Pinda avunja ukimya alivyokatwa Dodoma

  WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, amesema hawezi kuhama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuwataka waliohama baada ya kubwagwa kwenye kinyang’anyiro cha kugombea urais, kujiuliza iwapo wataihama nchi wakishindwa kufanikisha malengo yao huko walikohamia.
Pinda alisema hayo jana alipohutubia wakazi wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, alipokuwa akifunga maonesho ya wakulima ya Nanenane kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.
Alisema wakati wa mchakato wa kura za maoni, kila mmoja alipokuwa akizunguka mikoani kusaka wadhamini, alikuwa akiamini yeye ndiye anayeweza kupita, lakini hatimaye wachache walivuka hatua ya kwanza na wengine kuachwa nje na hatimaye mwisho akapatikana mmoja anayefaa zaidi.
Alisema haikuwa kosa kwa mmoja kati ya wagombea 38 waliorejesha fomu kupewa nafasi hiyo, kwa kuwa chama kiliamini anafaa na hivyo kinachopaswa kufanyika na makada wengine, ni kuendeleza chama ili kishinde kwa kishindo.
“Tulijitokeza wengi kuchukua fomu, watatu wakashindwa kurejesha fomu, wakawa wamejitoa wenyewe. Tulibaki thelathini na nane tuliorejesha fomu na kati ya hao wapo waliopita na wengine wakawekwa pembeni. “Mimi pia nikawekwa pembeni. Ninaamini kazi tuliyokwenda kuifanya tumeifanya vizuri, tena vizuri sana. “Sasa hapa katikati nilikaa kimya kidogo, watu wakaanza kusema kwenye mitandao… Oooh mbona mzee kimya! Au naye anataka kuhamia kule. Sasa niseme nimeachwa huku kwa hiyo nifanyaje? Nihame niende wapi? Hivi ukihama huku huko unakohamia ukishindwa utahamia wapi tena? Au ndiyo utahama nchi? “Wana uhakika gani na huko wanakohamia? Mbona nako kila siku tunasikia ya kusikia. Mivutano haiishi. Kila siku tunaona mambo. Tutabanana hapahapa, kama ni kusahihishana tutasahihishana humu humu,” alisema.
Hahami
Alisema hana mpango wowote wa kuacha chama hicho kwa kuwa amekulia humo na manufaa mengi ameyapata kupitia chama hicho, ikiwemo madaraka ya uwaziri mkuu kwa miaka nane.
Pinda alisema hataki kuwa miongoni mwa makada wachache wa chama hicho waliohama na kusahau mema waliyofanyiwa, huku akisema watu hao wametimiza usemi wa ‘Asiyeshukuru ni Kafiri’.
Aliwataka Watanzania kutodanganyika na viongozi wachache wenye uchu wa madaraka, wanaoshawishi kutokubaliana na mambo mazuri yanayofanywa na Serikali na badala yake wajiulize ni akina nani hao wanaotaka kuvuruga Taifa?
Waziri Mkuu alisema CCM ina Ilani yenye sera nzuri, na ndicho chama kinachopaswa kuaminiwa na Watanzania katika Uchaguzi Mkuu ujao na kuthibitisha kuwa anayo imani na sera ya CCM, hana mashaka kuwa chama hicho kitapata ushindi mnono kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Waziri Mkuu huyo alipongeza jitihada zinazofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini (NEC) katika maandalizi ya Uchaguzi Mkuu, ikiwemo uandikishaji wapigakura ambao wamevuka malengo yaliyowekwa awali.
Alisema licha ya changamoto nyingi zilizoibuka tangu kuanza kwa uandikishaji wapiga kura nchini kupitia mashine za Biometric Voters Register (BVR), Tume imeandikisha zaidi ya wapiga kura milioni 24 na imevuka malengo yaliyowekwa awali.
*Nyuki wavamia
Katika hatua nyingine, nusura shughuli ya kufunga maonesho ya wakulima ya Nanenane Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ndani ya viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, iharibike baada ya kutokea kwa kundi la nyuki waliovamia katika uwanja huo.
Nyuki hao walivamia eneo la Banda Kuu la mikutano ndani ya viwanja vya John Mwakangale, wakati shamrashamra za kufunga maonesho hayo zikiendelea.
Nyuki hao waliokuwa wakisafiri, walifika sehemu hiyo wakitokea upande wa Kusini Mashariki mwa Uwanja na baada ya kufika hapo umati wa wananchi ulipata wakati mgumu kwani wapo baadhi ya watu ambao walianza kuhaha kwa kulala chini, huku wengine wakibaki wameduwaa wasijue la kufanya.
Waandishi wa habari waliokuwa mashariki mwa jukwaa kuu, ni miongoni mwa watu waliolazimika kuinama kwenye kichumba kidogo kusubiri kwa muda mpaka nyuki hao walipoondoka.
Baada ya nyuki hao kupita, mwongozaji wa shughuli hiyo, Charles Mwakipesile alimtania Pinda kuwa nyuki hao walipita kumsabahi rafiki yao, kwa kuwa wanatambua kuwa amekuwa mstari wa mbele kupigania maisha yao kutokana na faida kubwa walizo nazo kwa binadamu.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved