Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mussa Iyombe, wabunge na wananchi ambao walijitokeza kwa wingi.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved